Jumatano tarehe 28 Juni, 2017
Leo ni Jumatano tarehe 28 Juni 2017.
Miaka 144 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa, Dakta Alexis Carrel, mwanabiolojia na mwanafalsafa wa Kifaransa. Msomi huyo alizaliwa katika mji wa Lyon nchini Ufaransa. Mwaka 1912 Dakta Carrel alitunukiwa tuzo ya heshima ya Nobel kutokana na mchango wake mkubwa katika uwanja wa tiba. Alitumia kipindi fulani katika maisha yake kutalii na kuzitembelea nchi mbalimbali zikiwemo za Kiislamu na kushuhudia kwa karibu mila na tamaduni za nchi hizo. Kwa sababu hiyo Dakta Alexis Carrel amesisitiza mno katika maandishi na vitabu vyake juu ya umuhimu na nafasi ya dini na masuala ya kiroho katika maisha ya mwanadamu. Nadharia nyingi za msomi huyo zimo katika kitabu mashuhuri alichokipa jina la "Mwanadamu, Kiumbe Asiyefahamika" ambamo ndani yake anapinga demokrasia ya kimagharibi.
Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 28 Juni 1914 aliuawa Franz Ferdinand, mrithi wa kiti cha ufalme wa Austria akiwa pamoja na mkewe, wakati alipokuwa safarini Sarayevo, mji mkuu wa Bosnia Herzegovina ya leo, baada ya kufyatuliwa risasi na mwanachuo mmoja wa Kiserbia. Mara baada ya kutokea shambulio hilo, serikali ya Austria ilitaka ipewe nafasi ya kuingilia kati uchunguzi wa faili la kesi hiyo, jambo lililopingwa na serikali ya Serbia. Amma baada ya kupita mwezi mmoja tu, Austria ilianza kuishambulia Serbia kwa kisingizio hichohicho, na kuanzia mwezi Agosti mwaka huohuo, vikaanza rasmi Vita vya Kwanza vya Dunia baada ya Ujerumani kuamua kuiunga mkono Austria na kuishambulia ardhi ya Ubelgiji.
Miaka 36 iliyopita mwafaka na tarehe 7 mwezi Tir mwaka 1360 Hijria Shamsiya, Ayatullah Dakta Muhammad Beheshti aliuawa shahidi akiwa pamoja na watu wengine 72 wakiwemo mawaziri na wabunge kadhaa, baada ya kuripuliwa kwa bomu ofisi kuu ya chama cha Jamhuri ya Kiislamu. Ayatullah Beheshti pia alikuwa miongoni mwa shakhsiya wa awali na waliotoa mchango mkubwa katika Mapinduzi ya Kiislamu. Dakta Beheshti pia alikuwa mmoja kati ya wasaidizi wakuu wa Imam Khomeini (MA).
Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, mji wa Sardasht huko magharibi mwa Iran ulishambuliwa kwa mabomu ya kemikali na ndege za kivita za utawala wa zamani wa Iraq. Wakazi wa mji huo wapatao 110 waliuawa shahidi na wengine 530 kujeruhiwa kwenye mashambulio hayo. Utawala wa zamani wa Iraq ambao ulikuwa umepoteza matumini ya kushinda vita ulivyovianzisha dhidi ya Iran, ulidhani kwamba kwa kuendesha mashambulio ya silaha za kemikali ungeweza kuitwisha Iran matakwa yake kupitia mashambulio hayo ya kinyama, lakini haukufanikiwa kufikia lengo hilo.
Na siku kama ya leo miaka 11 iliyopita sawa na tarehe 28 Juni mwaka 2006 jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha mashambulio makubwa dhidi ya watu wa Ukanda wa Ghaza. Utawala wa Kizayuni uliendesha mashambulio hayo ya kinyama kwa kisingizio cha kuuawa wanajeshi wake wawili siku tatu kabla ya mashambulio hayo. Israel ilidai kuwa wanamapambano wa Palestina walifanya oparesheni katika kituo kimoja cha upekuzi na kuua wanajeshi wake wawili na kumkamata mateka mwingine mmoja. Idadi kadhaa ya mawaziri, wabunge na wawakilishi wa baraza la mji la serikali halali ya Palestina iliyoongozwa na Hamas walitekwa nyara na wanajeshi wa Israel katika siku za kwanza za mashambulizi hayo makubwa ya jeshi yaliyopewa jina la "Mvua za Kiangazi".