Apr 04, 2025 02:34 UTC
  • Ijumaa, Aprili 4, 2025

Leo ni Ijumaa tarehe 5 Mfunguo Mosi Shawwal 1446 Hijria sawa na 04 Aprili mwaka 2025 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1095 iliyopita, sawa na tarehe 4 Shawwal mwaka 351 Hijiria, alifariki dunia Muhammad bin Hassan Daraqutni mmoja wa maulamaa na wataalamu wa lugha wa karne ya Nne Hijria.

Daraqutni alikuwa mmoja wa maqari na wafasiri watajika wa Qu'rani Tukufu katika zama zake hizo, na  alitumia umri wake kuandika vitabu.

Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo wa Kiislamu ni al Mu'jamul Akbar, al Manasik na al Maudhi' fii Ma'anil Qur'ani.   

Katika siku kama ya leo miaka 118 iliyopita, alifariki dunia Parvin I’tisami mwandishi na malenga mahiri wa Kiirani aliyekuwa na kipaji kikubwa.

Alizaliwa katika mji wa Tabriz ulioko kaskazini magharibi mwa Iran. Mshairi huyu alizaliwa katika familia iliyosifika kwa fadhila na heshima. Baba yake ni Yusuf I’tisam al-Mulk aliyekuwa mmoja wa watarjumi na waandishi watajika katika zama zake.

Parvin alijifunza fasihi ya Iran na ya Kiarabu kwa baba yake na alionyesha kipaji cha hali ya juu cha mashairi tangu akiwa mdogo. 

Parvin Etesami, aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 34 kutokana na homa ya matumbo, wakati alipokuwa akijiandaa kwa ajili ya kuchapisha diwani yake pili ya mashairi.

Katika siku kama hii ya leo miaka 65 iliyopita Senegal inayopatikana magharibi mwa Afrika ilipata uhuru.

Senegal ilikuwa chini ya ushawishi na ukoloni wa Wareno kuanzia karne ya 15 na kuanzia karne ya 17 pia Wafaransa nao walianza kuiba maliasili na utajiri wa nchi hiyo.

Senegal iko katika pwani ya bahari ya Atlantic na inapakana na nchi za Mauritania, Mali, Guinea Bissau na Gambia. 

Miaka 57 iliyopita katika siku kama ya leo Martin Luther King kiongozi aliyeongoza mapambano ya raia weusi wa Marekani aliuawa kwa kupigwa risasi na mtu mmoja au watu kadhaa wasiojulikana.

Martin Luther alizaliwa mwaka 1929 katika mji wa Atlanta huko Marekani. Alipata mafunzo katika Chuo Kikuu cha Boston na baadaye aliongoza harakati ya ukombozi ya Wamarekani weusi dhidi ya ubaguzi wa rangi waliokuwa wakifanyiwa raia weusi nchini Marekani.

Katika kipindi hicho raia weusi wa Marekani waliasisi harakati ya nchi nzima ya kupinga ubaguzi wa rangi na vilevile katika kulalamikia sheria iliyokuwa ikiwatambua wazungu kama watu wa daraja ya juu huko Marekani. Kwa mujibu wa baadhi ya ushahidi ni kuwa shirika la ujasusi la Marekani CIA lilihusika katika mauaji hayo.

Martin Luther King

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita Zulfikar Ali Bhutto, Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan alinyongwa.

Bhutto ambaye alikuwa mwasisi wa Chama cha Wananchi (PPP) alikuwa Rais wa Pakistan mwaka 1971.

Mwaka 1977 Jenerali Muhammad Dhiaul Haq alifanya mapinduzi na kumuondoa madarakani Bhutto akimtuhumu kuwa amefanya mauaji na kuisaliti Pakistan.

Hatimaye tarehe 4 Aprili mwaka 1979 Zulfiqar Ali Bhuttoalinyongwa, licha ya viongozi wa baadhi ya nchi duniani kutaka asamehewe. 

Zulfikar Ali Bhutto