Jumatatu tarehe 18 Machi 2024
Leo ni Jumatatu tarehe 7 Ramadhani 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 18 Machi 2024.
Siku kama ya leo miaka 1435 iliyopita, yaani tarehe 7 Ramadhani mwaka wa 10 baada ya kubaathiwa Mtume, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, Abu Twalib ami ya Mtume Muhammad (SAW) na baba wa Imam Ali (A.S) alifariki dunia.
Abu Twalib alichukua jukumu la kumlea Mtume wetu Muhammad (SAW) akiwa na umri wa miaka minane, baada ya kuaga dunia babu yake, Abdul Muttalib. Abu Twalib alikuwa mlinzi na msaidizi mkubwa wa Mtume (saw) baada ya mtukufu huyo kupewa Utume, na daima alisimama dhidi ya Washirikina wa Makka waliompiga vita Mtume wa Mwenyezi Mungu. Kabla ya kuaga dunia, Abu Twalib aliwausia jamaa na marafiki zake kufuata Uislamu na kumtetea Mtume Muhammad (saw).

Siku kama ya lao miaka 211 iliyopita, alizaliwa Christian Friedrich Hebbel mwanafasihi na mkosoaji mkubwa wa Ujerumani.
Akiwa kijana mdogo na kutokana na kufariki dunia baba yake, alilazimika kufanya kazi katika kiwanda cha kuchapisha magazeti kwa lengo la kujidhaminia mahitaji yake. Hata hivyo baada ya kufanya tafiti kadhaa na kujiongezea maarifa, alianza kazi ya uandishi. Akiwa na umri wa miaka 20 Christian Hebbel alianza kusambaza Makala zake kwa ajili ya kuchapishwa katika magazeti ya fasihi ya mjini Hamburg, Ujerumani.
Baada ya hapo alijiendeleza zaidi kielimu ambapo sambamba na kuendelea na masomo pia alikuwa akijihusisha na kazi za fasihi na kuandika michezo ya sinema mbalimbali ambapo pia katika uwanja huo ameacha athari katika uga wa fasihi na nadharia za ukosoaji. Hebbel alifariki dunia mwaka 1863 Miladia akiwa na umri wa miaka 50. ***

Miaka 166 iliyopita katika siku kama leo, alizaliwa mvumbuzi mashuhuri wa Kijerumani, Rudolf Diesel, ambaye alibuni injini ya diseli.
Diesel alifanya utafiti na uhakiki mkubwa kuhusu injini za mitambo mbalimbali na akafanikiwa kuvumbua chombo ambacho kinaweza kuzalisha nishati kubwa zaidi bila ya kuhitaji umeme lakini kwa kutumia nishati ya kawaida na rahisi zaidi.
Chombo hicho ambacho kilipewa jina lake mwenyewe la Diesel kilileta mabadiliko makubwa katika sekta ya viwanda na usafirishaji kwa kadiri kwamba licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia lakini injini za diseli zingalia zinatumika kwa kuwa ni zenye nguvu kubwa na zinazotumia nishati ndogo. Rudolf Diesel alifariki dunia mwaka 1913. ***

Miaka 59 iliyopita katika siku kama ya leo, mfalme Farouk wa Misri aliyekuwa ameondolewa madarakani aliaga dunia.
Mfalme Farouk alizaliwa 1920 Miladia. Alizaliwa katika kipindi ambacho baba yake yaani Ahmad Fuad alikuwa akitawala nchini Misri kwa anuani ya Fuad wa Kwanza. Farouk alichukua madaraka akiwa na umri wa miaka 16 baada ya kuaga dunia baba yakke.
Hata hivyo kutokana na kutotimiza umri wa kisheria, uongozi na usimamizi wa nchi ulikabidhiwa kwa Baraza la Niaba la Ufalme. ***
