Jul 14, 2016 06:33 UTC
  • Alkhamisi, 14 Julai, 2016

Leo ni Alkhamisi tarehe 9 Mfunguo Mosi Shawwal 1437 Hijria sawa na tarehe 14 Julai 2016.

Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita inayosadifiana na tarehe 24 Tir 1318 Hijria Shamsia, alizaliwa Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mji wa Mash'had ulioko kaskazini mashariki mwa Iran. Baada ya kumaliza masomo katika shule ya sekondari, alijikita zaidi katika masomo ya kidini kutoka kwa baba yake, na kupiga hatua kubwa ya kielimu katika kipindi kifupi. Ayatullah Khamenei alielekea mjini Qum kwa masomo ya juu ya kidini na kupata fursa ya kunufaika na elimu kutoka kwa maulamaa wakubwa katika mji huo, kama vile Imam Khomeini MA, Ayatullahil Udhma Burujerdi na Allamah Tabatabai katika masomo ya fiqh, usulul na falsafa. Akiwa bado kijana, Sayyid Khamenei  alikuwa mstari wa mbele katika harakati za mapinduzi dhidi ya utawala kibaraka wa Shah hapa nchini, na mara kadhaa alitiwa mbaroni, kutumikia vifungo na hata kupelekwa uhamishoni. Baada ya kufariki dunia Imam Khomeini MA mwaka 1368 Hijria Shamsia, Baraza la Wanachuoni linalomchagua Kiongozi wa Mkuu wa Iran, lilimchagua Ayatullah Khamenei wakati huo akiwa rais wa nchi, kuwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 1327 iliyopita, alifariki dunia Ibn Sirin, mtaalamu wa hadithi na fiqihi ambaye pia alikuwa msomi mashuhuri wa karne ya pili Hijiria. Ibn Sirin alizaliwa mjini Basra, kusini mwa Iraq na kuanza kujifunza elimu mbalimbali akiwa kijana mdogo. Alizipa umuhimu mkubwa hadithi za Bwana Mtume Muhammad (swa) na alihifadhi na kunakili hadithi hizo kwa umakini mkubwa. Ni kutokana na hali hiyo ndipo wataalamu wengi wa hadithi wakazitilia maanani sana hadithi zilizopokelewa na Ibn Sirin. Ni vyema ikafahamika hapa kwamba, Ibn Sirin alibahatika kukutana na masahaba 30 wa Mtukufu Mtume Muhammad (swa) na kuweza kunufaika kwao.

Tarehe 24 Tir mwaka 1347 Hijria Shamsia, Ismail Balkhi mwanamapambano na mwanafikra wa Kiafghani aliuawa shahidi mjini Kabul. Alizaliwa katika kijiji kimoja kaskazini mwa Afghanistan. Alianza kusoma kwa bidii masomo ya dini tangu akiwa mdogo na kipindi fulani alifanya safari nchini Iran na Iraq, lengo likiwa ni kujiendeleza zaidi kielimu katika masomo ya dini. Ismail Balkhi alikuwa akiendesha mapambano dhidi ya udikteta na daima alikuwa akiwashajiisha wananchi Waislamu wa Afghanistan kupambana na tawala dhalimu. Kutokana na harakati hizo, shahidi Balkhi alikuwa chini ya mashinikizo ya watawala wa wakati huo wa Afghanistan, na kwa miaka kadhaa alifungwa jela.

Na siku kama hii ya leo miaka 6 iliopita, miripuko miwili ya kujilipua kwa mabomu ilitokea katika mji wa Zahidan kusini mashariki mwa Iran na kuuwa watu 27 na kujeruhi wengine 169. Miripuko hiyo ilitokea mbele ya msikiti wa Zahidan wakati wa maadhimisho ya kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Hussein AS. Kundi la kigaidi linalojiita Jundullah lilitangaza kuhusika na miripuko hiyo. Kundi hilo aidha limehusika katika oparesheni nyingi za kigaidi na kuuwa raia wengi wa Iran. Oparesheni ya kigaidi ya Zahidan ilifanywa mwezi mmoja baada ya kunyongwa Abdulmalik Rigi kiongozi wa zamani wa kundi la kigaidi la Jundullah, ambaye alitiwa mbaroni katika oparesheni moja ya kiusalama iliyofanywa na jeshi la Iran. Baada ya kutiwa mbaroni, Abdul Malik Rigi, alikiri kuwa na uhusiano na Marekani. Magaidi watatu waliokuwa na ushawishi mkubwa katika kundi hilo walikamatwa na baadaye kunyongwa baada ya kutokea miripuko hiyo ya kuhuzunisha.