Apr 17, 2018 09:50 UTC
  • Aya na Hadithi (19)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni matumaini yetu kwamba muko tayari kabisa kusikiliza kipindi hiki mnachokipenda cha Aya na Hadithi ambacho hutufundisha mengi katika maarifa ya Kiislamu, na hasa katika kutushajiisha kufuatilia mambo yanayotuwezesha kupata radhi za Mwenyezi Mungu na kutuepusha na yale yanayomghadhabisha.

Hii ni sehemu ya 19 ya mfululuzo wa vipindi hivi ambapo kwa leo tunaanza kwa kusikiliza kwa makini Aya za 204 hadi 207 za Surat al-Baqarah ambapo Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

Na katika watu yupo yule ambaye maneno yake kwa maisha ya kidunia hukufurahisha; naye humshuhudisha Mwenyezi Mungu kwa yaliyomo moyoni mwake, na hali ni hasimu mkubwa kabisa. Na anapotawala hufanya bidii katika nchi kwa kufisidi humo na kuteketeza mimea na viumbe. Na Mwenyezi Mungu hapendi ufisadi. Na akiambiwa: Mwogope Mwenyezi Mungu, hupandwa na mori wa kutenda madhambi. Basi huyo inamtosha Jahannam. Paovu mno hapo kwa mapumziko. Na katika watu yupo ambaye huiuza nafsi yake kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake.

 

Kwa hivyo wapenzi wasikilizaji, Aya tatu za kwanza zinatahadharisha dhidi ya watu wanaotoa nara na maneno matamu ya kuvutia lakini ambayo hayaambatani hata kidogo na vitendo vyao, bali kinyume chake huwa yanabainisha ifisadi wao na kuwa kwao mbali na uchaji Mungu. Kisha Aya ya nne inakuja na kuzishajiisha nyoyo zizingatie na kuwafuata watu wema na wakweli ambao hufanya bidii kutii amri za Mwenyezi Mungu na kupata ridhaa yake. Katika kufafanua sababu ya kuteremshwa Aya hii, Ath-Tha'labi anasema hivi katika Tafsiri yake ya Qur'ani: 'Mtume (saw) alipoazimia kuhajiri (kwenda Madina), alimwacha nyuma Ali (as) ili apate kulipa madeni yake na kuwarejeshea wamiliki amana zao walizokuwa wameziacha kwa Mtume (saw). Usiku aliohijiri kuelekea kwenye pango, alimuamuru Ali (as) alale kitandani pake, hali ya kuwa nyumba yake ilikuwa imezingirwa na washirikina, naye Ali akawa amefanya kama alivyoamrishwa. Kufuatia hali hiyo Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwaambia Malaika Jibril na Mikail kupitia Wahyi kwa kusema: Mimi nimekufanyeni nyinyi wawili kuwa ndugu na kuufanya umri wa mmoja wenu kuwa mrefu zaidi kuliko wa mwenzake. Je, ni nani kati yenu atakayejitolea muhanga maisha yake kwa ajili ya mwenzake? Wawili hao hawakuwa tayari kujitolea katika hilo na wote wakachagua kulinda maisha yao. Hapo Mwenyezi Mungu akawaambia: Hamukuwa kama Ali bin Abi Talib ambaye baada ya mimi kumfanya kuwa ndugu na Muhammad, aliamua kulala kitandani kwake kama fidia na kuyatoa muhanga maisha yake (kwa ajili ya Muhammad). Teremkeni kwenye ardhi na mumlinde dhidi ya maadui wake. Waliteremka ardhini ambapo Malaika Jibril alisimama kichwani pa Ali naye Malaika Mikail akawa amesimama upande wa miguu yake. Malaika Jibril akawa anasema: Hongera! Hongera! Ni nani aliye mithili yako ewe Ali bin Abi Talib! Mwenyezi Mungu anajifaharisha nawe mbele ya Malaika wake. Hapo Mwenyezi Mungu akamtaremshia Mtume (saw) akiwa njiani kuelekea Madina, Aya ufuatayo katika kumsifu Ali bin Abi Talib (as): Na katika watu yupo ambaye huiuza nafsi yake kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu.

 

Naye al-Hafidh al-Khowarazmi ambaye pia ni katika wanazuoni wa Kisuni anasema katika kitabu chake cha Manaqib akimnunukuu Mtume (saw) akisema: 'Jibril (as) aliteremka kwangu asubuhi ya siku ya pango nami nikamuuliza: Mpendwa wangu Jibril! Kuna nini, nakuona ukiwa ni mwenye furaha na bashasha. Akasema: Ewe Muhammad! Nitakosaje kuwa hivyo ilihali nimefurahishwa na kile Mwenyezi Mungu amemkirimu nacho ndugu na wasii wako na vilevile Imamu wa Umma wako, Ali bin Abi Talib? Akauliza: Na ni nini hicho ambacho Mwenyezi Mungu amemkirimu nacho? Akasema: Jana Mwenyezi Mungu alijifaharisha (alijivunia) ibada yake mbele ya Malaika na wabeba Arshi yake kwa kusema: Malaika wangu! Mtazameni Hujja wangu katika ardhi yangu kwa waja wangu, baada ya Nabii wangu. Ametoa mhanga nafsi yake na kuweka shavu lake mchangani kwa kunyenyekea adhama (utukufu) yangu. Ninakushuhudisheni kwamba yeye ni Imamu na maula wa viumbe wangu.'

************

Wapendwa wasikilizaji, na katika Hadithi ambayo imenukuliwa katika Tafsiri ya Kanz ad-Daqaiq, Imam Hassan al-Askari (as) anatuelekeza katika njia ambayo itatuwezesha kumfuata Imam Ali al-Murtadha (as) katika ukweli wake, kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu. Imam (as) anatufafanulia maana ya Aya hii tukufu kwa kusema: 'Na katika watu yupo ambaye huiuza nafsi yake, yaani anaiuza na kuwaamrisha watu kwayo, anasubiri mbele ya udhia anaoupata kwayo na hivyo kuwa kama mtu aliyeiuza nafsi yake na kuisalimisha kwa ajili ya kupata ridha za Mwenyezi Mungu. Hivyo huwa hajali ni jambo gani limeipata nafsi hiyo baada ya kupata ridha za Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake (wote). Wale wanaotafuta ridhaa za Mwenyezi Mungu, huwafikisha kwenye upeo wa matamanio yao na hata kuwazidishia yale waliyokuwa hawayatazamii.'

************

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Aya na Hadithi ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni matumaini yetu kuwa mmeweza kunufaika na yale tuliyokuandalieni kwenye kipindi cha leo. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags