Alkhamisi, Julai 7, 2018
Leo ni Alkhamisi tarehe 22 Ramadhani 1439 Hijria, sawa na tarehe 7 Juni 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1166 iliyopita, alifariki dunia Ibn Majah, mpokezi wa hadithi na mfasiri mashuhuri wa Qur’ani wa Kiislamu. Ibn Majah alizaliwa mwaka 209 Hijria katika mji wa Qazvin nchini Iran. Alielekea katika nchi mbalimbali za Kiislamu ili kujifunza elimu ya hadithi. Aliandika kitabu chake mashuhuri kwa jina la "Sunan Ibn Majah" baada ya kuhitimu masomo katika elimu ya hadithi, kitabu ambacho ni moja kati ya vitabu sita vya hadithi vyenye itibari vya Waislamu wa madhehebu ya Suni.
Siku kama hii ya leo miaka 170 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Juni 1848 alizaliwa Paul Gauguin mchoraji mashuhuri wa Kifaransa. Gauguin alizaliwa Ufaransa na kisha kumuoa mwalimu aliyekuwa mahiri katika fani ya uchoraji, na kusababisha Gauguin kuvutiwa na sanaa hiyo iliyomuwezesha kuacha athari zake za sanaa ya uchoraji katika kisiwa cha Tahiti, kilichoko kusini mwa bahari ya Pasifiki. Gauguin aliishi kwenye kisiwa hicho hadi mwisho wa umri wake mwaka 1903, kwa kuchora picha zinazoakisi mandhari mbalimbali.
Siku kama ya leo miaka 175 iliyopita, alifariki dunia Johann Friedrich Hölderlin, malenga mkubwa wa nchini Ujerumani. Alizaliwa tarehe 20 Machi 1770 Miladia katika familia masikini ambapo akiwa kijana mdogo alifiwa na baba yake mzazi. Friedrich Hölderlin pia alijifunza elimu ya dini katika chuo kikuu ambapo alitokea kuwa na hisia za utumishi na urafiki sambamba na kusoma mashairi ya kidini. Malengo ya kupigania uhuru ya Ufaransa ni mambo yaliyotawala fikra za Johann Friedrich Hölderlin. Hata hivyo licha ya kwamba alikuwa na harakati mbalimbali lakini athari zake muhimu hazikuonekana kwa kipindi cha miaka 100 tangu kufariki kwake dunia. Miongoni mwa athari za Johann Friedrich Hölderlin ni 'Sherehe ya amani' na 'Mashairi ya Usiku'.
Siku kama ya leo miaka 153 iliyopita alifariki dunia, Haj Abdul-Hussein Tehrani, maarufu kwa jina la Sheikhul-Iraaqiyyin, mmoja wa maulama wakubwa wa Iran. Haj Abdul-Hussein Tehrani alitabahari katika elimu ya fiqhi, huku akiwa mcha-Mungu sana. Kadhalika alitambulika kwa kuwa na kumbukumbu ya hali ya juu katika msomo ya dini. Mbali na fiqhi, pia alikuwa alimu katika elimu ya hadithi na tafsiri ya Qur'an Tukufu. Alifanya juhudi kubwa katika kuasisi maktaba na kukusanya turathi za Kiislamu ambapo baada ya kufariki kwake dunia kuliasisiwa maktaba kubwa kwa ajili ya wanafunzi wa Kiislamu.
Siku kama hii ya leo miaka 139 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Juni 1879 vilianza vita vilivyochukua muda wa miaka mitano kati ya nchi za Peru, Chile na Bolivia. Vita hivyo vilianza baada ya serikali ya Bolivia kutiliana saini na shirika moja la Chile na kisha kukiuka makubaliano ya mkataba huo, na kusababisha Chile kuishambulia kijeshi Bolivia. Hatimaye Chile ilijipatia ushindi kwenye vita hivyo, na kutiliana saini makubaliano mapya na nchi za Bolivia na Peru, ambapo kwa mujibu wa makubaliano hayo, ufukwe wote wa Bolivia na sehemu ndogo ya ardhi ya Peru ilichukuliwa na Chile.
Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita na kufuatia kushindwa Waarabu katika vita na utawala haramu wa Israel, askari wa utawala huo waliingia katika mji wa kihistoria na kidini wa Beitul Muqaddas. Waislamu wanaupa utukufu maalumu mji huo kutokana na kuwa Msikiti Mtukufu wa al-Aqsa ambacho ni kibla cha kwanza cha Waislamu unapatikana humo na pia kutokana na kuwa ni sehemu ambayo Mtume Mtukufu (saw) alipaa mbinguni katika tukio la Mi'raaj kutokea hapo. Lakini tokea utawala ghasibu wa Israel uzikalie kwa mabavu ardhi za Wapalestina, utawala huo umekuwa ukitekeleza njama hatari za kuuharibu msikiti huo na badala yake kujenga hapo hekalu bandia la Nabii Suleiman (as). Utawala huo vilevile unatekeleza siasa hatari ya kuvuruga muundo wa jamii asili ya wakazi wa mji wa Beitul Muqaddas kwa kuwafukuza Wapalestina katika ardhi zao na kujenga hapo vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi na Kizayuni. Walowezi hao wa Kizayuni wanafanya njama kubwa ya kufuta kabisa nembo na alama za Wapalestina na Waislamu katika mji huo mtukufu wa Beitul Muqaddas.
Na siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Juni 1980, ndege za kijeshi za utawala wa Kizayuni wa Israel zilishambulia na kukiharibu kituo cha nyuklia cha Tamouz kilichoko karibu na Baghdad, mji mkuu wa Iraq. Licha ya kuharibiwa kikamilifu kituo hicho cha nyuklia, na kusababisha fikra za waliowengi duniani kuchukizwa na kulaaniwa kitendo hicho na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, amma hakuna hatua zozote za kivitendo zilizochukuliwa dhidi ya utawala wa Israel. Hivi sasa utawala huo ghasibu unamiliki zaidi ya vichwa 200 vya makombora ya nyuklia, na umekuwa ukikataa kuwaruhusu wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kuikagua mitambo na vinu vyake vya nyuklia.