Ijumaa, Machi 31, 2017
Leo ni Ijumaa tarehe Pili Rajab 1438 Hijria inayosadifiana na tarehe 31 Machi, 2017 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1217 iliyopita, alizaliwa Ibn Rumi, malenga mashuhuri wa Kiarabu mjini Baghdad, Iraq. Alianza kusoma elimu ya awali kwa baba yake akiwa kijana mdogo na baadaye akasoma kwa walimu wakubwa wa enzi zake. Aidha alipata kujifunza elimu za zama zake kama vile fasihi na mashairi. Ibn Rumi alikuwa akisoma sana mashairi ya kumsifu Imam Hassan Askari, mmoja wa Ahlu Bayti wa Mtume (saw) kutokana na mapenzi yake makubwa aliyokuwanayo kwa watu wa familia ya Mtume wa Allah (as). Malenga huyo alifariki dunia mwaka 283 Hijiria.

Siku kama ya leo miaka 998 iliyopita alifariki dunia Abu Raihan Biruni msomi, mnajimu na mwanahisabati mkubwa wa Kiirani huko katika mji wa Ghazne katikati mwa Afghnaistan ya sasa. Abu Raihan Biruni alikuwa hodari katika elimu za historia, jiografia na hisabati, tiba na utengenezaji wa dawa. Akiwa safarini nchini India, msomi huyo wa Kiirani alikutana na kufanya mijadala na maulama na watawala wa zama hizo. Abu Raihan alikusanya taarifa muhimu alizokuwa akizihitaji kwa ajili ya kuandika kitabu chake alichokiita 'Tahqiq Ma Lilhind' baada ya kujifunza lugha ya Sanskriti yaani lugha ya Kihindi ya kale.Katika kitabu hicho, Abu Raihan ameandika taarifa muhimu kuhusu sayansi, itikadi, mila na desturi za Wahindi. Msomi huyo wa Kiirani ameandika vitabu vingine vingi kuhusu elimu ya nujumu, mantiki na falsafa.

Miaka 421 iliyopita kama leo yaani tarehe 31 Machi mwaka 1596, alizaliwa Rene Descartes mwanafalsafa, mwanahisabati na mwanafizikia wa Kifaransa. Descartes alifikia daraja ya uhadhiri wa chuo kikuu baada ya kuhitimu masomo ya falsafa na hisabati. Aidha msomi huyo wa Kifaransa alifanya safari kwa kipindi fulani katika nchi mbalimbali na baadaye aliishi Uholanzi na kuanza kufanya utafiti. Rene Descartes aliitambua hisabati kuwa elimu kamili miongoni mwa elimu nyinginezo na kutaka kutumiwa elimu hiyo katika fani nyinginezo za kielimu. Miongoni mwa vitabu vya mwanafalsafa huyo ni Principles Of Philosophy, The Passions of the Soul na Discourse on the Method.

Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, garimoshi lililokuwa likitoka Cairo Misri likielekea katika bandari ya Haifa huko Palestina lililipuriwa kwa bomu, ikiwa ni katika kuongezeka mauaji ya umati dhidi ya Wapalestina yaliyokuwa yakifanywa na Wazayuni maghasibu. Wapalestina 40 waliuawa na wengine 60 kujeruhiwa katika jinai hiyo iliyofanywa na kundi moja la Kizayuni. Siku nne kabla ya mlipuko huo, garimoshi jingine lililipuliwa huko Palestina na Wazayuni wenye silaha, na kuuwa Wapalestina 24 na kujeruhiwa wengine 61.

Na siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zilisimamisha uanachama wa Misri katika jumuiya hiyo na nchi nyingi wanachama zikakata uhusiano wao na Cairo. Nchi za Kiarabu zilionesha radiamali hiyo kali kwa Misri baada ya rais wa zamani wa Misri Anwar Sadat kusaini hati ya mapatano ya Camp David na utawala wa Kizayuni wa Israel mwezi Januari mwaka 1978.
