Ijumaa, 29 Julai, 2016
Leo ni Ijumaa tarehe 24 Shawwal 1437 Hijria sawa na 29 Julai 2016.
Tarehe 8 mwezi Mordad kwa mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia ni siku ya kumuenzi mwanafalsafa, arifu na msomi mkubwa wa Kiislamu Shahabuddin Sohravardi aliyepewa lakabu ya Sheikhul Ishraq. Sheikhul Ishraq alizaliwa mwaka 549 Hijria karibu na mji wa Zanjan kaskazini magharibi mwa Iran. Alibobea haraka katika taaluma nyingi za Kiislamu za wakati huo hususan falsafa. Sheikh Sohravardi alifanya safari katika miji mbalimbali ya nchi za Kiislamu kwa ajili ya kutafuta elimu. Aliasisi mfumo mpya wa falsafa na irfani uliopewa jina la Ishraq. Sheikhul Ishraq ameandika vitabu vingi kama vile "Hikmatul Ishraq", al Mabda wal Maad", na "Talwihat".
Siku kama ya leo miaka 9 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Ali Akbar Faydh mashuhuri kwa jina la Ayatullah Mishkini. Ayatullah Mishkini alisoma kwa wanazuoni wakubwa wa zama hizo kama Ayatullah Burujerdi na Imam Khomeini. Alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kujiunga na harakati ya mapambano ya Imam Khomeini dhidi ya utawala wa Shah. Alitiwa nguvuni na kufungwa jela mara kadhaa sambamba na kubaidishwa. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Mishkini alishika nyadhifa mbalimbali, na muhimu zaidi ni ule wa Mwenyekiti wa Baraza la Wanazuoni Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu na Kusimamia Kazi Zake. Alimu huyo ameandika vitabu vingi kama Islahul Usul na Ndoa katika Uislamu.
Tarehe 29 Julai miaka 59 iliyopita Umoja wa Mataifa ulianzisha Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). Lengo la kuanzishwa taasisi hiyo ya kimataifa, lilikuwa ni kusimamia shughuli zote za mitambo ya nyuklia na kuhakikisha kwamba miradi ya nyuklia duniani inatekelezwa kwa njia za amani na kutotumika kwa malengo ya kijeshi na utengenezaji wa silaha za mauaji ya halaiki.
Na siku kama ya leo miaka 133 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 29 Julai 1883, alizaliwa Benito Mussolini mwanasiasa, dikteta na mwasisi wa chama cha Kifashisti nchini Italia. Ufashisti ni utawala wa kidikteta uliojikita katika kuleta aidolojia ya kibaguzi na kiutaifa, kuwakandamiza wapinzani na kupotosha itikadi na fikra za wananchi. Mwaka 1922 Mussolini alinyakua wadhifa wa uwaziri mkuu wa Italia, na hivyo udikteta kuendelea kutawala nchini humo. Muda mfupi baadaye Mussolini alishirikiana na Adolph Hitler na kuandaa mazingira ya kuanza Vita vya Pili vya Dunia.