Mar 16, 2017 03:56 UTC
  • Alkhamisi 16 Machi, 2017

Leo ni Alkhamisi tarehe 17 Rabiuthani 1438 Hijria sawa na Machi 16, 2017.

Siku kama ya leo miaka 914 iliyopita yaani tarehe 17 Jamadithani mwaka 524 Hijiria, alifariki dunia Bari Baghdadi, fasihi na malenga mashuhuri wa Kiarabu. Baghdadi alizaliwa mwaka 443 Hijiria na kuanza kusomea elimu ya nahau na lugha kutoka kwa maulama wakubwa wa kipindi chake. Moja ya athari mashuhuri za Bari Baghdadi ni kitabu cha mashairi kilichopewa jina lake na ambacho alikiandika akiwa na umri wa miaka 81 hali akiwa ni kipofu.

Siku kama ya leo miaka 851 iliyopita kulitiwa saini makubaliano ya kisiasa ya Acre katika kipindi cha Vita vya Msalaba baina ya Waislamu na Wakikristo. Makubaliano hayo yalitiwa saini kwa ajili ya kukabidhiwa mji wa Acre kwa Wakristo na mkabala wake kuachiliwa huru mateka wa Kiislamu wapatao 3000. Hata hivyo na bila ya kuheshimu makubaliano hayo, Wakristo waliwaua mateka hao wa Kiislamu suala lililosababisha kuanza tena kwa Vita vya Msalaba ambavyo vilimalizika kwa kushindwa vibaya Wakristo. Mji wa Acre ulikombolewa na Waislamu katika karne ya 15 Hijiria na ukachukuliwa tena na Wamagharibi mwaka 587. 

Salahuddin Ayyubi, aliyeongoza mapambano ya Acre 

Siku kama ya leo miaka 118 iliyopita alifariki dunia msomi wa Kiislamu Hajj Mirza Hussain Nuri. Msomi huyu mkubwa alifikia daraja ya juu katika ibada, ucha-Mungu na ukamilifu wa nafsi. Hajj Mirza Hussein alikuwa hodari katika elimu za fiqhi, hadithi, tafsiri ya Qur'ani tukufu na mashairi na mwandishi aliyebobea wa vitabu. Vitabu vyake vingi vilihusu elimu za hadithi, tafsiri na ufafanuzi kuhusiana na maisha ya wasomi wa Kiislamu. Mirza Hussain Nuri alilipa umuhimu mkubwa suala la kueneza athari za Ahlul Bait wa Mtume (saw). Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi na miongoni mwa athari zake mashuhuri ni pamoja na kitabu cha "Mustadrakul Wasaail", "Maalimus Sabr", "Jannatul Maawa" na "Nafasur Rahman". Mirza Hussein Nuri amezikwa katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq. 

Hajj Mirza Hussain Nuri

Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, alifariki dunia Bi Selma Lagerlof mwandishi wa Sweden. Lagerlof alizaliwa mwaka 1858 na baada ya kumaliza masomo yake akaanza kujishughulisha na ukufunzi na uandishi wa hadithi na hekaya. Lagerlof alikuwa mwanamke wa kwanza kutunukiwa tuzo ya Nobel katika fani ya fasihi mwaka 1909.

Selma Lagerlof

Katika siku kama ya leo miaka 22 iliyopita, sawa na tarehe 26 mwezi Esfand mwaka 1373 Hijria Shamsiya aliaga dunia Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Ahmad Khomeini, mwana wa Imam Ruhullah Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Sayyid Ahmad Khomeini alizaliwa mwaka 1324 Hijria Shamsiya katika mji mtukufu wa Qum nchini Iran na kuanza kujifunza elimu ya kidini kwa baba yake. Sayyid Ahmad Khomeini alikuwa na nafasi muhimu katika kuwaunganisha wanamapinduzi na Imam Khomeini wakati wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Sayyid Ahmad Khomeini