Apr 22, 2017 03:46 UTC
  • Jumamosi, Aprili 22, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 24 ya mwezi Rajab 1438 Hijria sawa na tarehe 22 Aprili mwaka 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1431 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, ngome ya Khaibar ambayo ilikuwa moja ya ngome madhubuti na imara zaidi za Mayahudi ilitekwa na kudhibitiwa na Imam Ali (as), mkwewe Mtume Mtukufu (saw). Mayahudi ambao hawakuacha kueneza uadui wao wa jadi dhidi ya Uislamu walikuwa wakiendeshea njama zao huko Khaibar kaskazini mwa mji mtakatifu wa Madina, ambako walikuwa wamejenga ngome saba muhimu, ambazo waliamini kuwa hazingepenyeka wala kudhibitiwa na adui. Katika mwaka wa saba Hijiria Mtume (saw) alibashiri kutekwa kwa mji wa Khaibar. Muda si mrefu na baada ya kuvunja mzingiro uliokuwa umewekwa na maadui, jeshi la Kiislamu lilifanikiwa kudhibiti ngome kadhaa kati ya hizo saba isipokuwa mbili. Hatimaye Mtume aliwahutubu makamanda wa jeshi hilo kwa kusema: 'Kesho nitampa bendera mtu ambaye anampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake na anapendwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Mwenyezi Mungu ataiteka ngome hii kupitia mikono yake. Siku iliyofuata, Mtume alimpa Imam Ali (as) uongozi wa jeshi ambapo alipigana vita vya kishujaa na hivyo kuweza kudhibiti ngome ya mwisho ya Mayahudi huko Khaibar.

Ngome ya Khaibar

 Katika siku kama ya leo miaka 1099 iliyopita yaani tarehe 24 Rajab mwaka 339 Hijria,Abunassr Muhammad Farabi, Mwanafalsafa, mwanahesabati na msomi mashuhuri wa Kiirani aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 259 Hijiria katika mji wa Farab ilioko kusini mwa nchi ya Kazakhstan ya leo. Baada ya kupata masomo ya msingi katika mji huo, Farabi aliamua kwenda mjini Baghdad huko Iraq ili kuendeleza masomo yake na hasa ya mantiki na falsafa. Werevu mkubwa aliokuwanao ulimuwezesha kusoma masomo mengi ya zama zake lakini alizingatia zaidi somo la falsafa. Mwanafalsafa huyo mashuhuri aliyefahamika zaidi kwa majina ya Muallim ath-Thani, Ustadh wa Falsafa na Malik al-Hukamaa alifanya juhudi kubwa za kuunganisha fikra za wanafalsafa tofauti na hasa za Aristotle na Platon, akiamini kulikuwa na falsafa moja tu. 

Abunassr Muhammad Farabi

Miaka 122 iliyopita katika siku kama ya leo wananchi wa Cuba kwa mara nyingine tena walianzisha mapambano ya kupigania uhuru wao kutoka kwa wakoloni wa Uhispania. Hayo yalikuwa mapambano yao ya tatu katika nusu ya pili ya karne ya 19 Miladia kwa ajili ya kutaka kujitawala. Uhispania ilituma wanajeshi laki tatu nchini humo kwa ajili ya kupambana na wanamapinduzi hao. Kufuatia vurugu hizo Marekani ilitumia fursa hiyo na kwa kisingizio cha kulipuliwa meli yake ya kivita karibu na pwani ya Cuba mwaka 1898 Miladia, kuingia katika vita hivyo dhidi ya Uhispania. Manuari za kivita za Uhispania ziliangamizwa katika maji ya Cuba na hatimaye nchi hiyo ya Amerika ya Latini ikakaliwa kwa mabavu na Marekani.

Bendera ya Cuba

Siku kama ya leo miaka 113 iliyopita,  alizaliwa mwanafizikia na mtengenezaji wa bomu la atomiki wa Marekani Robert Oppenheimer. Kabla ya Vita vya Pili vya Dunia mtaalamu huyo alifanya utafiti kuhusiana na jinsi ya kupasua atomu na kupata nishati ya nyuklia. Wakati wa vita hivyo alipewa wadhifa wa kusimamia kitengo cha utafiti katika Wizara ya Vita ya Marekani na chini ya usimamizi wake yakatengenezwa mabomu matatu ya kwanza ya nyuklia. Hata hivyo, wakati Marekani ilipoishambulia Japan kwa mabomu ya nyuklia mwaka 1945, makumi ya maelfu ya watu wasio na hatia waliuawa katika kipindi kifupi, hali iliyomfanya Oppenheimer kujutia kitendo chake hicho na akatoa wito wa kutumiwa nishati ya atomiki katika masuala ya amani. 

Robert Oppenheimer

Katika siku kamaya leo miaka 69 iliyopita, yaani tarehe 22 Aprili 1948, Wazayuni waliushambulia mji wa bandari wa Haifa huko kaskazini magharibi mwa Palestina wakati wa kukaribia kuanzishwa utawala haramu wa Israel. Wazayuni waliwauwa shahidi Wapalestina 500 katika mashambulizi hayo makubwa na kuwajeruhi wengine 200 ambao walikuwa wanawake na watoto waliokimbilia huko Haifa wakisubiri kupelekwa katika maeneo mengine.