Sura ya Al-A'nkabut 1-7 (703)
Sura ya Al-A'nkabut, aya ya 1-7 (Darsa ya 703)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Baada ya kuhatimisha tarjumi na maelezo ya sura ya 28 ya Al-Qas'as', katika darsa hii ya 703 tutaanza kutoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 29 ya Qur'ani tukufu ya Al-A'nkabut. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya kwanza hadi ya tatu ya sura hiyo ambazo zinasema:
الم
Alif Lam Mim (A.L.M.)
أَحَسِبَ النَّاسُ أَن يُتْرَكُوا أَن يَقُولُوا آمَنَّا وَهُمْ لا يُفْتَنُونَ
Je! Wanadhani watu wataachwa kwa kuwa wanasema: Tumeamini. Nao wasijaribiwe?
وَلَقَدْ فَتَنَّا الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَلَيَعْلَمَنَّ اللَّهُ الَّذِينَ صَدَقُوا وَلَيَعْلَمَنَّ الْكَاذِبِينَ
Hakika tuliwajaribu walio kuwa kabla yao. Kwa yakini Mwenyezi Mungu atawatambulisha walio wa kweli na atawatambulisha walio waongo.
Jina la sura hii kama zilivyo baadhi ya sura nyengine za Qur'ani limetokana na jina la wanyama wa jamii ya wadudu kama alivyotajwa ndani ya sura yenyewe. Ni aya ya 41 ya sura hii ya A'nkabut inayoeleza kuwa msingi wa shirki ni dhaifu na legevu mno kama ulivyo utando wa buibui.
Suratul A'nkabut ni miongoni pia mwa sura za Qur'ani tukufu zilizoanza kwa herufi za mkato. Tuliwahi kuashiria hapo kabla katika maelezo ya sura zenye sifa hii, kwamba herufi za mkato ni herufi zenye sura ya fumbo zinazomaanisha kwamba Qur'ani, muujiza wa Allah, imetokana na herufi hizi hizi za kawaida za alfabeti; kwa hivyo kama na nyinyi mnaweza, tumieni herufi hizo hizo kuleta na kuwaonesha walimwengu kitabu mithili ya Qur'ani. Aya za mwanzo za sura hii zinaashiria utaratibu na kaida moja kuu ya Allah inayowagusa watu wote katika zama zote za historia; ni kaida ya kutahiniwa na Mola, kunakodhihirisha na kuweka wazi nia na batini za watu na kuwapambanua walio wakweli na waongo miongoni mwa wanaodai kuwa waumini wa kweli.
Kila mara kunakuwepo watu wanaojihesabu wenyewe kuwa ni waumini wa kweli na kujidhania kuwa ni waja waliosalimu amri mbele ya maamrisho ya Mola; lakini wakati watu hao wanapokabiliwa na baadhi ya shida na misukosuko kwa sababu ya imani zao hubadilika na kuporomoka imani zao kirahisi kabisa. Na hapo ndipo inapodhihirika kwamba watu hao hawako kama ilivyokuwa ikidhaniwa.
Baadhi ya watu pia ni wanafiki, ambao hawana imani ndani ya nyoyo zao, lakini kwa kuwa wanaishi katika jamii ya Kiislamu hujitambulisha kuwa Waislamu na kuchunga mambo ya dhahiri ya dini ili kulinda maslahi yao ya kupita ya kidunia. Watu wa aina hii pia wakati wanapokabiliwa na matatizo na misukosuko unafiki na dhati yao ya nyuso mbili hufichuka na kudhihirika. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba imani si kutamka kwa ulimi tu na kwa kauli za hamasa na majigambo, bali inathibiti kwa mitihani na majaribu ya Allah. Mtu anapaswa kuonesha kwa matendo kwamba yuko tayari kufanya lolote la kujitolea mhanga ili kulinda imani yake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa mitihani na majaribu ni utaratibu thabiti alioweka Allah katika zama zote za historia; na kila mtu huwa anajaribiwa na kutahiniwa kwa namna yake. Tajiri kwa utajiri wake, masikini kwa umasikini wake, mwenye madaraka kwa mamlaka yake na mnyonge kwa udhaifu wake.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 4 na ya 5 ambazo zinasema:
أَمْ حَسِبَ الَّذِينَ يَعْمَلُونَ السَّيِّئَاتِ أَن يَسْبِقُونَا سَاء مَا يَحْكُمُونَ
Au wanadhani wanao tenda maovu kwamba watatushinda? Hukumu mbaya hiyo wanayo hukumu.
مَن كَانَ يَرْجُو لِقَاء اللَّهِ فَإِنَّ أَجَلَ اللَّهِ لَآتٍ وَهُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ
Mwenye kutaraji kukutana na Mwenyezi Mungu, basi hakika miadi ya Mwenyezi Mungu itafika bila ya shaka. Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
Baada ya aya zilizotangulia ambazo zilielezea kanuni na kaida jumla ya mitihani na majaribu ya Allah kwa waja wote, aya hizi zinayahutubu makundi mawili ya waumini na makafiri na kuwapa indhari makafiri kwa kuwaambia, wasidhani kwamba wanaweza kuikwepa na kuiepuka adhabu ya Mwenyezi Mungu na kuzishinda nguvu na uwezo wa Mola. Kumwasi kwao Mwenyezi Mungu na maudhi na manyanyaso wanayowafanyia waumini, yote hayo yamehifadhiwa, na yatakwenda kuhesabiwa na kulipwa adhabu yake mbele ya mahakama ya uadilifu ya Allah SW.
Kwa upande mwengine, waumini nao wanausiwa wajitahidi kufanya t’aa na ibada kadiri ya uwezo wao, wala wasiyumbe na kurudi nyuma kiimani kwa sababu ya vitimbi vya maadui au matatizo wanayokabiliana nayo; kwa sababu ahadi ya Allah kuhusu Kiyama ni ya hakika na yakini. Siku hiyo, pazia la vizuizi vya kimaada litararuka, hakika ya mambo itadhihirika, na wao watakuwa katika hadhi na nafasi ya kuondolewa hijabu na kizuizi baina yao na Mola wao na hivyo wataweza kuliona waziwazi dhihirisho la haki. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kufanya na kuendelea kutenda dhambi kuna taathira hasi kwa uono na mtazamo wa mtu, kwani humfanya atanzwe na fikra potofu na dhana zisizo sahihi kuhusu Mwenyezi Mungu na mfumo mzima wa ulimwengu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa wafanya maasi wasiingiwe na ghururi kwa sababu ya muhula waliopewa na Mola, kwa sababu fursa zina mwisho wake, na Kiyama, bila ya shaka yoyote kinakuja tu. Na wafanya mema wasiyumbe wala kutetereka katika subira bali waendelee kuwa thabiti kiimani, kwani ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya uhakika kabisa.
Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 6 na ya 7 ambazo zinasema:
وَمَن جَاهَدَ فَإِنَّمَا يُجَاهِدُ لِنَفْسِهِ إِنَّ اللَّهَ لَغَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ
Na anaye fanya juhudi basi bila ya shaka anafanya juhudi kwa ajili ya nafsi yake. Hakika Mwenyezi Mungu si mhitaji wa walimwengu.
وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَنُكَفِّرَنَّ عَنْهُمْ سَيِّئَاتِهِمْ وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَحْسَنَ الَّذِي كَانُوا يَعْمَلُونَ
Na walioamini na wakatenda mema, kwa yakini tutawafutia makosa yao, na tutawalipa mazuri zaidi ya waliyokuwa wakiyatenda.
Mtu muumini wapenzi wasikilizaji, si mtu wa kujitenga, kujibanza na wa kukaa tu vivihivi; ni mtu amilifu na wa harakati. Muumini anapaswa afanye juhudi na bidii kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Uislamu na Waislamu, na inapolazimu kuingia kwenye jihadi na kupambana na maadui wa dini. Hapana shaka yoyote kuwa Mwenyezi Mungu si mhitaji wa chochote kwa waumini, wala wa jitihada na idili wanayoifanya kwa ajili ya kuilinda dini; kwani yote wayafanyayo ni kwa manufaa ya nafsi zao wenyewe. Tab’an Allah SW ameahidi kuwa watu kama hao watapata rehma na fadhila zake maalumu. Lakini pia atawasamehe kwa kukosea na kuteleza kwao na atawapa malipo bora na ya juu zaidi ya thawabu kwa mema waliyoyafanya. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba makusudio ya jihadi katika aya hizi si ya vita na kitali pekee ya kupambana na maadui. Muradi wa aya ni kila aina ya jitihada kubwa afanyayo muumini. Inaweza jithada hiyo ikawa ni katika kuijenga mtu nafsi yake yaani Jihadi ya Nafsi, au ya kuzima njama za maadui katika uga wa siasa, uchumi na utamaduni. Yote hayo ni aina za jihadi, na hakuna shaka kwamba manufaa yake yanawarudia Waislamu wenyewe. Aidha aya hizi zinatuelimisha kuwa ikiwa tutafanya bidii na juhudi katika njia ya Allah na dini yake, Yeye Mola atatusamehe kwa taksiri zetu, kukosea kwetu na kuteleza kwetu, na atazilipa juhudi zetu kwa malipo ya namna bora kabisa. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 703 na ya kwanza kabisa iliyotoa tarjumi na maelezo ya Suratul- A’nkabut imefikia tamati. Tunamwomba Allah atughufirie madhambi yetu, azitakabali dua zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/