Dec 11, 2016 08:17 UTC
  • Jumapili  11 Disemba, 2016

Leo Jumapili tarehe 11 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1438 Hijria sawa na Disemba 11, 2016.

Katika siku kama ya leo miaka 206 iliyopita Alfred Louis Charles de Musset-Pathay malenga na mwandishi mwashuhuri wa Ufaransa alizaliwa katika familiayenye kuzingatia misingi ya utamaduni mjini Paris, Ufaransa. Musset akiwa na umri wa miaka 19 aliandika diwani yake ya kwanza ya mashairi kwa jina la Simulizi za Uhispania na Italia na hivyo kupata umashuhuri mkubwa kutokana na mbinu yake mpya ya uandishi na hivyo akapata hadhi katika jamii ya mabingwa wa fasihi Ufaransa. Akiwa na umri wa miaka 22 aliandika  tamthilia yake ya kwanza iliyoibua utata kutokana na masuala ya umaanawi na maadili. Fikra zake huru zilipelekea awe miongoni mwa waandishi waatajika wa nusu ya kwanza ya karen ya 19. Alfred de Musset aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 47 mwaka 1857.

Alfred de Musset

Tarehe 11 Disemba miaka 173 iliyopita alizaliwa daktari na mtaalamu wa vividudu maradhi wa Kijerumani aliyevumbua ugonjwa wa kifua kikuu,  Robert Koch. Baada ya kukamilisha masomo katika taaluma ya tiba, Robert Koch alijishughulisha na kutiwa wagonjwa katika miji mbalimbali ya Ujerumani sambamba na kufanya uhakiki kuhusu maradhi tofauti. Tarehe 24 Machi mwaka 1882 alifanikiwa kuvumbua ugonjwa wa kifua kikuu (TB). Katika safari zake nyingi barani Afrika, tabibu huyo wa Kijerumani pia alibaini kuwa ugonjwa wa malale uliokuwa ukisababisha vifo vya Waafrika wengi ulikuwa ukisababishwa na mdudu anayeitwa mbung'o.

Robert Koch

Siku kama ya leo miaka 145 iliyopita tarehe 11 Raibul Awwal mwaka 1293 Hijria Qamaria alizaliwa mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Allamah Agha Bozorge Tehrani. Alipata elimu ya msingi mjini Tehran na baadaye alielekea Najaf, Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Allamah Agha Bozorge Tehrani alikweya kwa kasi daraja za elimu na kuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa kidini. Allamah Tehrani alisafiri na kufanya uchunguzi katika maktaba nyingi za nchi kama Iran, Misri, Syria, Iraq, Hijaz, Palestina na kadhalika kwa ajili ya kutayarisha ensaiklopedia ya vitabu vya Kiislamu. Alifanikiwa kuandika tabu hilo kubwa lenye juzuu 26 ambalo alilipa jina la "Adhari'a ila Tasaanifish Shia". Kitabu kingine muhimu cha Allamah Agha Bozorge Tehrani ni "Tabaqatu Aalami Shia" chenye juzuu 8. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia katika mji mtakatifu wa Najaf na kuzikwa katika maktaba yake kama alivyokuwa ameusia.

Ayatullah Agha Bozirg Tehrani (katikati)

Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita yaani mwaka 1946, Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) uliasisiwa baada ya kupasishwa suala hilo kwa wingi wa kura. Kwa utaratibu huo, taasisi hiyo ikaanza rasmi shughuli zake chini ya Baraza la Masuala ya Kijamii la Umoja wa Mataifa. Awali Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF), ulikuwa na jukumu la kuwahudumia watoto waliojeruhiwa katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Hata hivyo baadaye asasi hiyo muhimu ikapanua zaidi shughuli zake na kuanza kuandaa mahitaji ya kimsingi maishani kama chakula, elimu na malezi kwa watoto waliokosa haki hizo za kimsingi. Makao makuu ya UNICEF yapo mjini New York, Marekani.

Siku kama ya leo yaani tarehe 11 Disemba mwaka 1958 Burkina Faso ilitangazwa kuwa Jamhuri.

Tangu mwanzoni mwa karne ya 19 nchi hiyo ilikuwa chini ya utawala na ukoloni wa Ufaransa. Burkina Faso ambayo hapo kabla ilikuwa ikiitwa Upper Volta, mnamo mwaka 1958 ilijitangazia utawala wa ndani wa jamhuri. Hata hivyo iliendelea kuwa sehemu ya Ufaransa. Miaka miwili baadaye yaani tarehe 5 Agosti 1960, Burkina Faso ilijipatia uhuru kamili sambamba na kukubaliwa kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. 

Bendera ya Burkina Faso

Mwaka 1984 jina la nchi hiyo lilibadilishwa rasmi kutoka Upper Volta na kuitwa Burkina Faso. Nchi ya Burkina Faso ina ukubwa wa karibu kilomita mraba 274,000 na inapatikana Magharibi mwa Afrika ikipakana na nchi za Mali, Ivory Coast, Ghana, Togo, Benin na Niger.