Jumatatu 11 Disemba, 2017
Leo ni Jumatatu tarehe 22 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1439 Hijria mwafaka na tarehe 11 Disemba mwaka 2017.
Siku kama ya leo miaka 1435 iliyopita, yaani tarehe 22 Rabiul-Awwal mwaka wa 4 Hijiria, kulianza vita kati ya Waislamu na Mayahudi wa kabila la Bani Nadhir baada ya watu wa kabila hilo kufanya njama za kutaka kumuua Mtume Muhammad (SAW). Bani Nadhir ni moja ya makundi matatu ya Mayahudi waliokuwa wakiishi katika vitongoji vya mji wa Madina, ambao kwa mujibu wa mkataba waliotiliana saini na Mtume (SAW), hawakupaswa kuchukua hatua yoyote iliyo dhidi ya mtukufu huyo na Waislamu kwa ujumla. Baada ya Mayahudi kuvunja mkataba huo, Mtume Muhammad (SAW) aliwaamuru waondoke Madina. Hata hivyo Mayahudi hao ambao tayari walikuwa wamepewa ahadi za kuungwa mkono na wanafiki wa mji huo, hawakuwa tayari kutii amri hiyo. Ni kwa sababu hiyo, ndipo mtukufu Mtume kwa kushirikiana na Waislamu akazizingira ngome za watu hao kwa muda wa siku kadhaa na kuwalazimisha kuondoka katika maeneo yao.

Tarehe 11 Disemba miaka 174 iliyopita alizaliwa daktari na mtaalamu wa vividudu maradhi wa Kijerumani aliyevumbua ugonjwa wa kifua kikuu, Robert Koch. Baada ya kukamilisha masomo katika taaluma ya tiba, Robert Koch alijishughulisha na kutiwa wagonjwa katika miji mbalimbali ya Ujerumani sambamba na kufanya uhakiki kuhusu maradhi tofauti. Tarehe 24 Machi mwaka 1882 alifanikiwa kuvumbua ugonjwa wa kifua kikuu (TB). Katika safari zake nyingi barani Afrika, tabibu huyo wa Kijerumani pia alibaini kuwa ugonjwa wa malale uliokuwa ukisababisha vifo vya Waafrika wengi ulikuwa ukisababishwa na mdudu anayeitwa mbung'o.

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) uliasisiwa baada ya kupasishwa suala hilo kwa wingi wa kura. Kwa utaratibu huo, taasisi hiyo ikaanza rasmi shughuli zake chini ya Baraza la Masuala ya Kijamii la Umoja wa Mataifa. Awali Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF), ulikuwa na jukumu la kuwahudumia watoto waliojeruhiwa katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Hata hivyo baadaye asasi hiyo muhimu ikapanua zaidi shughuli zake na kuanza kuandaa mahitaji ya kimsingi maishani kama chakula, elimu na malezi kwa watoto waliokosa haki hizo za kimsingi. Makao makuu ya UNICEF yapo mjini New York, Marekani.

Na miaka 36 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, aliuawa shahidi Ayatullah Sayyid Abdulhussein Dastgheib, alimu mkubwa na mwalimu wa akhlaq wa Kiislamu. Ayatullah Dastgheib aliuawa shahidi na kundi la munafiqin alipokuwa akielekea kwenye Swala ya Ijumaa. Alizaliwa katika mji wa Shiraz kusini mwa Iran na alipata elimu yake ya kidini hadi daraja ya ijtihadi katika chuo cha Najaf nchini Iraq. Ayatullah Dastgheib pia alishirikiana na maulamaa wengine waliokuwa na mwamko na wanaharakati wa Iran katika kufundisha elimu ya Kiislamu, kupambana na utawala wa Shah na mara kadhaa alikamatwa na kufungwa jela. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni "Madhambi Makubwa", "Maad" pamoja na tafsiri ya sura kadhaa za Qur'ani Tukufu.'
