Feb 23, 2017 04:35 UTC
  • Jumatano, 22 Februari, 2017

Leo ni Jumatano tarehe 24 Jamadil Awwal 1438 Hijria sawa na tarehe 22 Februari, 2017

Siku kama ya leo miaka 11 iliyopita, Haram mbili takatifu za Maimamu al Hadi na Hassan al Askari katika mji wa Samarra nchini Iraq, ziliharibiwa vibaya kwenye mlipuko wa mabomu kadhaa. Maimamu hao ni wajukuu na watu wa nyumba ya Mtume SAW. Kitendo cha kuharibiwa sehemu kubwa ya haram hizo, kiliwakasirisha mno Waislamu na hasa wafuasi wa Ahlul Bayt wa Mtume SAW. Shambulio hilo lilifanyika kwa lengo la kuzusha vita vya ndani vya kimadhehebu kati ya Waislamu wa Kishia na Kisuni. Hata hivyo kuwa macho wananchi wa Iraq na viongozi wa kidini wa nchi hiyo kulisambaratisha njama hizo.

Haram ya Maimamu al Hadi na Hassan al Askar (as)

Siku kama ya leo miaka 7 iliyopita Abdulmalik Rigi kiongozi wa kundi la kigaidi la Jundullah lenye makao yake huko Pakistan, alitiwa mbaroni katika oparesheni tata ya kiintelijinsia iliyofanywa na maajenti wa Wizara ya Usalama wa Ndani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baada ya kufanya mashambulizi mengi ya kigaidi, gaidi huyo katili alikuwa safarini kuelekea nchini Kyrgyzstan akitokea Dubai, Imarati, kwenda kukutana na kufanya mazungumzo na kiongozi mmoja wa ngazi ya juu wa Marekani. Hata hivyo wana usalama wa Iran waliokuwa wakifuatilia kwa karibu nyendo zake waliweza kuitambua ndege iliyokuwa imembeba gaidi huyo na kuisubiri iingie katika anga ya Iran na hivyo kuilazimisha kutua katika uwanja wa ndege wa Bandar Abbas wa kusini mwa Iran na baadae wakamtia mbaroni kiongozi huyo wa kundi la kigaidi la Jundullah. Rubani wa ndege hiyo alifanya jitihada kubwa za kutoroka na kutoka nje ya anga ya Iran, lakini alizidiwa nguvu na maafisa usalama wa Iran, na kulazimishwa kuishusha chini ndege hiyo kabla haijaingia kwenye anga ya Imarati. Abdulmalik Rigi alifanya jinai nyingi ikiwa ni pamoja na kutega na kuripua mabomu katika maeneo ya umma nchini Iran, kuwauwa kwa umati raia pamoja na kuwateka nyara. Rigi hakuwa na huruma hata kwa watu wake wa karibu. Abdulmalik Rigi alikiri kwamba alikuwa anapata misaada ya kila namna ikiwemo ya kifedha na kisilaha kutoka kwa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kama njia ya kuliwezesha kundi lake lifanye mauaji ya watu ndani ya Iran hususan katika maeneo ya kusini mashariki mwa Iran na kusababisha mizozo ya kimadhehebu katika maeneo hayo. Gaidi huyo alinyongwa tarehe 30 Khordad mwaka 1389 Hijria Shamsia sawa na tarehe 20 Juni, 2010 Milaadia yaani miezi minne baada ya kutiwa mbaroni. Kukiri huko kwa Rigi kunaonyesha wazi madai ya uwongo ya serikali ya Marekani ya eti inapambana na ugaidi.

Gaidi Abdulmalik Rigi akiwa mikononi wma wanausalama wa Iran

Tarehe 4 mwezi Esfand miaka 37 iliyopita, Ayatullah Dakta Muhammad Husseini Beheshti aliteuliwa kuwa mkuu wa kwanza wa Mahakama Kuu ya Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Hatua hiyo ilichukuliwa na Imam Ruhullah Khomeini baada ya kupasishwa Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu na kuundwa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge. Dakta Beheshti alikuwa miongoni mwa wanafikra wakubwa na shakhsia mashuhuri wa Mapinduzi ya Kiislamu. Msomi huyo aliuawa kigaidi katika shambulizi la bomu lililotekelezwa na kundi la kigaidi la MKO mwaka 1360 Hijria Shamsia.

Ayatullah Dakta Muhammad Husseini Beheshti

Miaka 59 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 22 Februari mwaka 1958, Abul Kalam Ahmad Azad, msomi, khatibu na mwanasiasa wa India alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 70. Abul Kalam Azad alianza harakati za kisiasa akiwa na umri wa miaka 17 na harakati zake zilikuwa  dhidi ya utawala wa kikoloni wa Uingereza kwa shabaha ya kuwazindua Waislamu wa India. Msomi huyo alifungwa gerezani mara kadhaa na wakoloni wa India, kutokana na hatua zake za kuchapisha na kutoa hotuba zenye kufichua ukandamizaji wa Uingereza. Mara baada ya India kuwa huru, alichaguliwa kuwa mbunge na Waziri wa Elimu na Malezi wa nchi hiyo.

Ayatullah Dakta Muhammad Husseini Beheshti