Dec 26, 2016 04:31 UTC
  • Jumatatu, tarehe 26 Disemba, 2016

Leo ni Jumatatu tarehe 26 Rabiul Awwal sawa na Tarehe 26 Disemba 2016.

Siku kama ya leo miaka 12 iliyopita mtetemeko mkubwa wa ardhi uliokuwa na daraja 9 kwa kipimo cha Rishta ulitokea katika Bahari ya Hindi na kusababisha mawimbi makubwa ya Tsunami. Mawimbi hayo yalisambaa na kuenea kwa kasi kubwa katika nchi kadhaa za kandokando ya bahari hiyo na kusababisha maafa makubwa. Kitovu cha mtetemeko huo kilikuwa maji ya kusini mashariki mwa Asia na kwa msingi huo nchi za India, Indonesia, Sri Lanka na Thailand ndizo zilizoathiriwa zaidi na mtetemeko huo. Tsunami iliyosababishwa na mtetemeko huo ilisababisha vifo vya watu wasiopungua laki mbili na elfu 20 na kuharibu nyumba za watu milioni mbili. Nchi hizo pia zilipata hasara ya mamilioni ya dola.

Athari za mtetemeko wa ardhi na Tsunami ya Bahari ya Hindi

Miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani liliivamia ardhi ya Afghanistan. Uvamizi huo wa Russia unatambuliwa na kizazi kipya cha viongozi wa nchi hiyo kuwa ni miongoni mwa makosa makubwa ya ikulu ya Kremlin katika siasa zake za nje. Uvamizi huo wa Urusi ulifanyika kutokana na ombi la rais wa zamani wa Afghanistan Babrak Karmal. Tangu wakati huo Mujahidin wa Afghanistan walianza mapambano dhidi ya jeshi la askari laki moja na 30 elfu la jeshi Jekundu (Red Army). Katika upande mwingine Marekani ambayo ilitambua kuwepo kwa Urusi ya zamani huko Afghanistan kuwa ni hatari kwa maslahi yake ilianza kuunda makundi ya wapiganaji na kuyasaidia kwa mali na silaha kwa ajili ya kukabiliana na Urusi. Makumi ya maelfu ya watu waliuawa na wengine kufanywa vilema katika kipindi cha miaka 10 ya uvamizi wa Urusi huko Afghanistan.

Mashambulizi ya Jeshi Jekundu nchini Afghanistan

Miaka 1094 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 26 Rabiul Awwal mwaka 344 alifariki dunia Ebn Sammak mtaalamu mkubwa wa masuala ya itikadi ya Kiislamu huko Baghdad.

Hata hivyo historia haijaweka wazi tarehe na mahala alipozaliwa msomi huyo, ila habari zinazojulikana ni kwamba msomi huyo aliishi Baghdadi katika himaya ya wasomi wa mji huo, pia msomi huyo naye alipata kuwalea wasomi wengine mashuhuri akiwemo Hakim Nishaburi.

Miongoni mwa vitabu vya Ebn Sammak ni kitabu cha "al Aamal" na vitabu vingine kadhaa kuhusu fadhila za Mtukufu Mtume Muhammad (saw).

ابن سماک