Ijumaa tarehe Mosi Disemba, 2017
Leo ni Ijumaa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1439 Hijria sawa na Disemba Mosi, 2017.
Siku kama ya leo miaka 1492 inayosadifiana na tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal miaka 53 kabla ya Hijria, kwa kauli ya baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu akiwemo Masoudi, alizaliwa Mtume Muhammad SAW. Wanachuoni wengine wa Kiislamu wanaamini kwamba, Mtume Muhammad (saw) alizaliwa tarehe 17 Rabiul Awwal mwaka huohuo. Kwa msingi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza kipindi cha kuanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal kila mwaka kuwa ni Wiki ya Umoja kati ya Waislamu kote duniani. Wiki ya umoja ni fursa nzuri ya kuzikurubisha nyoyo za Waislamu na kuimarisha umoja na mshikamano wao katika kukabiliana na maadui wa ulimwengu wa Kiislamu.

Tarehe 12 Rabiul Awwal mwaka wa kwanza Hijria, Mtume Muhammad (saw) aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa msikiti wa kwanza kabisa katika Uislamu katika kijiji cha Quba kilichoko pambizoni mwa Madina. Mtume (saw) aliweka jiwe la msingi la msikiti huo wa kihistoria wakati aliposimama kwa siku chache katika eneo la Quba akiwa njiani kutoka Makka na kuelekea Madina. Mtukufu huyo alisimama kwa muda katika kijiji cha Quba akimsubiri Ali bin Abi Twalib na jamaa wa familia ya Mtume.

Siku kama ya leo miaka 1198 iliyopita, inayosadifiana na 12 Rabiul Awwal 241 Hijria, alifariki dunia Imam Ahmad bin Hanbal mmoja kati ya maulamaa wakubwa wa Kiislamu katika mji wa Baghdad, Iraq ya leo. Ahmad bin Hanbal alizaliwa mwaka 124 Hijria, katika mji wa Baghdad na kujipatia elimu ya kidini katika mji huo kutoka kwa maulamaa wakubwa akiwemo Imam Shafii. Imam Hanbal amesafiri katika miji kadhaa kama vile Kufa, Basra, Makka, Madina, Sham na Yemen kwa minajili ya kukusanya hadithi za Bwana Mtume SAW. Ahmad bin Hanbal ni muasisi wa Madhehebu ya Kisuni ya Hanbal na ameacha kitabu mashuhuri cha hadithi, kiitwacho Musnad.

Miaka 192 sawa na leo, muungano wa kihistoria wa nchi za Ulaya uliojulikana kama Muungano Mtakatifu ulisambaratika baada ya kujiengua utawala wa Kikaitsar (Tsarist) wa Russia katika muungano huo. Baada ya kuanguka kwa utawala wa Napoleon, muungano huo ukaunda Congress ya Vienna, kati ya tawala za Russia, Austria na ufalme wa Pros na serikali hizo zikaafikiana kwamba nchi zilizo chini ya utawala wa muungano huo na katika uhusiano wa kimataifa zifuate misingi ya dini ya Kikristo.

Na katika siku kama ya leo tarehe Mosi mwezi Disemba kila mwaka, nchi mbalimbali duniani huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Ukimwi. Kuweko Siku ya kimataifa ya Ukimwi kulifikiriwa kwa mara ya kwanza mwezi Agosti mwaka 1987 na James W.Bunn na Thomas Netter, maafisa wawili wa habari wa Kitengo cha Kimataifa cha Kupambana na Ukimwi cha Shirika la Afya Duniani (WHO) huko Geneva Uswisi. Maafisa hao wawili waliwasilisha wazo hilo kwa Dakta Jonathan Mann, Mkurugenzi wa Shirika la UNAIDS na baadaye akakubali pendekezo hilo, na kuliidhinisha. Na hatimaye akaafiki siku ya kwanza ya kimataifa ya Ukimwi iadhimishwe duniani kote tarehe Mosi Disemba mwaka 1988. Kuanzia wakati huo kila mwaka siku ya kimataifa ya Ukimwi huadhimishwa duniani kote kila ifikapo tarehe Mosi Disemba.
