Ijumaa 19 Aprili 2019
Leo ni Ijumaa tarehe 13 Sha'aban 1440 Hijria, sawa na tarehe 19 Aprili, 2019 Miladia.
Miaka 2052 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya nadharia za wanahistoria, yaani tarehe 19 Aprili mwaka 33 kabla ya Miladia au kuzaliwa Nabii Issa AS, kulianzishwa mjini Roma maktaba ya kwanza ya ummah duniani yaani 'Public Library' na kila aliyekuwa na uwezo wa kusoma na kuandika alikuwa na haki ya kuingia humo na kusoma vitabu alivyotaka. Kabla ya Waroma kupata maktaba hiyo, Wasumeri, Waashuri, Wababeli na Wairani walikuwa na maktaba zao ingawa maktaba hizo hazikuwa zikitumika na watu wote, huku maktaba ya Waashuri ikiwa ndio maarufu zaidi. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, nchi ya kwanza ambayo ilianzisha asasi za uandishi na tarjama za vitabu duniani, ilikuwa ni Iran, ambapo karne 15 zilizopita zilikuwa zikifanya kazi hizo katika utawala wa Khosrow Anushirvan.

Siku kama ya leo miaka 137 iliyopita yaani 19 Aprili mwaka 1882, alifariki dunia mtaalamu wa elimuviumbe wa Uingereza Charles Darwin.Alizaliwa Februari 12 1809 nchini Uingereza. Msomi huyo alifanya utafiti kuhusu manma ya kutokea viumbe mbalimbali na alifanya safari ya muda mrefu duniani kwa ajili ya kukamilisha uchunguzi wake wa kielimu na baada tu ya kurejea aliandika kitabu maarufu cha "On the Origin of Species". Kwa mujibu wa nadharia ya Darwin ambaye ndiye aliyeanzisha mfumo wa Darwinism, chanzo cha viumbe vya leo ni viumbe vidogovidogo ambavyo vilibadilika kutokana na mazingira tofauti kwa miaka mingi na kufikia hali ya sasa. Fikra za Darwin zinapingana na mafundisho ya dini za mbinguni kuhusu namna ya kuumbwa mwanadamu lakini zimetumiwa kama msingi wa mifumo ya kilahidi kama ule wa Umaxi. Aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 73 na alizikwa pembizoni mwa Isaac Newton katika kanisa la Westminster Abbey mjini London.
Siku kama ya leo miaka 14 iliyopita, Kadinali Joseph Ratzinger alikabidhiwa uongozi wa Kanisa Katoliki Duniani baada ya kufariki dunia Papa John Paul wa Pili na kuchagua jina la Papa Benedict wa 16. Ratzinger alizaliwa mwaka 1927 nchini Ujerumani na alipanda daraja na kuwa askofu mwaka 1977 na hatimaye kufikia daraja ya ukadinali. Papa Benedict wa 16 alikabiliwa na matatizo mbalimbali akiwa kiongozi wa kanisa hilo ikiwa ni pamoja na mgogoro wa masuala ya kiroho katika nchi za Magharibi, ufisadi na utovu wa maadili pamoja na vitendo vya ubakaji vinavyofanywa na maaskofu na makasisi dhidi ya watoto wadogo. Papa Benedict wa 16 alilazimika kuachia uongozi wa Kanisa Katoliki Februari mwaka 2013 baada ya kuzongwa na kashfa nyingi za viongozi wa ngazi za juu ndani ya kanisa hilo.
Na miaka 25 iliyopita yaani tarehe 19 Aprili 1995 mlipuko uliosababisha mauaji wa Oklahoma City nchini Marekani. Katika siku hiyo Timothy McVeigh alilipua bomu mbele ya jengo la Federali la mji wa Oklahoma City ambalo liliua watu 168 . Mauaji hayo yalitambuliwa kuwa tukio kubwa zaidi la kigaidi katika historia ya Marekani hadi kabla ya mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001. McVeigh alisema kuwa sababu ya kuchukua hatua hiyo ni upinzani wake dhidi ya serikali ya federali ya Marekani na kulipiza kisasi tukio la kuchomwa moto makao ya kundi la Davidian katika mji wa Waco mwaka 1993 na kuuawa wafuasi 76 wa kundi hilo. Hujuma hiyo dhidi ya jengo la Federali ni tukio ambalo liliwaingiza woga na wahka Wamarekani na kubaini kuwa jamii ya nchi hiyo inakabiliwa na tishio kubwa la ndani ya nchi.