Ijumaa tarehe Mosi machi 2019
Leo ni Ijumaa tarehe 23 Jumadithani 1440 Hijria sawa na tarehe Mosi machi 2019.
Siku kama ya leo miaka 204 iliyopita, ufalme wa siku mia moja wa Napoléon Bonaparte ulianza nchini Ufaransa baada ya Bonaparte kutoroka sehemu aliyokuwa amebaidishwa katika kisiwa cha Elba. Tarehe 27 mwezi Februari mwaka huohuo akiwa pamoja na wanajeshi elfu moja Napoleon Bonaparte alifanikiwa kutoroka katika kisiwa cha Elba ambako alikaa akiwa ubaidishoni kwa kipindi cha miezi kumi na kurejea Ufaransa na utawala wa kifalme ukaanza huko Ufaransa.
Siku kama ya leo miaka 127 iliyopita yaani tarehe 1 Machi mwaka 1892 Miladia, alizaliwa mjini Tokyo mwandishi na mtaalamu mkubwa wa Japan anayejulikana kwa jina la "Rhunosuke Akutagawa". Mwandishi huyo anahesabika kuwa mmoja wa waasisi wa kanuni mpya za fasihi huko Japan. Akutagawa ameacha athari muhimu na miongoni mwake ni vitabu vya "Binti wa Buibui" na "Tushi Gun." Mwandishi huyo alifariki dunia mwaka 1927.
Miaka 121 iliyopita siku kama leo, kisiwa cha Puerto Rico kilichoko katika ya Bahari ya Atlantic kaskazini mwa Amerika ya Kusini, kilikaliwa kwa mabavu na vikosi vya majeshi ya Marekani baada ya kumalizika vita vya kikoloni vya Uhispania na Marekani. Baada ya Marekani kukitwaa kwa nguvu kisiwa hicho ilikifanya ghala kubwa la silaha, kiasi kwamba Marekani iliasisi kambi 13 za kijeshi kisiwani humo. Kisiwa hicho ambacho mara kwa mara hukumbwa na ukosefu wa amani, miongoni mwa nchi zinazozungumza lugha ya Kihispania katika bara la America.
Na tarehe 10 Esfand miaka 40 iliyopita hayati Imam Ruhullah Khomeini kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran aliwasili katika mji wa kidini wa Qum baada ya kuwa uhamishoni kwa kipindi cha miaka 15. Imam alipelekwa uhamishoni na utawala wa Shah hapo mwaka 1343 Hijria Shamsia baada ya matukio ya umwagaji damu ya tarehe 15 Khordad mwaka 1342. Tarehe 12 Bahman mwaka 1357 Imam alirejea nchini akitokea Ufaransa na katika siku kama ya leo baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliwasili katika mji mtakatifu wa Qum na kuishi huko. Miezi kadhaa baadaye Imam Ruhullah Khomeini alihamia Tehran kutokana na udharura wa kuongoza harakati ya Mapinduzi.
