Dec 28, 2018 02:58 UTC
  • Ijumaa, Disemba 28, 2018

Leo ni Ijumaa tarehe 20 Mfunguo Saba Rabiuthani 1440 Hijria sawa na Disemba 28 Disemba 2018 Milaadia.

Miaka 39 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 7 Dey mwaka 1358 Hijria Shamsia, Imam Khomeini (MA)  mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alitoa amri ya kuanzishwa harakati ya kupambana na ujinga wa kutojua kusoma na kuandika. Imam Khomeini alitoa amri kwa wananchi wote wa Iran kushirikiana bega kwa bega kwa shabaha ya kumtokomeza adui ujinga. Hivi sasa kiwango cha watu wanaojua kusoma na kuandika nchini Iran kimeongezeka sana, na kufikia hatua kwa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO kuiweka Iran kwenye kundi la nchi zenye idadi kubwa ya watu wanaojua kusoma na kuandika.

Miaka 44 iliyopita katika siku kama ya leo, aliuawa shahidi Ayatullah Hussein Ghaffari aliyekuwa miongoni mwa wanazuoni na wanamapambano wa Kiislamu nchini Iran. Ayatullah Ghaffari aliuawa shahidi akiwa katika jela ya utawala wa wakati huo wa kifalme hapa Iran. Ayatullah Ghaffari aliendesha harakati za kupambana na utawala wa kidikteta wa Shah kwa kuandika vitabu na majarida mbalimbali. Baadaye alitiwa mbaroni na kutiwa jela na hatimaye aliuawa shahidi katika siku kama ya leo, baada ya kuvumilia mateso mengi gerezani.

Ayatullah Hussein Ghaffari

Siku kama ya leo miaka 93 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 28 Disemba 1925 alizaliwa Apollo Milton Obote Rais wa zamani wa Uganda. Obote aliiongoza Uganda kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza mwaka 1962. Aliiongoza Uganda akiwa Waziri Mkuu kuanzia mwaka 1962 hadi 1966. Milton Obote alikuwa Rais wa Uganda kuanzia mwaka 1966 hadi 1971 alpoondolewa madarakani na Idi Amin Dada. Hata hivyo mwaka 1980 alirejea madarakani baada ya Idi Amin kuondolewa uongozi na kuiongoza nchi hiyo hadi mwaka 1985 wakati alipoondolewa madarakani na kulazimika kukimbilia Tanzania na baadaye Zambia. Obote alifariki dunia mwaka 2005 huko Johannesburg, Afrika Kusini kutokana na matatizo ya figo.

Apollo Milton Obote

Siku kama ya leo miaka 123 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 28 Disemba 1895 kwa mara ya kwanza katika historia ya sanaa ya filamu, filamu ya kwanza ya kisa ilioneshwa kwenye mkusanyiko wa watu wengi. Filamu hiyo ilitayarishwa na kuandaliwa na ndugu wawili waliojulikana kwa majina ya Auguste na Louis Lumiere. Miaka iliyofuata ilitengenezwa mitambo bora zaidi ya kurekodi na kuonesha filamu na hatua kwa hatua filamu zenye ubora wa juu na za aina mbalimbali zikaanza kuonyeshwa katika nchi mbalimbali duniani.

Auguste na Louis Lumiere

Na siku kama ya leo miaka 244 iliyopita, Joseph Priestley, mwanakemia na mwanafizikia wa Uingereza alifanikiwa kugundua gesi ya oksijeni. Msomi huyo aliishi katika kipindi kilichokuwa maarufu kama zama za dhahabu za kemia. Gesi ya oksijeni ina mchango na nafasi muhimu sana kwa maisha ya mwanadamu na viumbe vingine hai na huingia katika mwili wa mwanadamu wakati wa kupumua na kuchanganyika na chakula. Matokeo ya kazi hiyo ni kuzalishwa nishati ambayo hutumika katika kubakia hai mwanadamu. Joseph Priestley alifariki dunia mwaka 1804.

Joseph Priestley

 

Tags