Jan 24, 2017 09:27 UTC

Sura ya Ar-Rum, aya ya 27-29 (Darsa ya 722)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwingine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 722 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 30 ya Ar-Rum. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 27 ambayo inasema:

وَهُوَ الَّذِي يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ وَهُوَ أَهْوَنُ عَلَيْهِ وَلَهُ الْمَثَلُ الأَعْلَى فِي السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ

Na Yeye ndiye anaye anzisha uumbaji, kisha ataurudisha mara nyengine. Na jambo hili ni jepesi zaidi kwake. Naye ndiye mwenye mfano bora katika mbingu na ardhi. Na Yeye ndiye Mwenye uwezo, Mwenye hikima.

Katika aya tulizosoma katika darsa kadhaa zilizopita, Qur'ani tukufu imeashiria alama na ishara za Allah SW katika ulimwengu wa uumbaji, ishara ambazo zinadhihirisha elimu, uwezo na hekima isiyo na ukomo ya Mola Muumba. Aya hii imeendelea na maudhui hiyo kwa kugusia suala la ma'adi na kufufuliwa viumbe na kueleza kwamba: Mungu huyo huyo aliyeanzisha uumbaji ni Muweza wa kuvirudisha tena Siku ya Kiyama viumbe alivyoviumba mara ya kwanza. Japokuwa kwa Mwenyezi Mungu hakuna jambo lolote lililo gumu zaidi au rahisi zaidi kulifanya kulinganisha na jingine kwa kuwa ugumu na wepesi wa kufanya jambo unatuhusu sisi wanadamu ambao tunabanwa na vitu chungu nzima katika ufanyaji mambo hayo lakini katika aya tuliyosoma Mwenyezi Mungu amezungumza kwa kutumia lugha yetu sisi wanadamu ili iwe wepesi zaidi kwetu kufahamu na kuukubali ukweli huo. Kwa sababu hiyo akasema: Wakati kukuumbeni tena nyinyi wanadamu ni rahisi zaidi kuliko kukuumbeni mara ya mwanzo kabla ya kuwepo kwenu, hivi kweli Mwenyezi Mungu Mtukufu asiyebanwa na mpaka wa kitu chochote na Mwenye sifa zote za ukamilifu atashindwa kuifanya kazi hiyo? Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba sifa za Mwenyezi Mungu ni za juu na zilizotukuka zaidi ya zinavyoweza kusawirika na kuelezewa na wanadamu; na hakuna yeyote wala chochote kinachoweza kulinganishwa na Yeye. Yeye ni wa juu zaidi kwa viumbe katika hali zote. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kutokana na hekima isiyo na ukomo ya Allah SW inapasa uwepo ulimwengu mwingine baada ya kufa viumbe; na kifo kisiwe ndio hatima na mwisho wa mwanadamu.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 28 ambayo inasema:

ضَرَبَ لَكُم مَّثَلا مِنْ أَنفُسِكُمْ هَل لَّكُم مِّن مَّا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُم مِّن شُرَكَاء فِي مَا رَزَقْنَاكُمْ فَأَنتُمْ فِيهِ سَوَاء تَخَافُونَهُمْ كَخِيفَتِكُمْ أَنفُسَكُمْ كَذَلِكَ نُفَصِّلُ الآيَاتِ لِقَوْمٍ يَعْقِلُونَ

Amekupigieni mfano kutokana na nafsi zenu. Je! Katika hao iliyo wamiliki mikono yenu ya kulia mnao washirika katika hivyo tulivyo kuruzukuni, mkawa nyinyi katika hivyo ni sawasawa, mkawahofia kama mnavyo hofiana wenyewe kwa wenyewe? Namna hivi tunazipambanua Aya zetu kwa watu wenye akili. 

Washirikina walikuwa wakimfanyia Mwenyezi Mungu washirika aina kwa aina ambao walikuwa viumbe tu wa Mwenyezi Mungu, lakini wao waliwaona waungu hao bandia wana uwezo na taathira katika masuala ya ulimwengu kama alivyo Allah SW. Aya tuliyosoma inaivunja imani hiyo potofu ya washirikina kwa kutoa mfano unaowahusu watu wenyewe kwa kusema: Ikiwa nyinyi mtakuwa mnamiliki watumwa, je mtawaruhusu wawe na mamlaka ya kutumia na kumiliki mali zenu? Je mtawafanya wao washirika wenu ambao wana haki ya kutumia mali zenu kama mnavyotumia nyinyi wenyewe? Inakuwaje nyinyi hamkubali mnaowamiliki wawe na hadhi sawa na nyinyi wenyewe lakini mnawaweka viumbe wa Mwenyezi Mungu ambao wote ni milki yake Yeye Allah kwenye hadhi sawa na Yeye na mnawapa haki ya kuingilia mamlaka ya Mwenyezi Mungu kwa kuwafanya waweza wa kufanya mambo mbalimbali katika ulimwengu wa uumbaji?

Kama hao mnaowamiliki nyinyi ni washirika wenu na wana hadhi sawa na nyinyi basi viumbe wa Allah, nao pia wanaweza kuwa washirika wake Mola! Lakini kama nyinyi hamkubali mnaowamiliki wawe na mamlaka ya kutumia mali zenu bila ya idhini yenu inakuwaje basi mnakubali na mnathubutu kuwapa mamlaka viumbe wa Mwenyezi Mungu ya kuingilia masuala yanayomhusu Yeye Mola bila ya idhini yake? Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba dhamiri ya ndani ya nafsi ni hakimu bora kabisa wa kumwamulia mtu. Sisi watu, ambao hatukubali katu wanadamu wenzetu ambao ni watu kama sisi wawe washirika na wenye hadhi sawa na sisi kwa sababu tu ni watumishi, wafanyakazi na vibarua walio chini ya mamlaka yetu; sasa inakuwaje tunawafanya watu au vitu ambavyo havina mshabihiano wowote na Mwenyezi Mungu bali ni viumbe alivyoviumba Yeye wawe na hadhi sawa na Yeye na kuwafanya washirika wake? Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa aya za Qur’ani zinamhutubu mwanadamu kwa msingi wa akili na mantiki na daima zinawataka watu watumie akili na kutafakari juu ya mambo.

Tunaihatimisha darsa yetu ya leo kwa aya ya 29 ambayo inasema:

بَلِ اتَّبَعَ الَّذِينَ ظَلَمُوا أَهْوَاءهُم بِغَيْرِ عِلْمٍ فَمَن يَهْدِي مَنْ أَضَلَّ اللَّهُ وَمَا لَهُم مِّن نَّاصِرِينَ

Bali walio dhulumu wamefuata hawaa zao pasina kujua. Basi nani atamwongoa ambaye Mwenyezi Mungu amemuacha apotee? Wala hao hawatakuwa na wa kuwanusuru

Aya hii inaendelea kuzungumzia maudhui ya aya iliyotangulia kwa kutoa mfano unaokubalika na akili na mantiki kwa kueleza kwamba watu wanaomfanyia Allah washirika wamejiweka mbali na akili na mantiki kwa kutekwa na matashi na matamanio ya nafsi zao. Watu hao, pasina kuwa na hoja ya kielimu, wameingia katika shirki, na matokeo yake ni kuzifanyia dhulma kubwa kabisa nafsi zao wenyewe. Watu wanaoacha kutumia akili na elimu na badala yake wakaamua kufuata hawaa na matamanio ya nafsi zao, matokeo ya hatua yao hiyo ni kupotoka; na wala hakuna matumaini ya wao kuongoka. Kwa sababu sharti la kuongoka ni kutumia akili na mantiki ili kuweza kubaini hakika zinazofikisha kwenye elimu na uelewa. Lakini yule ambaye hataki kutafuta hakika ya mambo akawa anapigania tu kupata matakwa yake mtu kama huyo ni mwenye kufuata matamanio ya nafsi yake; si akili aliyojaaliwa na Mola. Mwanadamu anapokuwa na sifa kama hiyo hawezi kufika popote na wala hakuna mtu awezaye kumsaidia ila pale yeye mwenyewe atakapoacha kufuata hawaa na matamanio ya nafsi yake na kurejea kwenye njia ya akili na mantiki. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba ukengeukaji wowote wa njia iliyonyooka ya Tauhidi ni aina mojawapo ya dhulma anayoifanyia mtu nafsi yake; na katika mafundisho ya Uislamu ubaya wa kuidhulumu nafsi hautofautiani na kuwafanyia dhulma watu wengine, kwa sababu kuifanyia dhulma mtu nafsi yake hufuatiwa na dhulma kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kumshirikisha Mwenyezi Mungu ambako leo hii kunaendelea kufanywa katika dini kama za Mabuda na Wahindu kwa sura ya kuabudu masanamu yenye maumbo ya watu na wanyama wa aina mbalimbali, kunadhihirisha ujahilia wa wanadamu katika zama na karne za sasa. Mwanadamu wa leo anapiga hatua mbele za maendeleo katika mambo yote kwa kutumia nyenzo za akili na elimu lakini katika imani yake juu ya asili ya ulimwengu na uumbwaji ametingwa na ujahili, khurafa na imani za uzushi.  Wapenzi wasikilizaji darsa ya 722 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuoneshe haki na kutupa taufiqi ya kuifuata na atuoneshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/ 

 

Tags