Msafara wa Nuru
Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Kwa kuwadia mwezi wa Muharram, kumbukumbu ya hamasa inayobakia milele ya Karbala hujirudia tena akilini. Kila mtu, na kwa njia tofauti hujenga mawasiliano maalumu na Hussein Ibn Ali (AS) na harakati yake tukufu. Na sababu ni kwamba mapambano ya Imam Hussein (AS) hayakuwa ni vita na makabiliano tu ya silaha.
Harakati hiyo ni darasa la somo lenye mafunzo aali na matukufu kabisa ya akhlaqi na utambuzi. Siku Imam Hussein (AS) alipoanzisha harakati yake, sehemu kubwa ya jamii ya watu wa mji wa Kufa walikuwa wapenzi wa Ahlu Bayt wa Bwana Mtume SAW. Watu hao walikuwa wakiufahamu barabara ufasiki na udhalimu wa Yazid na namna asivyofaa hata chembe kuwa kiongozi. Lakini pia wakiitambua vyema hadhi na utukufu wa Imam Hussein (AS). Lakini ni wachache tu miongoni mwa watu hao waliojitolea kumsaidia Imam. Lakini hebu tujiulize, wafuasi wa Imam Hussein (AS) walikuwa na sifa gani maalumu, hata ikawa katika zama ambapo watu wengi walikuwa wameghariki kwenye lindi la usingizi mzito wa mghafala, wao walijitolea hadi pumzi yao ya mwisho kumhami Hussein (AS)? Bila ya shaka moja ya sifa za kipekee za harakati ya Imam Hussein (AS) ilikuwa ni hamasa ya kujivunia na kujitolea mhanga kulikooneshwa na wafuasi wake waaminifu. Kulifahamu barabara tukio la Karbala hakuyumkiniki pasina kuwafahamu wafuasi waaaminifu wa mtukufu huyo ambao basira na muono wa kina waliokuwa nao ndio uliowatoa walikokuwa na kuwafikisha kwenye ardhi hiyo.Moja ya sifa maalumu za wafuasi wa Imam Hussein (AS) ilikuwa ni yakini na maarifa ya kina waliyokuwa nayo juu ya njia waliyoamua kuifuata. Yakini, humfanya mtu awe thabiti katika njia anayoshikamana nayo. Yakini ni mithili ya mwenge uangazao unaoteketeza na kuigeuza jivu kabisa shaka na wasiwasi wowote uliomo ndani ya nafsi ya mtu. Bila ya kuwa na maarifa na utambuzi wa yakini mtu hukengeuka njia sahihi iliyonyooka na kuangukia kwenye dhalala na upotofu. Wafuasi wa Hussein Ibn Ali (AS) walifikia daraja ya maarifa na utambuzi wa kina. Walikuwa wakijua wamejitolea kumpa msaada mtu gani na ni wapi wanakoelekea.Wapenzi wasikilizaji, katika kipindi hiki maalumu tutazungumzia kwa muhtasari kisa cha mmoja wa wafuasi hao waaminifu waliojitolea mhanga nafsi zao katika ardhi ya Karbala.

Habib bin Madhahir, anampanda farasi wake akiuaga mji wa Kufa huku akiwa amefuatana na Muslim Ibn Ausajah. Umri wa Habib unapindukia miaka 80 lakini anamtoa shoti farasi wake mithili ya kijana mkakamavu ili awahi kufika Karbala. Wafuasi hao wawili, ambao huko nyuma walipata taufiki ya kuwa pamoja na Imam Ali (AS) sasa wanakimbilia Karbala ili kuwahami na kuwasaidia watoto wa mtukufu huyo. Baada ya kukata masafa kidogo tu, Habib bin Madhahir anasita na kugeuka nyuma kutazama anakotoka. Hakionekani chochote ghairi ya anga nyeusi ya mji wa Kufa. Mji wa wasaliti na wavunja ahadi. Habib anazikumbuka zile siku watu wa mji huo, wake kwa waume walipomlaki na kumkaribisha Muslim Ibn Aqil, mjumbe wa Imam Hussein (AS). Walibubujikwa na machozi ya shauku kubwa wakati waliposikia kwamba Hussein Ibn Ali (AS) atakwenda huko Kufa. Lakini baada ya kutishwa kidogo tu na kurubuniwa na kulaghaiwa, watu hao ambao jana tu walikuwa marafiki wa Imam, leo waligeuka kuwa masahibu vipenzi wa maadui zake.Habib bin Madhahir, akiwa amefuatana na Muslim bin Ausajah wanawasili Karbala siku ya mwezi sita Muharram; na kwa hamu na shauku kubwa wanakwenda moja kwa moja kuonana na Imam Hussein. Imam anamkumbatia Habib, ambaye huku akibubujikwa na machozi anaporomoka chini kwenye mchanga wa jangwa la Karbala kusujudu sijda ya kumshukuru Allah kwa kumjaalia taufiki ya kuwa pamoja na maulana wake Hussein Ibn Ali (AS).

Karbala inahudhuriwa na Habib bin Madhahir, mfuasi mzee zaidi wa Imam Hussein, lakini mwenye uchangamfu usioelezeka unaozipa nyoyo za wafuasi wengine wa mtukufu huyo hamasa na msisimko mkubwa. Katika giza la usiku sauti ya Qur'ani anayoisoma Habib inatanda kwenye anga ya jangwa la Karbala. Habib bin Madhahir ana mazoea makubwa na ya muda mrefu na Qur'ani. Kila fursa anayopata, Habib anaitumia kuzungumza na jeshi la adui, ambalo idadi ya askari wake inaendelea kuongezeka siku baada ya siku. Akiwa na matumaini kuwa huenda kukawepo na moyo utakaobadilika na kurudi kwenye haki, Habib anawaelekea watu hao na kuwaambia:"Enyi kaumu ya watu wabaya; ni jana tu mliandika barua ya kumwalika Hussein (AS), lakini leo mnavunja na kukhalifu ahadi yenu. Mtakuwa na jibu gani kesho Kiyama, mtakapokwenda huku mkiwa mumemuua mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu pamoja na jamaa zake na wafuasi wake wakeshao kwa ibada!"Katika usiku wa kuamkia siku ya Ashura hamu na shauku ya kujitolea mhanga inamjaa na kuivaa nafsi yote ya Habib. Agizo la Imam Hussein (AS) tayari limewafikia watu wote, kwamba jiandaeni kwa ajili ya kesho, ambayo haina hatima nyengine ghairi ya kuuawa shahidi. Sauti ya munajati na minong'ono ya kisomo cha kuvutia cha Qur'ani inazipa nyoyo uhai na msisimiko. Usiku wa manane unaingia wakati sauti hiyo inaposikika ikivuma kutoka kwenye hema la Habib bin Madhahir.

Alfajiri ya siku ya hamasa na mapambano imewadia. Baada ya adhana ya kusisimua nyoyo inayoadhiniwa na Ali Akbar (AS), mwana shujaa wa Imam Hussein (AS) na kufuatiwa na Sala ya jamaa inayosalishwa na mtukufu huyo; tayari kumepambazuka, na Habib tayari amevinjari upande wa kushoto wa jeshi la haki. Amechangamka zaidi na mwepesi zaidi kuliko alivyo kijana kwa hamasa na ukakamavu. Mfuasi mzee zaidi miongoni mwa wafuasi wa Hussein (AS) anazipanga safu za vijana, tayari kwa mapambano. Hamu na shauku imetanda kwenye uso wake huku midomo na ulimi wake ukiwa unasoma maneno matukufu ya Mwenyezi Mungu ya Qur'ani. Wakati askari wa jeshi la batili la Omar Saad wanapoanza kuvurumisha mishale, uso wa Habib bin Madhahir unaonekana umeng'ara na kumeremeta kuliko mwezi na nyota. Mawe, mishale na mikuki inaendelea kumiminika, lakini Habib analikabili bila ya woga jeshi la batili na kuwasambaratisha askari wake huku akipiga takbiri. Askari mmoja wa jeshi la Omar Saad anajaribu kumjongelea kwa karibu Habib bin Madhahir, lakini upanga wa sahaba huyo mwaminifu wa Imam Hussein haumpi fursa ya kutoa pigo. Katika lahadha hiyo mshale wenye ncha kali wa adui unamchoma ubavuni Habib bin Madhahir na upanga mkali unapasua kichwa chake. Wakati Habib anaanguka chini ndipo jeshi la adui linapothubutu kumkaribia. Linamzingira zaidi na zaidi. Sahaba huyo shujaa wa Bwana Mtume SAW, Imam Ali (AS) na sasa Imam Hussein (AS), ameanguka na kunyooka juu ya mchanga wa ardhi ya Karbala. Michirizi ya damu inatiririka na kurowesha nywele nyeupe za Habib. Muda mfupi baadaye kichwa cha jemedari huyo wa Ashura kinazungushwa kwenye medani ya vita huku nywele zake nyeupe zikining'inia. Wakati anapoiona mandhari hiyo, Imam Hussein anabubujikwa na machozi; na kwa huzuni na majonzi anamhutubu Habib kwa kusema:"Ewe Habib, Mwenyezi Mungu akubariki. Ulikuwa mja mwema ulioje kutokana na kukesha hadi alfajiri huku ukihatimisha kuisoma Qur'ani.Amani na rehma za Allah ziwe juu ya Hussein, na juu ya wana wa Hussein na juu ya masahaba wa Hussein. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.