Jumatano, 31 Julai, 2019
Leo ni Jumatano tarehe 28 Dhulqaada 1440 Hijria sawa na Julai 31 mwaka 2019.
Siku kama ya leo miaka 1080 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Abul-Qassim Tabarani mmoja wa maulama wa Kiislamu wa mjini Isfahan Iran aliaga dunia. Alikuwa mmoja wa wanazuoni, wasomi na wapokezi mashuhuri wa hadithi wa karne ya nne Hijria. Abul Qassim Tabarani alifanya safari katika ardhi mbalimbali za Kiislamu kwa ajili ya kukusanya hadithi. Baada ya miaka 33 ya uhakiki na utafiti alianza kufundisha na kufanikiwa kulea na kutoa wanafunzi wengi mno. Vitabu muhimu zaidi vya msomi huyu wa Kiislamu al Mu'jamul Kabiir, al Mu'jamul Ausat na al Mu'jamul Saghiir.

Miaka 788 iliyopita katika siku kama ya leo As’ad bin Halwan Dimashqi daktari na tabibu mashuhuri wa Kisyria alifariki dunia. Alizaliwa mwaka 503 Hijria na baada ya kusoma elimu ya tiba aliibuka na kuwa katika orodha ya matabibu mashuhuri wa zama zake. Bin Hal’wan alikuwa ametabahari pia katika fani ya fasihi, mantiki na hisabati na ameacha athari zenye thamani kubwa katika fani hizo.

Tarehe 31 Julai miaka 213 iliyopita ardhi ya Cape huko kusini mwa bara la Afrika ilivamiwa na wanajeshi wa Uingereza. Ardhi ya Cape au mji wa Cape Town ni sehemu ya kusini ya nchi ya Afrika Kusini iliyoko pembeni ya Rasi ya Tumaini Jema au (Cape of Good Hope) ambayo ipo kati ya bahari za Atlantic na Hindi. Eneo hilo lina utajiri mkubwa wa dhahabu na almasi na ni kwa sababu hiyo ndiyo maana daima wakoloni wakawa wanalikodolea jicho la tamaa.
Miaka 133 iliyopita aliaga dunia Franz Liszt mtunzi wa nyimbo wa Hungary. Franz alizaliwa mwaka 1811. Franz Liszt pia alikuwa na kipawa na maarifa makubwa katika utungaji wa nyimbo. Nyimbo Hungarian Rhapsodies na shairi la Symphony ni miongoni mwa kazi za utunzi wa Franz Liszt.
Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita aliaga dunia Antoine de Saint-Exupery mwandishi na mwana anga wa Kifaransa katika Vita vya Pili vya Dunia baada ya ndege yake kuanguka. Exupery alizaliwa mwaka 1900 katika mji wa Lyon nchini Ufaransa. Mwandishi Antoine de Saint Exupery alijishughulisha na masuala ya kusafiri angani kutokana na kupenda sana fani hiyo. Aidha alijiunga na jeshi la Ufaransa katika Vita vya Pili vya Dunia na kuwa afisa wa masuala ya usafirishaji wa posta. Siku hiyo Antoine de Saint Exupery alirusha ndege hewani akiwa katika kazi zake za kawaida, lakini ndege yake ilitoweka na athari za mwili wake na ndege hiyo hazijaonekana hadi leo hii. Mwandishi huyo ameandika vitabu kadhaa na miongoni mwake ni "The Little Prince", Southern Mail na Night Flight."
Tarehe 31 Julai miaka 59 iliyopita kiongozi wa Waislamu Wamarekani weusi Elijah Muhammad alitaka kuundwe dola la watu wuesi chini ya usimamizi wa serikali ya Federali ya Marekani. Lengo la wito huo lilikuwa kuwakomboa watu weusi na ubaguzi wa rangi nchini Marekani. Elijah Muhammad alikubali dini ya Uislamu baada ya kuathiriwa na kiongozi mwingine wa Waislamu weusi wa Marekani aliyejulikana kwa jina la Wallace Fard Muhammad, mwasisi wa chama cha Nation of Islam na alihesabiwa kuwa miongoni mwa vinara wa harakati hiyo ya kupigania dola la Wamarekani weusi. Hata hivyo baadhi ya wanaharakati wa chama hicho kama Malcom X hawakukubaliana na itikadi na sera za Elijah Muhammad. Ilikuwa wazi kwamba serikali ya Washington isingekubaliana na fikra ya kuanzishwa dola la Wamarekani weusi nchini humo.
Tarehe 9 Mordad mwaka 1366 Hijria Shamsia yaani siku kama ya leo miaka 32 iliyopita kulitokea tukio la kusikitisha la Ijumaa ya Damu mjini Makka. Siku hiyo mamia ya mahujaji wa Kiirani na mahujaji kadhaa wa nchi nyinginezo wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu waliuawa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa serikali ya Saudi Arabia, walipokuwa wakitekeleza faradhi ya kujibari na kujiweka mbali na washirikina ndani ya Nyumba ya Mwenyezi Mungu. Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu hutekeleza ibada hiyo kila mwaka wakati wa Hija, kutokana na mafunzo ya Kiislamu na Qur'ani Tukufu, ambapo sambamba na kutoa wito wa umoja na mshikamano baina ya Waislamu, hutoa tangazo la kujiweka mbali na maadui wa Uislamu hasa Marekani na utawala ghasibu wa Israel. Siku hiyo askari wa Kiwahabi wa Saudia walishambulia mahujaji hao kwa risasi na kuua mahujaji 400 za Kiirani na kujeruhi wengine zaidi ya elfu moja.