Apr 26, 2017 07:18 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (161)

Assalaama Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Hii ni sehemu ya 161 ya mfululizo wa vipindi hivi vya itikadi ya Kiislamu ambapo leo tutakamilisha swali lililoulizwa na msikilizaji wetu Bwana Faisal Badr wa Lamu Kenya ambaye alitaka kujua maana ya neno ‘imam’ katika aya ya  Quráni inayosema: ‘’Siku tutakapowaita kila kikundi cha watu kwa Imam wao.’’

Tuliona katika kipindi kilichopita na baada ya kuchunguza kwa kina maana ya aya hiyo kwamba maana ya neno ‘imam’ ni kila mtu ambaye watu wameamua kumfuata kama kiongozi katika maisha yao ya kila siku katika kila zama awe ni imam wa wongofu au wa upotovu. Tulipata pia kujua kwamba lengo hasa hapa ni kutuambua na kuwatenganisha wafuasi wa Maimamu walioteuliwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwaongoza wanadamu na wafuasia wa maimamu wa watu walioptea njia katika kila zama.

Tulikuahidini mwishoni mwa kipindi kilichopita kwamba katika kipindi cha leo tutakunukulieni baadhi ya hadithi ambazo zimepokelewa na madhehebu zote mbili za Kiislamui ambazo zinasisitiza maana hii tuliyoifafanua kutokana na aya tukufu tuliyoitaja, hivyo endeleeni kuwa nasi hadi mwisho wa kipindi, karibuni.

**********

Tunaanza kwa hadithi ambayo imenukuliwa na Jalal ad-Deen as-Suyuti ambaye ni mwanazuoni mkubwa wa Kisuni katika tafsiri yake ya ad-Durr al-Manthur kutoka kwa Mtume Mtukufu (saw) katika kufasiri aya iliyotajwa. Vilevile at-Tha’labi mwanazuoni mwingine wa Kisuni amenukuu hadithi hiyo inayosema: ‘Kila kaumu itaitwa kwa imamu wa zama zake, kitabu cha Mola wake na Suna za Nabii wake.’

Hadithi hii imepokelewa pia kwa njia ya madhehebu ya Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) yaani Shia, kupitia kitabu cha Uyun Akhbar ar-Ridha na vitabu vinginevyo. Ibn Jarir at-Tabari, mfasiri mkubwa wa Kisuni anasema katika tafsiri yake ya Jamiu al-Bayaan, baada ya kuchunguza na kufafanua kauli tofauti za wafasiri wa Quráni kuhusiana na aya hii: ‘Na kauli tunayoiona kuwa ni sahihi zaidi kwetu ni ya wale wanaosema kuwa maana ya, ‘’Siku tutakapowaita kila kikundi cha watu kwa Imam wao,’’ ni siku ambayo watu wataitwa kwa yule imamu waliyekuwa wakimfuata na kumsikiliza humu duniani. Hii ni kwa sababu Waarabu hutumia zaidi neno imamu kumaanisha yule mtu wanayemzingatia na kumfuata, na hivyo maana ya maneno ya Mweyezi Mungu huelekezwa zaidi kwenye maana iliyozoeleka na kutumika zaidi kwenye jamii, na suala hili linapasa kuheshimiwa isipokuwa katika hali ambayo tutakuwa na hoja inayoonyesha kinyume na hivyo.’

Na hivihivi ndivyo anavyosema ar-Raghib al-Isfahani katika kitabu chake cha Mu’jam Mufradaat al-Qurán na waandishi wengine wa masuala ya lafudhi za Quráni Tukufu.

 

Ama kuhusiana na madhehebu ya Ahlul Beit (as), Imam Baqir (as) amenukuliwa katika tafsiri za Ali bin Ibrahim na al-Ayashi na wengineo akisema katika kufasiri aya hii: ‘Mtume (saw) atakuja kwenye kaumu yake, Ali kwenye kaumu yake, al-Hassan kwenye kaumu yake, al-Hussein kwenye kaumu yake na kila aliyeaga katika kila zama atakuja akiwa ameandamana na imam.’

Ila katika hadithi za Ahlul Beit (as) kuna ishara ya kuvutia sana inayofafanua kwamba Mtume Mtukufu (saw) ndiye Bwana na Imam wa Maimamu wote wa wongofu. Imepokelewa katika tafsiri ya al-Burhan kwamba Imam Swadiq (as) alisema: ‘Je, hamumuhimidi Mwenyezi Mungu? Hakika Siku ya Kiama watakapoitwa kila kaumu kumwendea waliyekuwa wakimfuata, sisi - yaani Maimamu wote wa wongofu - tatakumkimbilia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), na nyinyi - yaani wafuasi wao – mtatukimbilia sisi.’

Imam Swadiq (as) pia amenukuliwa katika tafsi ya al-Ayashi akisema: ‘Ardhi haiachwi bila ya kuwa na Imam anayehalalisha halali ya Mwenyezi Mungu na kuharamisha haramu yake na hilo linatokana na kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema, ‘’Siku tutakapowaita kila kikundi cha watu kwa Imam wao.’’ Kisha akasema: Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: ‘Mtu anayekufa bila ya kuwa na Imam, huwa amekufa kifo cha ujahili.’ Na Imam (as) pia amesema kama ilivyonukuliwa katika tafsiri ya al-Ayashi: ‘Mwenyezi Mungu atakaposema Siku ya Kiama: ‘Je, si ni katika uadilifu wa Mola wenu kujaalia kila kaumu kiongozi waliyemfuata? Watasema ndio, ni sawa. Hapo Mwenyezi Mungu Mtukufu atasema: ‘Basi gawanyikeni, nao watagawanyika.’.…….yaani wafuasi wa Maimamu wa wongofu watagawanyika na kujitenga na wafuasi wa maimamu wa waliopotea.

 

Ndugu wasikilizaji, na maneno ya Mtume Mtukufu (saw) yanayobainisha kwa uwazi mkubwa zaidi maana ya neno ‘imam’ katika aya tunayoijadili hapa na ambayo inasema wazi kuwa Uimamu wa Mtume hauishii tu kwenye Uimamu wa Bwana huyo wa Mitume (saw) ni yale maneno aliyoyatamka kwa uwazi mkubwa mtukufu huyo as-Swadiq al-Amin (saw) kupitia mjukuu wake Imam Swadiq (as) kama anavyonukuliwa katika kitabu cha al-Mahasin aliposema: ‘Wakati aya ’Siku tutakapowaita kila kikundi cha watu kwa Imam wao,’ ilipoteremshwa, Waislamu walisema: ‘Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, si ni wewe ndiwe Imam wa watu wote? Mtume (saw) akajibu: Mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa watu wote lakini baada yangu kutakuwepo na Maimamu kwa ajili ya watu kutoka kwa Watu wa Nyumba yangu, kutoka kwa Mungu - yaani walioteuliwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwa Maimamu – ambao watasimama miongoni mwa watu na kukadhibishwa na vilevile kudhulumiwa na maimamu wa kufri na upotovu pamoja na wafuasi wao.’

Kisha Mtume alisema: ‘Hivyo mtu atakayewafanya kuwa viongozi wake na kuwafuata pamoja na kuwasadikisha basi huyo atakuwa anatokana nami, kuwa pamoja nami na atakutana na mimi. Na yule anayewadhulumu na kusaidia katika kudhulumiwa kwao na kuwakadhibisha basi huyo si katika mimi wala hayuko pamoja nami, nami ninajitenga naye.’

Katika hadithi hii tukufu kuna ishara ya kuvutia kwamba wale wote waliohusishwa na ibara ya ‘Imam wao’ katika Maimamu wa wongofu wanarejea kwa Mtume Mtukufu (saw) ambapo yeye Mtume ni Imam wa Maimamu hao wa wongofu (as).

 

Na hadi hapa ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho kimekujieni moja kwa moja kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena katika kipindi kingine juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote wapenzi wasikilizaji kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

 

 

Tags