Jan 03, 2017 10:26 UTC

Sura ya Al-Qas’as’, aya ya 51-55 (Darsa ya 694)

 

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 694, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 28 ya Al-Qas’as’. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 51 na 52 ambazo zinasema:

وَلَقَدْ وَصَّلْنَا لَهُمُ الْقَوْلَ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ

Na kwa hakika tumewafululizia maneno (ya aya za Qur’ani) ili wapate kukumbuka.

الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ مِن قَبْلِهِ هُم بِهِ يُؤْمِنُونَ

Wale tulio wapa Kitabu kabla yake wanaiamini (Qur’ani).

Aya hizi kwanza zinaashiria ukanushaji na ukaidi wa washirikina na kueleza kwamba: Sisi tumeziteremsha aya za Qur'ani kidogo kidogo lakini kwa mfuatano ili ziweze kupenya na kuwa na athari ndani ya nyoyo za washirikina, hata hivyo hawakuzinduka na wakayakataa maneno ya haki. Hali ya kuwa baadhi ya Ahlul Kitab ambao walikuwa wamemwamini Mtume mwengine na kitabu kingine, wakati walipobainikiwa na ukweli wa Nabii Muhammad SAW wamemwamini na kumfuata. Kwa mfano, kama maandiko ya historia yanavyoeleza, baadhi ya makasisi wa ardhi ya Uhabeshi, yaani Ethiopia ya sasa, kwa ushauri wa mfalme wa nchi hiyo Najjashi, walifunga safari na kuelekea Makka ili kuchunguza na kuielewa dini aliyokuja nayo Bwana Mtume SAW. Makasisi hao waliyasikiliza maneno ya haki na yenye kuathiri nyoyo ya Nabii huyo wa rehma wakasilimu na wakawa walinganiaji wa dini ya Uislamu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba malezi na mafunzo ni suala la taratibu na la hatua kwa hatua linalohitaji kutumia njia ya miongozo na ukumbushaji, si utwishaji na ulazimishaji. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa vitabu vyote vya mbinguni na Mitume wote wa Allah wamekuja na wito mmoja na wenye lengo moja. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba Ahlul Kitab wa kweli, yaani Mayahudi na Wakristo ni wale ambao baada ya kumtambua Bwana Mtume Muhammad SAW na dini ya Uislamu aliyokuja nayo wanasilimu na kumwamini na wala hawaendelei kufanya taasubi ya kushikilia itikadi na mafundisho yaliyokwisha potoshwa ya Mitume wao Musa na Isa (AS).

Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya za 53 na 54 ambazo zinasema:

وَإِذَا يُتْلَى عَلَيْهِمْ قَالُوا آمَنَّا بِهِ إِنَّهُ الْحَقُّ مِن رَّبِّنَا إِنَّا كُنَّا مِن قَبْلِهِ مُسْلِمِينَ

Na wanapo somewa wanasema: Tunaiamini. Hakika hiyo ni Haki inayo toka kwa Mola wetu Mlezi. Hakika sisi kabla yake tulikuwa ni Waislamu, tulio nyenyekea.

أُوْلَئِكَ يُؤْتَوْنَ أَجْرَهُم مَّرَّتَيْنِ بِمَا صَبَرُوا وَيَدْرَؤُونَ بِالْحَسَنَةِ السَّيِّئَةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ

Basi hao watapewa ujira wao mara mbili kwa walivyo vumilia, na wakaondoa ubaya kwa wema, na wakatoa katika tuliyo waruzuku.

Aya hizi zinaendelea na maudhui iliyoashiriwa katika aya zilizotangulia na kueleza kwamba: Wale Ahlul Kitab ambao walisilimu na kumwamini Bwana Mtume Muhammad SAW ni watu wenye nyoyo safi na salama na zenye kunyenyekea mbele ya haki, kiasi kwamba wakati mtukufu huyo anapowasomea aya za Qur'ani wanasema: sisi tunajua kuwa haya yanatoka kwa Mwenyezi Mungu na tunayaamini; kwani kabla ya kufikiwa na haya pia tulimwamini na kumtii Mtume wetu aliyetujia. Qur'ani tukufu inasema: ni kwa sababu hiyo, watu hao watapata malipo ya thawabu mara mbili; ya kwanza kwa kuamini Kitabu na Mtume wao aliyetangulia; na ya pili kwa kusilimu na kumwamini Nabii Muhammad SAW na kitabu alichokuja nacho. Kisha Allah SW anawazungumzia waumini wenye nyoyo safi na nyofu kwa kusema: Wao ni watu wanaolipa ubaya kwa wema. Wanapozungumza nao watu kwa kutumia lugha chafu, wao hujibu kwa kutumia lugha ya maneno mazuri; huwa na subira ya kuvumilia mwenendo mbaya wa watu, na wanapofanyiwa uadui huonyesha upendo na huruma; na wao ni watu wenye kutoa kuwasaidia wanyonge na wahitaji. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba watu wenye kuipenda haki huikubali na kuifuata. Si kipimo kwao wao ni nani aliyesema, ana asili gani, na kwa lugha gani ameyasema maneno ya haki; suala la msingi kwao ni haki yenyewe; hilo ndilo muhimu kwao. Kwa hivyo mtu yeyote ambaye ameisema haki inapasa tumkubali na kuifuata haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kuikubali na kuifuata haki kunahitaji subira na kusimama imara kukabiliana na kila aina ya matatizo na upinzani. Wa aidha aya hizi zinatufunza kwamba msingi katika mahusiano ya kijamii na kuamiliana na watu ni kufumbia macho makosa na kumsamehe anayetukosea. Lakini daraja ya juu zaidi ya hilo ni kuwatendea wema wale waliotufanyia ubaya.

Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 55 ya sura yetu ya Al-Qas'as ambayo inasema:

وَإِذَا سَمِعُوا اللَّغْوَ أَعْرَضُوا عَنْهُ وَقَالُوا لَنَا أَعْمَالُنَا وَلَكُمْ أَعْمَالُكُمْ سَلامٌ عَلَيْكُمْ لا نَبْتَغِي الْجَاهِلِينَ

Na wanapo sikia upuuzi hujitenga nao na husema: Sisi tuna amali zetu, na nyinyi mna amali zenu. Salamun Alaikum, Amani juu yenu! Sisi hatutaki kujibizana na wajinga.

Aya hii inaendelea na maudhui iliyozungumziwa katika aya zilizotangulia kwa kuashiria moja ya vielelezo na mifano hai ya subira katika kukabiliana na maneno na mwenendo muovu wa baadhi ya watu na kueleza kwamba: waumini wa kweli wanapoandamwa kwa maneno machafu na ya matusi huwa hawalipizi kwa waliyofanyiwa kwa kujibizana na watu hao kwa kutumia lugha chafu na ya matusi. Bali huamiliana na watu hao kwa upole na kuwajibu kwa heshima kwamba: kama njia yetu na mwenendo wetu sisi si sahihi, athari na madhara yake yataturejea sisi wenyewe, sio nyinyi. Na ikiwa muyafanyayo nyinyi pia si sahihi, athari na madhara yake yatakurejeeni nyinyi wenyewe, sio sisi. Kwa hivyo nyinyi fuateni njia yenu, na sisi tunafuata yetu! Sisi hatutaki kufanya mambo ya kijahili. Ikiwa nyinyi mnaamiliana na kulahikiana nasi vibaya na kwa lugha chafu sisi hatutokufanyieni hivyo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba moja ya masharti ya kuwa na imani ya kweli juu ya Allah ni kujiepusha na maneno ya lahau na upuuzi pamoja na lugha chafu na ya matusi. Tusiwaambie watu maneno ya upuuzi wala tusiwalipizie watu wanaotumia lugha ya kejeli na dharau dhidi yetu, kwa sababu muumini wa kweli hujiepusha na kujiweka mbali na lugha kama hizo za maneno ya upuuzi, dharau na matusi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kujipeusha na lahau na upuuzi katika uzungumzaji, usikilizaji, utazamaji na katika kulahikiana na kuchanganyika na watu ni sifa njema ambayo imesifiwa na kutukuzwa na dini zote za mbinguni. Aidha kwa mujibu wa aya hii inatubainikia kwamba ikiwa tutahisi kukataza kwetu maovu hakuna taathira basi jambo tunalopaswa kufanya ni angalau kujiweka mbali na maovu hayo na anayeyafanya ili aweze kufahamu kuwa sisi haturidhii wala hatuko tayari kuwa pamoja naye katika maovu yake hayo. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 694 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa wenye kupendeza kwa watu kwa tabia na mwenendo wetu, si kwa maumbile na dhahiri yetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/