May 20, 2019 01:18 UTC
  • Jumatatu, Mei 20, 2019

Leo ni Jumatatu tarehe 14 Ramadhani mwaka 1440 Hijria, mwafaka na tarehe 20 Mei mwaka 2019 Miladia.

Miaka 1373 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 14 Ramadhani mwaka 95 Hijria, aliuawa shahidi Mukhtar bin Abi Ubaida Thaqafi mlipiza kisasi wa damu ya Imam Hussein bin Ali AS, mjukuu wa Mtume Mtukufu Muhammad SAW. Imam Hussein AS akiwa pamoja na wafuasi wake na watu wa familia yake, aliuawa shahidi baada ya kuingia kwenye vita visivyokuwa na mlingano na wafuasi wa Yazid bin Muawiya, kwa ajili ya kuilinda dini ukufu ya Kiislamu. Mukhtar alianzisha harakati zake katika mji wa Kufa. Kabla yake, kulijitokeza kundi la 'Tawwabiin' ambalo lilitekeleza harakati dhidi ya utawala wa Bani Umayya, kwa lengo la kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein AS. Mukhtar Thaqafi alitawala Kufa kwa muda wa mwaka mmoja hivi, hatimaye alishindwa na jeshi la Mus'ab bin Zubair na kuuawa.

Kaburi la Mukhtar Thaqafi

@@@@@@@@@@

Miaka 513 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 20 Mei mwaka 1506 Miladia, aliaga dunia baharia mashuhuri wa Kiitalia Christopher Columbus. Columbus alizaliwa Septemba 21 mwaka1451 Miladia huko kusini mwa Italia. Mwezi Agosti mwaka 1492 Miladia, Christopher Columbus, alianza safari yake kuelekea Bahari ya Atlantiki. Watu wengi wanamtambua Columbus kuwa mtu wa kwanza aliyevumbua bara la Amerika. Hata hivyo ni vyema kuashiria hapa kuwa, hiyo ni kwa mujibu wa historia ya watu wa Ulaya. Tangu wakati huo historia ya bara hilo ikaandikwa kwa mujibu wa matakwa ya wazungu na wahamiaji wapya. Historia hiyo iliambatana na machungu ya ukoloni kutoka maeneo tofauti ya dunia dhidi ya wakazi asili wa ardhi hizo, huku ubaguzi ukiwa ndizo siasa kuu zilizotekelezwa na wahamiaji hao. 

Christopher Columbus

@@@@@@@@@@

Miaka 59 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Kiafrika ya Cameroon ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Kwa miaka mingi nchi hiyo ilikuwa chini ya ukoloni wa nchi za Ulaya ikiwemo Ujerumani ambayo iliikalia kwa mabavu Cameroon kuanzia mwaka 1884.  Baada ya Ujerumani kushindwa katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia Ufaransa na Uingereza ziligawana baina yao ardhi ya Cameroon. Hata hivyo haukupita muda kabla ya kuanza mapambano ya kupigania uhuru nchini humo. Hatimaye mapambano ya kupigania uhuru nchini Cameroon yalizaa matunda katika siku kama ya leo baada ya nchi hiyo iliyoko magharibi mwa Afrika kujipatia uhuru.

Bendera ya Cameroon

 

@@@@@@@@@@

Na siku kama ya leo, miaka 56 iliyopita, mwafaka na tarehe 20 Mei mwaka 1963, kongamano la kihistoria la nchi za Afrika lilifanyika huko Addis Ababa, Ethiopia. Madola mengi ya Kiafrika yalijinyakulia uhuru katika miaka ya 60 na 70, na katika kipindi hicho hayakuwa na uhusiano baina yao. Ili kuunda jumuiya ya kwanza itakayozikurubuisha nchi za Afrika, kongamano la kwanza la nchi hizo lilifanyika katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa tarehe kama ya leo. Kongamano hilo ilikuwa hatua ya mwanzo ya kuasisiwa Jumuiya ya Nchi za Afrika OAU. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, Umoja wa Afrika (AU) ulichukua nafasi ya Umoja wa Afrika (OAU) ambao uliundwa mwaka 1963 kwa shabaha ya kusimamia maslahi ya nchi wanachama, kuhamasisha maendeleo ya bara hilo na kutatua migogoro kati ya nchi Afrika.

Umoja wa Afrika