Jul 13, 2017 02:38 UTC
  • Alkhamisi Julai 13, 2017

Alkhamisi tarehe 18 Shawwal 1438 Hijria, sawa na Julai 13, 2017.

Siku kama ya leo miaka 1953 iliyopita inayosadifiana na tarehe 13 Julai mwaka 64, kulitokea ajali kubwa ya moto katika mji wa Roma, makao ya Mfalme wa Rumi. Sehemu kubwa ya nyumba za mji huo ziliteketea moto kwa muda mfupi tu tangu kuzuka kwa moto huo, na hasa ikizingatiwa kuwa nyumba nyingi za mji huo wakati ule zilikuwa zimejengwa kwa mbao. Tukio hilo lilitumiwa na mtawala katili wa wakati huo wa mji huo aliyejulikana kwa jina la Nero kuwatuhumu Wakristo kuwa walihusika na njama hiyo. Baada ya hapo mtawala huyo katili aliwauwa kwa halaiki zaidi ya Wakristo laki moja.

Moto mkubwa ulioteketeza mji wa Roma

Miaka miaka 840 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe 18 Shawwal mwaka 598 Hijria, alifariki dunia Muhammad bin Idris Hilli, fakihi na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 543 Hijiria katika katika mji wa Hilla nchini Iraq. Ibn Idris alijifunza Qur'ani na elimu ya dini tangu akiwa mtoto na baadaye akaondokea kuwa alimu mkubwa. Miongoni mwa athari zenye thamani kubwa za alimu huyo ni kitabu kinachoitwa Sarair ambacho ni muhimu na chenye itibari kubwa katika Uislamu.

Siku kama ya leo miaka 617 iliyopita liliundwa jeshi la kale zaidi duniani nchini Uswisi. Jeshi hilo la kale zaidi duniani hadi hii leo lemebakia kama lilivyokuwa na hata mavazi ya wanajeshi wake hayajabadilika. Idadi ya wanajeshi wa jeshi hilo dogo lakini lenye nidhamu kubwa ni watu 83. Jeshi hilo ambalo wanachama wake daima huwa raia wa Uswisi, liliundwa kwa ajili ya kulinda viongozi wa Kikatoliki wa wakati huo na hii leo baada ya kupita zaidi ya miaka zaidi ya 600 tangu liundwe, jeshi hilo lina jukumu la kumlinda Papa wa Kanisa Katoliki huko Vatican.

Jeshi la Uswisi

Siku kama ya leo miaka 246 iliyopita, baharia na nahodha mashuhuri wa Kiingereza aliyejulikana kwa jina la James Cook alikamilisha safari yake ya kitafiti na kielimu ya kuelekea The Great Southern Continent. Safari hiyo ilikuwa imeanza tarehe 26 Julai mwaka 1768. Safari hiyo ndefu iliishirikisha pia timu ya watalaamu wa elimu ya Sayansi Asilia au Natural Science kwa kimombo. Wataalamu hao walikuwa na nia ya kufanya utafiti wa kielimu kuhusiana na mimea pamoja na viumbe wanaopatikana katika maeneo hayo.

James Cook

Tarehe 18 Shawwal miaka 184 iliyopita alizaliwa Mirza Hussein Nuri, alimu na faqihi mashuhuri wa Kiislamu katika mji wa Nur kaskazini mwa Iran. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali, Mirza Hussein Nuri alielekeza juhudi na jitihada zake katika masuala ya kujifunza na kukusanya hadithi. Msomi huyo wa Kiislamu alitokea kuwa mmoja wa wasomi wakubwa wa masuala ya hadithi na baadaye akaanza kuandika vitabu vya thamani katika uwanja huo. Miongoni mwa vitabu hivyo ni "Akhbaru Hifdhil Qur'an", "Tawi la Mti wa Tuba" na "Historia ya Viongozi Adhimu wa Uislamu".

Mirza Hussein Nuri