Mar 22, 2017 02:19 UTC
  • Jumatano, tarehe 22 Machi, 2017

Leo ni Jumatano tarehe 23 Jamadithani 1438 Hijria sawa na Machi 22, 2017.

Leo ni Siku ya Maji Duniani. Ongezeko la jamii ya wanadamu, kuongezeka kwa matumizi ya maji, kukatwa ovyo miti ya misitu na mabadiliko ya hali ya hewa, kupanuka kwa miji na kuongezeka kwa viwanda vinavyochafua mazingira na vyanzo vya maji, mbinu zisizofaa za kilimo na kadhalika vimechangia uhaba wa maji, suala ambalo linatishia jamii ya mwanadamu. Kwa msingi huo na ili kuwazindua walimwengu kuhusu umuhimu wa maji, mkutano uliofanyika mwaka 1992 katika mji wa Rio de Janeiro nchini Brazil uliitangaza tarehe 22 Machi kuwa Siku ya Kimataifa ya Maji na suala hilo likapasishwa rasmi katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.  

Siku ya Maji Duniani

Siku kama ya leo miaka 13 iliyopita aliuawa shahidi Sheikh Ahmad Yassin mwanachuoni na mwasisi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas pamoja na watu wengine 10. Sheikh Ahmad Yassin aliuawa shahidi baada ya kumaliza swala ya Alfajiri katika msikiti mmoja ulioko eneo la Ukanda wa Gaza, wakati aliposhambuliwa na helikopta za utawala wa Kizayuni wa Israel. Sheikh Ahmad Yasin aliasisi harakati ya Hamas mwaka 1987 akishirikiana na wanamapambano wengine kadhaa wa Kipalestina na miaka miwili baadaye alifungwa jela na utawala ghasibu wa Israel. Mauaji ya mpigania uhuru huyo ambaye alikuwa kiwete na kipofu wakati wa kuuawa kwake, yalidhihirisha tena ugaidi wa kiserikali wa utawala haramu wa Israel.

Tarehe Pili Farvardin 1361 Hijria Shamsia, ambayo ni sawa na tarehe 22 Machi mwaka 1982 ilianza operesheni kubwa ya 'Fat-hul Mubiin' ya wapiganaji shujaa wa Kiislamu huko kusini magharibi mwa Iran kwa shabaha ya kuyarejesha nyuma majeshi vamizi ya Iraq. Kwenye operesheni hiyo iliyopelekea kukombolewa miji ya Dezful, Andimeshk, Shush na mamia ya vijiji vya eneo hilo, wanajeshi wasiopungua elfu 25 wa Iraq waliuawa na wengine elfu 15 kukamatwa mateka.

Sayyad Shirazi, kamanda wa operesheni ya Fat-hul Mubin akiwa pamoja na Muhsin Rezai

Na siku kama ya leo leo miaka 136 iliyopita lilianzishwa Shirikisho la Soka la Kimataifa kwa shabaha ya kusimamia mashindano ya mpira wa miguu kote duniani. Kabla ya kuundwa muungano huo, mashindano ya soka yalikuwa yakifanyika katika nchi mbalimbali kwa sura isiyokuwa rasmi. Muungano huo ulibadilisha muundo wake na kujulikana baadaye kwa jina la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na liliandaa pambano rasmi la kwanza la kimataifa mwaka 1901, kati ya Uingereza na Ujerumani.