Apr 28, 2023 12:51 UTC
  • Kuongezeka gharama za kijeshi za Ulaya baada ya Vita Baridi kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa

Matumizi ya kijeshi barani Ulaya katika mwaka ulipoita wa 2022 yalipita kiwango hata cha kipindi zilipomalizika enzi za Vita Baridi.

Ongezeko hilo halijawahi kushuhudiwa mfano wake tokea miongo mitatu iliyopita hadi hivi sasa; na vita vya Ukraine ndio sababu kuu ya kukithiri kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa cha gharama hizo za kijeshi. Poland, Uholanzi, na Sweden ni miongoni mwa nchi ambazo katika muongo mmoja uliopita zimewekeza na kugharimika zaidi kifedha kwa ajili ya vikosi vyao vya ulinzi.

Nchini Ukraine pekee, matumizi ya kijeshi yameongezeka kufikia dola bilioni 44 kwa mwaka, ambayo ni theluthi nzima ya pato lote la taifa hilo. Hii ni pamoja na makumi ya mabilioni ya dola za misaada ya kijeshi na silaha, ambazo kambi ya Magharibi imeipatia Ukraine. Tathmini zinaonyesha kuwa Russia pia imeongeza kwa asilimia 9.2 matumizi yake ya kijeshi na uwekezaji katika vikosi vyake vya ulinzi. Lakini hata ukiondoa nchi hizo mbili zilizoko vitani, gharama za kijeshi barani Ulaya zimeongezeka kwa kiwango kikubwa.

Silaha za Magharibi zimemiminwa kwa wingi nchini Ukraine

 

Katika mwaka uliopita, nchi za Ulaya ziliwekeza jumla ya dola bilioni 480 kwa ajili ya vikosi vyao vya ulinzi. Na hii ni katika hali ambayo, katika kipindi cha miaka kumi iliyopita gharama za kijeshi katika nchi za Ulaya ziliongezeka kwa kiwango cha theluthi moja tu. Nan Tian, mtaalamu wa masuala ya kijeshi, anasema: “Vita vya Ukraine vimezifanya nchi za Ulaya zifikirie zaidi kuongeza gharama za matumizi yao ya kijeshi kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa”.

Baada ya Russia kuishambulia kijeshi Ukraine, mabadiliko ya kimsingi yametokea katika muelekeo wa kijeshi na kiusalama wa nchi za Ulaya hususan Ujerumani, ikiwa ndio nchi muhimu zaidi na yenye uchumi mkubwa zaidi barani humo. Kwa kweli vita vya Ukraine vimekuwa mithili ya chachu iliyoongeza kasi ya nchi za Ulaya kushupalia zaidi masuala ya kivita na kijeshi. Kwa upande wa Ujerumani, katika enzi za utawala wa Kansela wa zamani Angela Merkel, nchi hiyo na licha ya kuahidi mara kadhaa, ikiwa mmoja wa wanachama wa shirika la kijeshi la NATO, haikukubali kutekeleza ahadi ya kutenga asilimia mbili ya pato lake la taifa kwa ajili ya masuala ya kijeshi.

Msimamo huo wa Berlin uliochukuliwa hasa wakati wa kipindi cha urais wa Donald Trump nchini Marekani ulikuwa moja ya sababu za mvutano mkubwa uliozuka kati ya Berlin na Washington, na kupelekea hata Trump kuamuru kuondolewa idadi kubwa ya wanajeshi wa Marekani waliokuweko Ujerumani kama hatua ya kuiadhibu nchi hiyo. Lakini katika wakati wa urais wa Joe Biden, na kwa kuzingatia mtazamo wake kufufua mshikamano wa nchi wanachama wa NATO, serikali ya Berlin imeonyesha ulainifu katika suala hilo na kuwa tayari kuongeza bajeti yake ya kijeshi. Pamoja na hayo, vita vya Ukraine vimekuwa sawa na chachu kwa Ujerumani ya kuongezea gharama za matumizi yake ya kijeshi.

Jeshi la nchi za Magharibi NATO

 

 

Kwa mtazamo wa Berlin, kushambuliwa kijeshi Ukraine kumeonyesha kuwa, kinyume na imani waliyokuwa nayo wengi, kwamba uwezekano wa kutokea vita rasmi baina ya nchi mbili katika bara la Ulaya ni mdogo sana, hasa baada ya Vita vya Pili vya Dunia, mabadiliko ya kisiasa na kijeshi yaliyojitokeza yamepelekea kujiri kile kilichodhaniwa kuwa muhali kutokea. Kwa hiyo, ili kuongeza kiwango cha kujizatiti kwake kijeshi kwa ajili ya kukabiliana na vitisho vya sasa na vya baadaye hususan kutoka kwa Russia, Berlin iliamua kuimarisha kwa kiwango cha juu mno uwezo wake wa kijeshi kwa kutenga bajeti ya yuro bilioni 100 kwa ajili ya suala hilo. Kinachotoa mguso zaidi ni kwamba, kiwango hicho ni kikubwa zaidi kuliko hata kile kilichoainishwa na shirika la kijeshi la NATO. Hatua hiyo ya Ujerumani imekaribishwa kwa mikono miwili na Washington hasa baada ya Berlin kuchukua hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa ya kutaka kununua idadi kubwa ya ndege za kivita aina ya F-35 za kizazi cha tano kutoka Marekani. Hata hivyo, mabadiliko hayo katika muelekeo wa kijeshi wa Ujerumani yamekosolewa na vyama vya upinzani vya nchi hiyo.

Dietmar Bartsch, kiongozi wa wabunge wa chama cha Mrengo wa Kushoto ndani ya Bunge la Ujerumani amesema, mpango wa serikali wa kutenga yuro bilioni 100 kwa ajili ya kulizatiti upya kwa silaha jeshi la nchi hiyo ni uwendawazimu, na akaeleza kwamba hatua hiyo inaweza kusababisha kupungua misaada ya kijamii. Bartsch ameeleza katika taarifa yake: "mpango wa kutenga yuro bilioni 100 kwa ajili ya la kulizatiti upya kwa silaha jeshi la Ujerumani ni uwendawazimu, ambao wabunge wa mrengo wa kushoto watasimama kuupinga; na sababu ni kuwa hatua hii inaweza kusababisha kupunguzwa misaada ya kijamii kwa watu wa Ujerumani. Bajeti hii ni neema kwa sekta ya ulinzi, lakini ni pesa nyingi mno kwa watu wanaohangaika ili kuweza kujikimu kimaisha”.

Wakati huo huo, Marekani, ikiwa ndiye kinara wa NATO, si tu inafanikisha maslahi yake ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama kwa kuwahimiza washirika wake wa Ulaya wapeleke silaha zaidi nchini Ukraine, lakini pia inashupalia kuvuruga uthabiti na usalama barani Ulaya ili kwa njia hiyo iimarishe zaidi satua yake barani humo na kuzifanya nchi za Ulaya zizidi kuwa tegemezi kwake kiusalama na kijeshi. Jambo hili linafanikishwa hasa kwa kuyadhaminia faida nono makampuni ya kijeshi na viwanda ya Marekani kupitia ongezeko la mauzo ya silaha kwa nchi za Ulaya. Ununuzi wa zana za kisasa za kijeshi lakini kwa bei ghali mno kama ndege za kivita za Marekani aina ya F-35, ni miongoni mwa sababu kuu za kuongezeka gharama za matumizi ya kijeshi katika nchi hizo. Na mfano wake ni Ujerumani, ambayo kabla ya hapo haikuwa na hamu ya kununua mitambo ya silaha za Kimarekani, lakini sasa imekuwa ya mbele kwenye foleni ya ununuzi wa silaha hizo. /

Tags