Jumanne Agosti Pili, 2015
Leo ni Jumanne tarehe 28 Shawwal 1437 Hijria sawaq na 2 Agosti 2016.
Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 2 Agosti 1990, jeshi la utawala wa Ba'ath nchini Iraq lilivamia na kuikalia kwa mabavu nchi ya Kuwait iliyoko kusini mwa Iraq. Hilo lilihesabiwa kuwa shambulio la pili na kuikalia kwa mabavu nchi jirani, baada ya kuishambulia na kuikalia kwa mabavu baadhi ya mikoa ya Iran mwaka 1980. Saddam Hussein alitangaza kuwa, Kuwait ni sehemu ya ardhi ya Iraq na kwamba ni jimbo la 19 la nchi hiyo.
Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, kulifanyika kongamano la Potsdam. Kongamano hilo la tatu na la mwisho la viongozi waitifaki walioshiriki katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, lilianza tarehe 17 mwezi Julai na kumalizika tarehe Pili 1945, Miladia. Aidha kongamano hilo, lililofanyika katika mji wa Potsdam ulio karibu na mji mkuu wa Ujerumani, Berlin lilihudhuriwa na Joseph Stalin, Harry S. Truman na Winston Churchill, marais wa wakati huo wa Urusi ya zamani, Marekani na Uingereza.
Siku kama ya leo miaka 82 iliyopita inayosadifiana na tarehe Pili Agosti 1934, alifariki dunia Paul von Hindenburg Rais wa zamani wa Ujerumani na Amiri jeshi mkuu wa vikosi vya majeshi ya nchi hiyo wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia. Hindenburg alichaguliwa kuwa Rais wa Kwanza wa Ujerumani mwaka 1925.
Na tarehe 2 Agosti miaka 94 iliyopita alifariki dunia mvumbuzi wa Kiscotland wa Marekani, Alexander Graham Bell. Alizaliwa mwaka 1847 nchini Scotland na baada ya kupatwa na maradhi ya kifua kikuu alihamia Canada akiwa pamoja na familia yake na kisha akahamia Marekani. Alexander Graham Bell alianza kufanya uchunguzi wa jinsi ya kuhamisha sauti na akazidisha utafiti na uchunguzi huo baada ya kujuana na Thomas Watson. Mwaka 1876 alifanikiwa kuvumbua simu. Hata hivyo chombo hicho kilichovumbuliwa na Alexander Graham Bell kilifanyiwa mabadiliko mengi na kumuwezesha mwanadamu kuhamisha sauti kutoka sehemu moja na kwenda nyingine bila ya kutumia waya.