Ahadi mpya ya Taliban kuhusu elimu ya wasichana
https://parstoday.ir/sw/news/world-i95708-ahadi_mpya_ya_taliban_kuhusu_elimu_ya_wasichana
Sher Mohammad Abbas Stanikzai, naibu waziri wa mambo ya nje wa serikali ya Taliban akiwa safarini katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) amezungumzia marufuku ya elimu kwa wasichana Waafghanistani na kusema milango ya elimu haipaswi kufungiwa yeyote.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 31, 2023 02:09 UTC
  • Ahadi mpya ya Taliban kuhusu elimu ya wasichana

Sher Mohammad Abbas Stanikzai, naibu waziri wa mambo ya nje wa serikali ya Taliban akiwa safarini katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) amezungumzia marufuku ya elimu kwa wasichana Waafghanistani na kusema milango ya elimu haipaswi kufungiwa yeyote.

Aidha amesema elimu ni haki ya kila mtu, awe ni mwanaume au mwanamke na kuongeza kuwa ni wajibu kwa wote kupata elimu. A,esisitiza kuwa Taliban inajaribu kushughulikia tatizo la elimu ya wasichana na kuwaruhusu kuendelea na masomo. Akiashiria kwamba serikali ya Taliban ya Afghanistan haijatangaza kwa yakini kwamba inapinga elimu kwa wasichana na wanawake, Stanikzai amesisitiza kwamba: "Huu ni uamuzi wa muda, idadi kubwa ya wasomi wa Kiislamu wa Afghanistan wanaamini kuwa wanawake na wasichana wanapaswa kuruhusiwa kwenda shuleni kusoma."

Katika ziara ya hivi majuzi ya ujumbe wa UAE nchini Afghanistan, msimamo kama huo kuhusu elimu ya wasichana ulitolewa na Taliban. Kubadilika msimamo wa Taliban kuhusu kadhia ya elimu ni muhimu kwa mitazamo kadhaa.

Kwanza, mashinikizo ya kikanda na kimataifa yameongezeka kwa utawala wa Taliban uruhusu wasichana waendelee kusoma. 

Pili, UAE na Saudi Arabia, nchi mbili za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi, ndizo waungaji mkono wakuu wa utawala wa Taliban nchini Afghanistan, na kidhahiri nchi hizo zinataka wasichana wa Afghanistan waendelee kusoma. Gholam Hossein Naseri, mtaalamu wa masuala ya elimu na jamii nchini Afghanistan anazungumzia nukta hiyo kwa kusema: "Taliban wameahidi mara kadhaa katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu kwamba elimu ya wasichana itaendelea, lakini hawajachukua hatua yoyote ya kivitendo kuhusu kadhia hii. Inaonekana kwamba kupinga kuendelea masomo ya wasichana bado ni tatizo sugu."

Inaelekea kuwa kuna misingi ya kiitikadi katika msimamo wa Taliban wa kupinga wasichana kuendelea na elimu na huu ni msimamo ambao umekuwepo katika  miongo miwili iliyopita. Matamshi ya Stanikzai kwamba hakuna sababu ya Kiislamu ya kuwafungia wasichana shule, na kwamba wasomi wote wa Afghanistan wanakubali kwamba wasichana wanapaswa kuruhusiwa kuendelea na masomo haraka iwezekanavyo ni nukta inayoashiria kuwepo hitilafu za kimaoni juu ya suala hili katika ngazi tofauti za Taliban.

Stanikzai, ambaye ni msomi katika kundi la Taliban na ana elimu ya juu, ndiye mshika bendera katika mrengo ulio ndani ya Taliban ambao unatetea kuendelea masomo kwa ajili ya wasichana. Hata hivyo watoa maamuzi wakuu katika suala hili ni mrengo wa Taliban ulioko Kandahar, ambao hauna mtazamo chanya kuhusu wasichana kuruhusiwa kwenda shule.

Asadullah Zairi, mtaalamu wa masuala ya kisiasa nchini Afghanistan, anasema: "Taliban ya leo sio sawa na Taliban ya Afghanistan miongo miwili iliyopita, na kuna mirengo kadhaa kama mrengo wa Haqqani, ambao umeungana na kundi hili. Mrengo wa Haqqani unaonekana kuwa karibu zaidi na Pakistan. Ingawa  wanachama wote wa Taliban wamepata elimu aina moja ya kidini lakini wanatofautiana katika mitazamo ya kisiasa na kijeshi. 

Kwa vyovyote vile, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Afghanistan, hatua ya serikali ya Taliban ya kuwazuia wasichana kuendelea na masomo inaendelea kukosolewa kitaifa na kimataifa.

Miongoni mwa wakosoaji wa sera hiyo ya Taliban ni Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ambayo imesema kuwa kuzuia wasichana na wanawake kusoma nchini Afghanistan ni kinyume cha Sheria za Kiislamu.

Hata hivyo, serikali ya Taliban imetangaza mara kwa mara kwamba haijawakataza wasichana kuendelea na masomo na kwamba inajaribu kuwaandalia mazingira maalumu ya kuendelea na elimu. Pamoja na hayo hadi sasa Taliban haijaweka muda maalumu wa wasichana kurejea shuleni.

Hii ina maana kwamba hakuna makubaliano yaliyopo baina ya mirengo mbali mbali ya Taliban kuhusu kadhia hii. Inavyolekea ni kuwa mrengo mmoja wa Taliban unatoa ahadi kuwa wasichana wataruhusiwa kusoma ili kuushinikiza mrengo wenye misimamo mikali ulegeze kamba na hivyo hatimaye kuwaruhusu wasichana na mabinti wa Afghanistan waweze kuendelea na masomo.