Jumamosi, 14 Oktoba, 2017
Leo ni Jumamosi tarehe 23 Mfunguo Nne Muharram 1439 Hijria mwafaka na tarehe 14 Oktoba 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 142 iliyopita, Allama Mullah Muhammad Mahdi Naraqi, alimu na msomi mkubwa wa Kiislamu aliaga dunia. Alimu huyo baada ya kumaliza masomo ya awali nchini Iran Mahdi Naraqi alielekea Najaf nchini Iraq kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Mullah Mahdi Naraqi alisoma kwa bidii na kuwa mahiri katika taaluma mbalimbali. Baadaye Allama Naraqi alijishuhugulisha na kazio ya uhakiki, kufundisha na uandishi wa vitabu. Jamius Saadat ni moja ya vitabu mashuhuri vya mwanazuoni. ***
Katika siku kama ya leo miaka 203 iliyopita, mkutano wa kihistoria wa Vienna ulifanyika kwa lengo la kujadili “Ulaya baada ya Napoleon Bonaparte”. Baada ya kujiuzulu na kubaidishwa Bonaparte mwezi Aprili mwaka 1814, mkutano wa kihistoria wa Vienna ulianza kufanyika katika siku kama ya leo katika mji mkuu wa Austria Vienna ili kuchukua maamuzi kuhusu ardhi zilizokaliwa kwa mabavu na Ufaransa katika kipindi cha vita vya Bonaparte. Wakati wa kuendelea kufanyika mkutano huo, Napoleone Bonaparte alikimbia kutoka mahala alipokuwa amebaidishiwa na mwishoni mwa mwezi Februari mwaka 1815 kwa mara nyingine tena akashika hatamu za uongozi kwa muda mfupi, kipindi ambacho kiliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la “Utawala wa Siku 100”. Aliposhika tena hatamu za uongozi alijianda kuwashambulia maadui zake. ***
Miaka 84 iliyopita katika siku kama ya leo, kwa amri ya Adolf Hitler Kansela wa wakati huo wa Ujerumani, nchi hiyo ilijitoa katika Jumuiya ya Kimataifa. Kuingia madarakani Adolf Hitler akiwa Kansela wa Ujerumani kulikuwa kumepelekea kuzuka wasiwasi mkubwa katika kila kona ya Ulaya kutokana na mipango yake ya kijeshi. Baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia na kutiwa saini mkataba wa amani wa Warsaw ambao ulidhibiti sana zana za kijeshi za Ujerumani, Hitler na viongozi wengine wa Kinazi walikasirishwa mno na hatua hiyo.***
Katika siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, Wazayuni wa Israel walivamia kijiji cha Qibya kilichoko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kufanya jinai kubwa za kutisha. Katika mashambulizi na uvamizi ulioendelea katika kijiji hicho kwa muda wa siku mbili, Wazayuni walitekeleza mauaji na ukatili mkubwa dhidi ya raia wa Kipalestina wasio na hatia. Mbali na Wazayuni hao kuwaua na kuwajeruhi kwa umati raia wa Kipalestina zaidi ya 42, askari wa Israel waliokuwa wakiongozwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, Ariel Sharon, walibomoa makumi ya nyumba na shule za kijiji hicho. Mauaji hayo ya halaiki ni miongoni mwa mifano ya ugaidi wa utawala ghasibu wa Israel hususan Waziri Mkuu wa zamani wa utawala huo, Ariel Sharon. ***
Na siku kama ya leo miaka 18 iliyopita alifariki dunia kiongozi wa zamani wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anayejuliakana pia kama Baba wa Taifa. Nyerere alizaliwa mjini Butiama mkoani Mara mwaka 1922. Mwaka 1955 aliingia katika ulingo wa siasa akiongoza chama cha Tanganyika Africa Nation Union (TANU). Mwaka 1961 Nyerere alikuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika na mwaka mmoja baadaye akawa Rais wa nchi hiyo. Kutokana na juhudi zake mwaka 1964 Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuunda nchi moja ya Tanzania. Nyerere aliendelea kuongoza nchi hiyo hadi mwaka 1985 ambapo aliachia hatamu za uongozi. Hata hivyo Nyerere aliendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Tanzania hadi alipofariki dunia. Nyerere analaumiwa kwa siasa yake ya kiujamaa kuwa ilichelewesha maendeleo ya kiuchumi wa Tanzania. Pia kuna makundi ya Waislamu Tanzania yanayomtuhumu kwamba, aliendesha kwa siri vita dhidi ya dini yao na kupendelea Wakristo katika utoaji wa elimu na madaraka. Aidha baadhi ya Wazanzibar wanamtuhumu Nyerere kwamba alimhadaa aliyekuwa Rais wa Zanzibar Mzee Abeid Amaan Karume kwa kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar na kuanza kupora kidogo kidogo mamlaka ya Zanzibar..***