Apr 24, 2018 03:13 UTC
  • Jumanne,  Aprili 24, 2018

Leo ni Jumanne tarehe 7 Shaaban mwaka 1439 Hijria inayosadifiana na tarehe 24 April, mwaka 2018.

Siku kama ya leo miaka 1466 iliyopita kwa mujibu wa mahesabu ya wanahistoria wengi, iliasisiwa kwa mara ya kwanza taasisi ya kuandika na kutarjumu vitabu duniani hapa nchini Iran. Uamuzi huo ulichukuliwa na Khosrow Anushirawan, mfalme wa Sasani nchini hapa. Taasisi hiyo iliyoenda sambamba na maktaba ya kijamii kwa pamoja vilikamilishwa kujengwa mwaka huo huo sawa na tarehe 24 April mwaka 552 Miladia. Vitabu tofauti vililetwa kutoka maeneo mbalimbali ya dunia kwa ajili ya kutarjumiwa huku mfalme huyo akimtuma pia daktari wake kwenda nchini India kwa ajili ya kuleta vitabu kwa ajili ya shughuli hiyo.

Maktaba

Siku kama ya leo miaka 747 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 24 April mwaka 1271, mtalii Marco Polo wa Venice alianza safari ya kihistoria ya kutembelea bara la Asia. Kabla yake baba na ami yake walitembelea China kupitia njia ya Asia Ndogo na Iran. Baada ya kurejea ndugu wa Polo kutoka Ulaya, Marco Polo akifuatana na baba yake kwa mara nyingine walielekea China na kutembelea ardhi ya nchi hiyo na visiwa vya kusini mshariki mwa Asia. Baada ya kurejea nchini kwake, Marco Polo aliandika kumbukumbu ya safari iliyoitwa "Maajabu" kuhusiana na hali ya kijiografia ya ardhi za China, Turkemanistan, Mongolia na sehemu za kusini mashariki mwa Asia. Safari ya Marco Polo barani Asia ilichukua karibu miaka 20.

Marco Polo

Siku kama ya leo miaka 91 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 24 April mwaka 1927 chanjo ya B.C.G iligunduliwa. Chanjo hiyo iligunduliwa na madakatari wa kifaransa Albert Calmette na Guerin, baada ya kufanya uchunguzi wa miaka mingi. Chanjo ya B.C.G hutumika kukinga maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu au TB. Kugunduliwa chanjo hiyo kumepunguza vifo vya watu wanaopatwa na ugonjwa wa TB duniani kote.

Chanjo ya B.C.G

Na siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, sawa na tarehe 24 Aprili mwaka 1916 kulianza harakati ya tatu ya raia wa Ireland kwa ajili ya kujipatia uhuru wao kutoka kwa serikali ya Uingereza. Harakati hiyo ilienda sambamba na kujiri kwa vita vikali vya kidini baina ya Waprotestanti na Wakatoliki. Vita hivyo vilimalizika kwa kufikiwa makubaliano baina ya David Lloyd George, Waziri Mkuu wa wakati huo wa Uingereza na kiongozi wa harakati ya raia wa Ireland waliokuwa wanataka kujitenga hapo mwaka 1922 Miladia.

Bendera ya Ireland

 

Tags