Jul 30, 2019 02:26 UTC
  • Jumanne tarehe 30 Julai mwaka 2019

Leo ni Jumanne tarehe 27 Dhulqaada 1440 Hijria inayosadifiana na Julai 30 mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka minne uliopita yaani tarehe 27 Dhulqaada 1436 Hijria winchi lililokuwa limewekwa katika eneo la mashariki ndani ya Msikiti mtakatifu wa Makka lilianguka na kuua idadi kubwa ya mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu. Katika tukio hilo lililotokea saa 17.1 kwa wakati wa Makka, mahujaji 107 waliuawa na wengine 238 walijeruhiwa. Mahujaji wengi waliopoteza maisha katika tukio hilo ni kutoka nchi za India, Pakistan, Indonesia na Iran. Serikali ya Saudi Arabia ilitangaza kuwa sababu ya kuanguka winchi hiyo ni upepo na tufani kali iliyovuma mjini Makka.

Winchi lililoua mahujaji zaidi ya mia moja ndani ya Msikiti wa Makka

Tukio hilo lililodhiohirisha uzembe wa serikali ya Saudia na la lile la maafa ya Mina katika siku ya Idi Kubwa mwaka huo huo ni miongoni mwa matukio machungu zaidi katika historia ya ibada ya Hija. Maelfu ya Waislamu walifariki dunia katika maafa ya Mina wakati wa kuelekea kwenye eneo la kumpiga mawe shetani.

Siku kama ya leo miaka 12 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Ali Akbar Faydh mashuhuri kwa jina la Ayatullah Mishkini. Ayatullah Mishkini alisoma kwa wanazuoni wakubwa wa zama hizo kama Ayatullah Burujerdi na Imam Khomeini. Alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kujiunga na harakati ya mapambano ya Imam Khomeini dhidi ya utawala wa Shah. Alitiwa nguvuni na kufungwa jela mara kadhaa sambamba na kubaidishwa. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Mishkini alishika nyadhifa mbalimbali, na muhimu zaidi ni ule wa Mwenyekiti wa Baraza la Wanazuoni Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu na Kusimamia Kazi Zake. Alimu huyo ameandika vitabu vingi.

Ayatullah Ali Akbar Faydh

Tarehe 8 mwezi Mordad kwa mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia ni siku ya kumuenzi mwanafalsafa, arifu na msomi mkubwa wa Kiislamu Shahabuddin Sohravardi aliyepewa lakabu ya Sheikhul Ishraq. Sheikhul Ishraq alizaliwa mwaka 549 Hijria karibu na mji wa Zanjan kaskazini magharibi mwa Iran. Alibobea haraka katika taaluma nyingi za Kiislamu za wakati huo hususan falsafa. Sheikh Sohravardi alifanya safari katika miji mbalimbali ya nchi za Kiislamu kwa ajili ya kutafuta elimu. Aliasisi mfumo mpya wa falsafa uliopewa jina la Ishraq. Sheikhul Ishraq ameandika vitabu vingi kama vile "Hikmatul Ishraq", al Mabda wal Maad", na "Talwihat".

Shahabuddin Sohravardi

Siku kama ya leo miaka 121 iliyopita, alifariki dunia Otto von Bismarck, Kansela wa kwanza na mwanasiasa mkongwe wa Ujerumani. Bismarck aliongoza vita vitatu ambavyo viliainisha mustakbali wa Ujerumani kama nchi huku akikabiliana pia na madola ya Ulaya wakati huo. Bismarck alikuwa rais wa Prussia akiwa na umri wa miaka 28 na kwa mara ya kwanza akawa pia Kansela wa Ujerumani. Mwaka 1862 aliteuliwa kuwa waziri mkuu wa Prussia na kuanzisha mpango wa Ujerumani moja. Ili kufikia lengo hilo hakuwa na njia nyingine ghairi ya kuiondoa Austria katika shirikisho la majimbo ya Ujerumani ya Kikatoliki sambamba na kulikomboa jimbo la Schleswig-Holstein kutoka udhibiti wa Denmark na kuhitimisha upenyaji wa Ufaransa katika majimbo ya kusini mwa Ujerumani. Baada ya kujiimarisha kijeshi alipigana vita vitatu na kufikia malengo yake katika vita vyote hivyo. Kwa mujibu wa historia, Otto von Bismarck alizishinda nchi za Denmark, Austria na Ufaransa, kulikoenda sambamba na kuteuliwa kuwa kansela wa Ujerumani mwaka 1890.

Otto von Bismarck

Tarehe 30 Julai miaka 72 iliyopita alifariki dunia mvumbuzi wa Kimarekani anayejulikana kama baba wa sekta ya utengenezaji magari wa nchi hiyo Henry Ford. Alizaliwa tarehe 30 Julai 1863 katika familia ya kimaskini na tangu utotoni alikuwa na hamu kubwa ya masuala ya mekaniki. Siku moja Ford aliona gari likitembea barabarani bila ya kuvutwa na farisi na akaamua kutengeneza gari lake mwenyewe. Henry Ford alifanyia majaribio mkokoteni wa kwanza usiotumia farasi akiwa na umri wa miaka 12 tu. Mvumbuzi huyo aliboresha zaidi mkokoteni huo na mwaka 1896 alifanikiwa kutengeneza gari lake la kwanza. Mwaka 1895 alipewa haki ya kutengeneza magari licha ya kwamba watu wengine pia walikuwa wanatengeneza chombo hicho na mwaka 1903 aliasisi kampuni ya magari ya Ford Motor. Ford aliwapiku watengeneza magari wengine kwa kutengeneza magari mengi ya bei rahisi.

Henry Ford

 

Tags