Alkhamisi, tarehe 4 Aprili, 2024
Leo ni Alkhamisi tarehe 24 Ramadhani 1445 Hijria sawa na 04 Aprili mwaka 2024.
Siku kama ya leo miaka 735 iliyopita, alifariki dunia Qutbuddin Shirazi, tabibu, mwanahesabati, mwanafikizia na mwanafalsafa wa Kiirani katika mji wa Tabrizi huko kaskazini magharibi mwa Iran.
Qutbuddin Shirazi alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Khaja Nasiruddin Tusi. Alibobea pia katika elimu za mantiki na irfani. Alifanya hima kubwa kutafuta elimu ya tiba na alihudumu kwa miaka mingi kama tabibu katika hospitali ya Shiraz, kusini mwa Iran.
Qutbuddin Shirazi alikuwa mtu wa kwanza kufanya uchunguzi kuhusu upinde wa mvua na kupata tafsiri ya kisayansi kuhusu suala hilo. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi katika taaluma mbalimbali.

Siku kama hii ya leo miaka 64 iliyopita Senegal inayopatikana magharibi mwa Afrika ilipata uhuru. Senegal ilikuwa chini ya ushawishi na ukoloni wa Wareno kuanzia karne ya 15 na kuanzia karne ya 17 pia Wafaransa nao walianza kuiba maliasili na utajiri wa nchi hiyo. Senegal iko katika pwani ya bahari ya Atlantic na inapakana na nchi za Mauritania, Mali, Guinea Bissau na Gambia.

Miaka 56 iliyopita katika siku kama ya leo Martin Luther King kiongozi aliyeongoza mapambano ya raia weusi wa Marekani aliuawa kwa kupigwa risasi na mtu mmoja au watu kadhaa wasiojulikana.
Martin Luther alizaliwa mwaka 1929 katika mji wa Atlanta huko Marekani. Alipata mafunzo katika Chuo Kikuu cha Boston na baadaye aliongoza harakati ya ukombozi ya Wamarekani weusi dhidi ya ubaguzi wa rangi waliokuwa wakifanyiwa raia weusi nchini Marekani. Katika kipindi hicho raia weusi wa Marekani waliasisi harakati ya nchi nzima ya kupinga ubaguzi wa rangi na vilevile katika kulalamikia sheria iliyokuwa ikiwatambua wazungu kama watu wa daraja ya juu huko Marekani. Kwa mujibu wa baadhi ya ushahidi ni kuwa shirika la ujasusi la Marekani CIA lilihusika katika mauaji hayo.

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita Zulfikar Ali Bhutto, Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan alinyongwa. Bhutto ambaye alikuwa mwasisi wa Chama cha Wananchi (PPP) alikuwa Rais wa Pakistan mwaka 1971.
Mwaka 1977 Jenerali Muhammad Dhiaul Haq alifanya mapinduzi na kumuondoa madarakani Bhutto akimtuhumu kuwa amefanya mauaji na kuisaliti Pakistan. Hatimaye tarehe 4 Aprili mwaka 1979 Zulfiqar Ali Bhuttoalinyongwa, licha ya viongozi wa baadhi ya nchi duniani kutaka asamehewe.
