Sep 04, 2023 11:50 UTC
  • Sura ya Annajm, aya ya 19-30 (Darsa ya 966)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 966 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 53 ya An-Najm. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 19 hadi ya 23 ya sura hiyo ambazo zinasema:

أَفَرَأَيْتُمُ اللَّاتَ وَالْعُزَّىٰ

 Je! Mmemuona Lata na Uzza?

وَمَنَاةَ الثَّالِثَةَ الْأُخْرَىٰ

Na Manata, mwingine wa tatu? 

أَلَكُمُ الذَّكَرُ وَلَهُ الْأُنثَىٰ

Je, nyinyi mnao watoto wa kiume na Yeye ndio awe na watoto wa kike (mnaowachukia)?

تِلْكَ إِذًا قِسْمَةٌ ضِيزَىٰ

Huo ni mgawanyo wa dhulma!

إِنْ هِيَ إِلَّا أَسْمَاءٌ سَمَّيْتُمُوهَا أَنتُمْ وَآبَاؤُكُم مَّا أَنزَلَ اللَّهُ بِهَا مِن سُلْطَانٍ ۚ إِن يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَمَا تَهْوَى الْأَنفُسُ ۖ وَلَقَدْ جَاءَهُم مِّن رَّبِّهِمُ الْهُدَىٰ

Hayo hayakuwa ila ni majina mliyo wapa nyinyi na baba zenu. Mwenyezi Mungu hakuleta uthibitisho wowote juu ya hayo. Hawafuati ila dhana tu na zinayoyapenda nafsi (zao). Na kwa yakini uwongofu ulikwisha wafikia kutoka kwa Mola wao Mlezi.

Aya hizi zinatoa changamoto kwa moja kati ya imani na itikadi muhimu zaidi waliyokuwa nayo waabudu masanamu wa Makka kwa kuwaambia watu hao: nyinyi kwa upande mmoja mnayamithilisha masanamu haya na malaika na kuyaabudu. Na kwa upande mwingine mnawaitakidi malaika kuwa ni mabanati wa Mwenyezi Mungu na mnatumai kuwa watakushufaieni na kukuombeeni kwa Mwenyezi Mungu, wakati kwanza kabisa ni kwamba, Allah SWT hana mwana; na malaika si wana wa Mungu. Lakini pili, malaika hawakuumbwa kama wanadamu kwa sura ya kuwa katika jinsia mbili ya kike na ya kiume. Isitoshe ni kuwa, nyinyi mnamchukulia mtoto wa kike kuwa ni kitu cha aibu, kisirani na nuhusi, kiasi kwamba mko tayari hata kumzika akiwa hai. Sasa inakuwaje mnawaitakidi malaika kuwa ni mabinti wa Mwenyezi Mungu na kuwanasabisha na Yeye Allah SWT?! Je, mnayo nyinyi hoja na burhani ya kuthibitishia dai lenu hilo? Au hayo ni matokeo ya kuathiriwa na khurafa na mambo ya bidaa na uzushi ambayo wamekuachieni mababa na mababu zenu na nyinyi mumeamua kuyakubali bila hoja wala ushahidi wowote? Kama mnataka muwe na utambuzi sahihi wa Mwenyezi Mungu, jueni kwamba Allah SWT ameshakuonyesheni njia ya uongofu kwa kukuleteeni Mtume wake wa mwisho na Kitabu chake cha Qur'ani ili msije mkaishia kwenye dhalala na upotofu. Baadhi ya tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kwamba, washirikina walikuwa wakiamini kuwepo kwa Mwenyezi Mungu, lakini wakiingiza khurafa na uzushi katika ibada, kwa kuabudu masanamu ya mawe, waliyoyafanya kuwa nembo ya mabinti wa Mwenyezi Mungu. Jengine tunalojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa, katika kuzikabili hoja za upotofu tunaweza kutumia mbinu ya majadiliano na kumshinda mpinzani wa haki kwa kutumia mantiki ileile anayoitegemea yeye. Ikiwa wao washirikina wa Makka walikuwa wakiwaona watoto wa kike nuhusi na kisirani, vipi walikuwa wakiwaitakidi malaika kuwa ni mabinti wa Mwenyezi Mungu? Halikadhalika aya hizi zinatutaka tujue kwamba, kufanya ubaguzi kati ya watoto wa kike na wa kiume na kumkweza mmoja juu ya mwingine ni miongoni mwa vielelezo vya dhulma na utovu wa uadilifu. Wa aidha aya hizi zinatuonyesha kuwa, kwa vile mila na itikadi za waliotangulia zina taathira kubwa katika utamaduni wa vizazi vinavyofuatia, kuzifuata mila, desturi na itikadi hizo kibubusa si hasha kukawa sababu ya kuenea uzushi na upotofu katika jamii za wanadamu. Vilevile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, imani zisizo na mashiko na kufuata hawaa na matamanio ya nafsi ndio sababu ya kupotoka watu wengi na kujiweka mbali na njia ya Mwenyezi Mungu ya uongofu.

Aya ya 24 hadi ya 26 ya sura yetu ya An-Najm ndizo zinazotuendelezea darsa yetu hii. Aya hizo zinasema:

أَمْ لِلْإِنسَانِ مَا تَمَنَّىٰ

Ati mtu anakipata kila anacho kitamani?

فَلِلَّهِ الْآخِرَةُ وَالْأُولَىٰ

Ni ya Mwenyezi Mungu tu akhera na dunia.

وَكَم مِّن مَّلَكٍ فِي السَّمَاوَاتِ لَا تُغْنِي شَفَاعَتُهُمْ شَيْئًا إِلَّا مِن بَعْدِ أَن يَأْذَنَ اللَّهُ لِمَن يَشَاءُ وَيَرْضَىٰ

Na wako Malaika wangapi mbinguni, ambao uombezi wao hautafaa chochote isipo kuwa baada ya Mwenyezi Mungu kutoa idhini kwa amtakaye na kumridhia.

Kwa mujibu wa aya hizi, washirikina walikuwa wakiwaabudu malaika kwa tamaa ya kushufaiwa na kuombewa msamaha na viumbe hao, ilhali matamanio hayo, kama yalivyo matamanio na matarajio yao mengine yasiyo na msingi wala mashiko hayawezi kuthibiti katu. Na sababu ni kuwa dunia na akhera zinaendeshwa kwa irada na matakwa ya Mwenyezi Mungu na wala hazifuati wanayotamani na wanayoyataraji wao. Ni jambo lisilo na shaka kwamba, matumaini juu ya mustakabali ndio injini ya kuendeshea harakati za mtu na kumjenga na kumuinua katika mambo yake. Bila kuwepo matumaini, hakuna mtu yeyote atakayejipinda na kufanya juhudi wala kupiga hatua yoyote kwa ajili ya kusonga mbele katika masuala ya maisha yake. Lakini pamoja na hayo, matumaini na matarajio ya mtu inatakiwa yaendane na suhula na nyenzo alizonazo, kipawa na uwezo wake, la sivyo matarajio na matumaini hayo yatakuwa sawa na njozi na ndoto za alinacha. Kwa hivyo inachokikataa aya tuliyosoma, ni mtu kuwa na matarajio hewa na yasiyo na msingi ambayo hayakubaliwi na akili na mantiki au wahyi wa mbinguni. Na kwa hakika kuachana na matarajio hewa kama hayo yasiyoendana na uhalisia wa mambo wala kukubaliwa na akili timamu, huwa ni msingi wa ukuaji na utukukaji, kwa mtu binafsi na jamii ya wanadamu kwa ujumla. Miongoni mwa tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kwamba, kuiweka pembeni akili na Wahyi ambazo ni nyenzo za kumuonyesha mwanadamu njia ya uongofu, saada na mafanikio; na kuishi kwenye matarajio hewa na njozi za alinacha, humdumaza mtu akashindwa kupiga hatua za ukuaji na utukukaji kiroho na kukosa rehma na fadhila za Allah, hapa duniani na huko akhera. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, inatupasa tuyaoanishe matakwa na matarajio yetu na matakwa na irada ya Allah SWT ili tuweze kupata tija tuliyoikusudia; na si kutaka au kutaraji irada ya Allah inayoendana na hekima, ifuate irada na matarajio yetu sisi. Wa aidha aya hizi zinatuonyesha kwamba, ikiwa malaika waliokurubishwa kwa Allah hawawezi kuwaombea na kuwatakia shufaa watu bila ya irada na idhini yake Yeye Mola, litarajiwe nini kwa vitu kama masanamu, ambavyo havina uhai wala faida yoyote?

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 27 hadi 30 ya sura yetu ya An-Najm ambazo zinasema:

إِنَّ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ لَيُسَمُّونَ الْمَلَائِكَةَ تَسْمِيَةَ الْأُنثَىٰ

Hakika wasio amini Akhera bila ya shaka wao ndio wanawaita Malaika kwa majina ya kike.

 وَمَا لَهُم بِهِ مِنْ عِلْمٍ ۖ إِن يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ ۖ وَإِنَّ الظَّنَّ لَا يُغْنِي مِنَ الْحَقِّ شَيْئًا

Nao hawana ujuzi wowote wa hayo isipo kuwa wanafuata dhana tu. Na hakika dhana haisaidii chochote mbele ya haki.

فَأَعْرِضْ عَن مَّن تَوَلَّىٰ عَن ذِكْرِنَا وَلَمْ يُرِدْ إِلَّا الْحَيَاةَ الدُّنْيَا

Basi mwachilie mbali anaye upa kisogo ukumbusho wetu, na wala hataki ila maisha ya dunia.

ذَٰلِكَ مَبْلَغُهُم مِّنَ الْعِلْمِ ۚ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ بِمَن ضَلَّ عَن سَبِيلِهِ وَهُوَ أَعْلَمُ بِمَنِ اهْتَدَىٰ

Huo ndio mwisho wao wa ujuzi. Hakika Mola wako Mlezi ndiye anaye mjua zaidi mwenye kuipotea njia yake, na Yeye ndiye anaye mjua zaidi mwenye kuongoka.

Kama tulivyotangulia kueleza hapo kabla pia, washirikina walikuwa wakiamini na kukubali kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye Muumba wa ulimwengu, lakini hawakuwa wakiamini kuwepo kwa Kiyama wala kulipwa watu thawabu na adhabu katika ulimwengu wa baada ya kifo. Kwa sababu hiyo, aya tulizosoma zinasema: watu wanaomnasibisha Allah na mambo ya khurafa, bidaa na uzushi na kuabudu masanamu kutokana na itikadi hizo za uzushi, wao kwa hakika hawaamini Kiyama na wala hawana hofu juu ya hatima ya matendo yao. Mwendelezo wa aya unaashiria moja ya mambo yanayozisababishia madhara jamii za wanadamu na kueleza kwamba: imani na itikadi walizonazo watu wengi kuhusu asili na mwisho wa ulimwengu, yaani mabda'a na maadi zinatokana na dhana na ukisiaji tu, ilhali katika masuala kama hayo, mtu anatakiwa awe na ujuzi na elimu ya yakini ili aweze kuwa na uhakika wa kile anachokiamini. Na kwa kawaida, watu wanaotaka wawe na utambuzi sahihi wa asili ya ulimwengu, huwa wanawaendea Mitume na kuelimika kwa miongozo yao ya uongofu, wakati ukomo wa uelewa wa watu wengine kuhusu ukweli na hakika ya mambo unaishia kwenye kuijua dhahiri ya dunia pamoja na manufaa na raha zake za kimaada tu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kufuata dhana na makisio katika mambo ya kawaida na yasiyo na umuhimu mkubwa, huenda hasara yake isiwe kubwa sana au ikaweza pengine hata kufidika; lakini ufuataji wa aina hiyo katika masuala ya imani na itikadi humsababishia mtu hasara kubwa mno na isiyoweza kufidika, kwa sababu umri na uhai wa mwanadamu hauwezi katu kurudiwa mara ya pili. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, katika kuwafunza, kuwaelimisha na kuwalingania watu wito wa Allah, tuwaendee wale ambao wana kiu ya kuijua haki na ukweli, si kuwashughulikia watu walioamua kujitenga na utajo wa Allah na kuamua kufumba macho na masikio yao wasiutazame wala kuusikiliza ukweli na haki. Halikadhalika aya hizi zinatuonyesha kwamba, kupenda dunia ni moja ya sababu za kumsahau Mwenyezi Mungu na Siku ya Kiyama. Kutumia raha za kimaumbile za maisha kwa namna sahihi na inayokubalika kiakili, si jambo baya, bali ni lenye kupendeza pia, lakini kuikumbatia kupita kiasi dunia na kwa namna isiyo ya kawaida ni jambo linalokemewa na lenye madhara kwetu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 966 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuepushe na desturi ya kufuata dini kwa dhana na mazoea na atujaalie kuwa miongoni mwa waja wake wanaotekeleza mafundisho ya dini yake kwa ujuzi na elimu ya yakini. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags