Jumapili, 27 Novemba, 2016
Leo ni Jumapili tarehe 27 Swafar 1438 Hijria, sawa na tarehe 27 Novemba mwaka 2016 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 123 iliyopita, alifariki dunia Abul-Ma'alii Kalbasi Isfahani. Muhammad Bin Haj Muhammad Ibrahim Kalbasi, ni miongoni mwa maulama wakubwa wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia katika kipindi cha mwanzoni mwa karne ya 14 Hijiria. Kielimu, Kalbasi Isfahani alikuwa na daraja ya juu huku akiandika vitabu vingi. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na kitabu cha 'Sharh Kifaayat Sabzawari' 'Sharhu Khutbat-Damashqiyyah' na 'al-Jabr wa al-Tafwiidh.' Mbali na vitabu hivyo msomi huyo pia aliandika vitabu kuhusu wapokezi wa hadithi.
Siku kama ya leo miaka 97 iliyopita kuliainishwa michoro mipya ya mipaka baina ya Ulaya na eneo la Mashariki ya Kati baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Itakumbukwa kuwa baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia na kutiwa saini baadaye mkataba wa amani wa Versailles, kulitiwa saini mikataba mingine kwa ajili ya kuainisha wadhifa wa falme za Austria, Hungary, Othmania na nchi ya Bulgaria ambapo kila upande ulikubali kulipa gharama kubwa kwa nchi zilizoshinda. Kongamano la Paris ambalo liliainisha mipaka mipya ya Ulaya na nchi za Mashariki ya Kati, lilileta mabadiliko makubwa duniani.
Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 65 Eugene O’Neill mwandishi wa tamthilia maarufu wa nchini Marekani. O’Neill alizaliwa mwaka 1888 huku maisha yake yakiwa na matukio mengi. Akiwa kijana mdogo alipendelea sana tamthilia na hivyo akajikita katika fani hiyo. Mwaka 1936 alitunukiwa zawadi ya Nobel kutokana na tamthilia alizoziandaa.
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, karibu miezi miwili baada ya kuanza vita vya kulazimishwa vya utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya Jamahuri ya Kiislamu ya Ira, jeshi la baharini la nchi hii lilitekeleza operesheni katika eneo la Ghuba ya Uajemi na kuweza kulishinda jeshi la Iraq. Katika operesheni hiyo ambayo iliendana na kujiri mapigano makali baina ya askari wa nchi mbili, jeshi la Iran liliwaangamiza askari wengi wa Iraq sambamba na kuwasababishia hasara kubwa. Kufuatia operesheni hiyo jeshi la Iran na kwa uwezo wake mkubwa likafanikiwa kudhibiti kikamilifu Ghuba ya Uajemi. Siku hiyo inatambuliwa nchini hapa kama siku ya askari shupavu wa baharini.
Na siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Abdul A'alaa Mussawi Sabzawari mwanachuoni mashuhuri nchini Iran. Ayatullah Haj Sayyid Abdul A'alaa aliyekuwa mtoto wa Sayyid Ali Ridha Musawi Sabzawari, mmoja wa maulama wakubwa wa mjini Najaf, alizaliwa mwezi Swafar 1328 Hijiria, ambapo baada ya kuhitimu masomo yake ya awali mjini Sabzawari na Khorasan, alihamia mjini Najaf na kufanya makazi yake huko. Akiwa mjini Najaf alisoma elimu ya kidini kutoka kwa maulama wakubwa wa zama hizo akiwemo Ayatullah Mirza Naini, Ayatullah Agha Dhiyaud-Din Iraqi, Sayyid Abul-Hassan Isfahani na Sheikh Muhammad Hussein Gharawi Isfahani na kutabahari katika elimu ya fiqhi na usulu fiqhi sambamba na kufikia daraja ya Ijtihad.