Sep 24, 2018 08:53 UTC
  • Jumatatu tarehe 24 Septemba 2018

Leo ni Jumatatu tarehe 14 Muharram 1440 Hijria sawa na Septemba 24, 2018.

Miaka 40 iliyopita katika siku kama hii ya leo, vikosi vya usalama vya utawala wa Baath nchini Iraq vikishirikiana na utawala wa Shah viliizingira nyumba ya Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu huko Najaf. Kwa kuzingatia uhusiano wake mzuri na utawala wa Shah, utawala wa zamani wa Iraq ulimtaka Imam Khomeini asifanye mahojiano na waandishi wa habari, kutoa taarifa, kuhutubia wala kuzungumzia hali ya mambo ya Iran dhidi ya utawala wa Shah. Imam Khomeini aliwajibu kwa kusema kuwa: "Nitatekeleza wajibu wangu wa kisheria popote pale nitakapokuwa." Baada ya hapo, serikali ya wakati huo ya Iraq, ilimlazimisha Imam Khomeini kuondoka Iraq na hatua hiyo ikaandaa uwanja wa hijra ya kihistoria ya Imam Khomeini ya kuelekea Paris, Ufaransa na kupamba moto harakati za Mapinduzi ya Kiislamu.

imam Khomeini akiondoka Iraq kuelekea Paris

Katika siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, Guinea Bissau ilitangaza uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mreno. Guinea Bissau iligunduliwa mwaka 1446 na Mwana Mfalme Henry aliyekuwa akitawala Ureno pamoja na wenzake na kuwa koloni la nchi hiyo. Guinea Bissau ambayo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Guinea Ureno, ilikuwa miongoni mwa vituo vya biashara ya utumwa ya wazungu katika karne za 17 na 18. Na hatimaye ilipofika mwaka 1974, Ureno ikakubali kuwa huru nchi ya Guinea Bissau. Guinea Bissau iko kaskazini magharibi mwa Afrika na katika pwani ya Bahari ya Atlantic.

Bendera ya Guinea Bissau

Katika siku kama ya leo miaka 79 iliyopita, ndege za kijeshi za Ujerumani zilianza kufanya mashambulio makubwa dhidi ya mji mkuu wa Poland, Warsaw. Mashambulio hayo yalifanyika sambamba na kuanza Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na yalidumu kwa muda wa siku tatu. Hatimaye wananchi wa mji huo walisalimu amri mbele ya majeshi ya Ujerumani baada ya mapambano na siku kumi na moja. Mashambulio hayo ya kinyama yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 15,000.

Sehemu ya mji wa Warsaw

Siku kama ya leo miaka 116 iliyopita, alifariki dunia Sayyid Abul Qasim Lahore. Abul Qasim Bin Hussein Bin Naqi Ridhawi Taqawi Lahore na aliyekuwa faqihi na mfasiri wa Qur'an Tukufu alizaliwa mjini Kashmir. Aidha Sayyid Abul Qasim Lahore alikuwa miongoni mwa maulama wakubwa nchini India huku akiwa ameandika vitabu vingi katika uwanja huo. Msomi huyo alizikwa mjini Lahore. Miongoni mwa vitabu vyake ni pamoja na 'Burhanu Shaqqul-Qamar wa Raddun-Nayril-Akbar' 'As-Swiraatul-Mustaqim.'

Siku kama ya leo miaka 177 iliyopita, alifariki dunia mjini Isfahan, moja ya miji maarufu ya Iran, Sayyid Sayyid Sadrud-Din Musawi Amili, msomi na mtaalamu wa hadithi wa Kiislamu. Sayyid Sadrud-Din Musawi Amili alizaliwa katika moja ya viunga vya mji wa Jabal Amel, nchini Lebanon. Akiwa kijana mdogo alisafiri nchini Iraq ambapo baada ya kuhitimu masomo yake ya awali katika hawza ya elimu ya mjini Najaf, alianza kufanya utafiti katika elimu kadhaa kama vile fiqhi, usulu fiqhi na hadithi na kufikia daraja la juu katika uwanja huo. Sayyid Sadrud-Din Musawi Amili ameandika vitabu mbalimbali katika uga wa elimu ya sheria, nahawu na mifano ya aya za Qur’ani Tukufu.

Sayyid Sadruddin Musawi

 

Tags