Sep 07, 2016 03:59 UTC
  • Jumanne 6 Septemba, 2016

Leo ni Jumanne tarehe 4 Dhulhija 1437 Hijria sawa 6 Septemba 2016.

Siku kama ya leo miaka 250 iliyopita, alizaliwa John Dalton, msomi na mtaalamu wa fizikia wa Kingereza katika familia ya watu wa kijijini. Kutokana na Dalton kupendelea sana kusoma na licha ya kukabiliwa na matatizo mengi, hatimaye alifanikiwa kwenda shuleni na kujifunza. Ni wakati huo ndipo alipoanza kufanya uchunguzi na utafiti katika masuala mbalimbali ya kielimu. Dalton alikuwa akiamini kuwa, mada ndogondogo sana zimeundwa na atomu ambayo nayo inatokana na mada hizo. Msomi huyo ambaye macho yake yalikuwa na hali ya upofu, hakuchoka na badala yake aliendeleza utafiti mkubwa katika uga huo. Hatimaye mwaka 1944 John Dalton, alifariki dunia ambapo mazishi yake yalihudhuriwa na watu wengi.

Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita, jeshi la India lilianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Pakistan kufuatia machafuko ya zaidi ya mwezi mmoja katika mipaka ya nchi mbili hizo. Hivyo vilikuwa vita vya pili vikubwa kuwahi kutokea kati ya nchi mbili hizo jirani kuhusiana na eneo la Kashmir. Vita hivyo vilidumu kwa takribani wiki tatu. Pakistan na India zilikubaliana kusimamisha mapigano kufuatia upatanishi wa Urusi ya zamani. Viongozi wa nchi mbili hizo hatimaye waliafikiana kuanza mazungumzo tarehe 10 mwezi Juni mwaka 1966 huko Tashkent mji mkuu wa Uzbekistan nchini ya upatanishi wa Waziri Mkuu wa Urusi ya zamani. Japokuwa azimio la Tashkent lilibainisha njia za kumaliza mgogoro wa eneo la Kashmir na namna ya kuboresha uhusiano kati ya New Delhi na Islamabad na pia kukaribishwa na nchi mbalimbali duniani, lakini lilishindwa kumaliza hitilafu kati ya India na Pakistan kuhusu umiliki wa eneo la Kashmir.

Na siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Swaziland ilipata uhuru kutoka kwa Uingereza na kila inapowadia siku kama ya leo husherekewa nchini humo kwa anwani ya siku ya taifa. Kuimarika ukoloni wa Ulaya huko kusini mwa Afrika kulisababisha pia Swaziland kukaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Ulaya. Hatimaye katika siku kama ya leo nchi hiyo ndogo ya kusini mwa Afrika ilipata uhuru. Swaziland ina ukubwa wa kilomita mraba 17364 na kijiografia iko kusini mwa bara la Afrika ikiwa inapakana na nchi za Msumbiji na Afrika Kusini

Tags