Ijumaa tarehe 30 Agosti mwaka 2019
Leo ni Ijumaa tarehe 28 Dhulhija 1440 Hijria sawa na Agosti 30 mwaka 2019.
Tarehe 28 Dhulhija miaka 1377 iliyopita, yaani miaka miwili baada ya harakati na mapambano ya mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) Imam Hussein bin Ali (AS) katika ardhi ya Karbala hapo mwaka 61 Hijria, kulijiri tukio la Harrah. Mwaka huo watu wa mji mtukufu wa Madina waliokuwa wamechoshwa na dhulma na ukatili wa mtawala Yazid bin Muawiya, walimfukuza gavana wake mjini humo Marwan bin Hakam. Baada ya tukio hilo Yazid alituma jeshi likiongozwa na mtumishi wake mmwaga damu na mtenda dhulma Muslim bin Uqbah katika mji mtakatifu wa Madina na kuliamuru kufanya mauaji makubwa mjini humo na kupora mali. Mauaji kama hayo hayakuwahi kushuhudiwa katika historia ya zama za awali za Uislamu na wanahistoria wamesema kuwa Waislamu zaidi ya elfu kumi wakiwemo maswahaba wa Mtume, waliuawa katika shambulizi hilo. Vitabu vya historia pia vinasema utawala wa Yazid bin Muawiya ulihalalisha mji wa Madina kwa askari wake kwa muda wa siku tatu na kwamba wasichana na wanawake wa maswahaba walinajisiwa katika tukio hilo.

Siku kama ya leo miaka 148 iliyopita, alizaliwa Ernest Rutherford, mtaalamu mkubwa wa fizikia wa nchini Uingereza maarufu kwa jina la baba wa nishati ya nyuklia. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali eneo alikozaliwa, Ernest alielekea katika mji wa kielimu wa Cambridge na kujiunga na chuo kikuu cha mji huo. Kuanzia mwaka 1919 Rutherford alitokea kuwa mhadhiri mwenye tajriba katika uga wa fizikia chuoni hapo, huku akijiunga na jumuiya ya kifalme ya mjini London hapo mwaka 1903. Mwaka 1904, msomi huyo alisambaza kitabu chake alichokipa jina la ‘Shughuli za Mionzi’. Baadaye Ernest Rutherford aliongoza kundi la utafiti katika chuo kikuu cha Manchester, kundi ambalo haraka liliweza kuandaa nadharia mpya kuhusiana na muundo wa atomiki. Mwaka 1908 Miladia, msomi huyo alitunukiwa zawadi ya Nobel kutokana na shughuli zake hizo na kupata umaarufu mkubwa katika uga huo.
Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, Jamhuri ya Azerbaijan ilitangaza uhuru wake kutoka Urusi ya zamani. Ardhi ya Azerbaijan ilitekwa na kukaliwa kwa mabavu na silsila ya Kiirani ya Wasasani tangu mwanzoni mwa karne ya Tatu Miladia na katika kipindi kikubwa cha historia yake ilikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Vita kati ya Urusi ya zamani na Iran vilijiri mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia, kufuatia kupenda kujitanua kwa utawala wa kifalme wa Tsar huko katika Umoja wa Kisovieti. Iran ilipata pigo katika vita hivyo na kupelekea sehemu moja ya ardhi ya kaskazini ya Azerbaijan kukaliwa kwa mabavu na Urusi ya zamani mwaka 1813 kwa mujibu wa mkataba wa Golestan.
Siku kama ya leo miaka 20 iliyopita, wananchi wa Timor ya Mashariki huko kusini mashariki mwa bara Asia walishiriki katika kura ya maoni na kuchagua kujitenga nchi hiyo na Indonesia. Kisiwa cha Timor ya Mashariki sambamba na visiwa vingine vya Indonesia kilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Kireno mwaka 1511 Miladia. Timor Mashariki iliunganishwa na Indonesia mwaka 1976.
Leo tarehe 8 Shahrivar kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia imepewa jina la Siku ya Kupambana na Ugaidi. Sababu ya kupewa jina hilo ni mauaji yaliyofanywa na wapinzani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya Rais wa wakati huo wa Iran, Muhammad Ali Rajai na Waziri Mkuu Hujjatul Islam Muhammad Javad Bahonar.
Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, Muhammad Ali Rajai Rais wa wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Waziri Mkuu Hujjatul Islam Walmuslimiin Muhammad Javad Bahonar waliuawa shahidi baada ya kutokea mlipuko mkubwa wa bomu katika ofisi ya Waziri Mkuu. Jinai hiyo ya kinyama ilifanywa na kundi la kigaidi la Munafiqeen (MKO). Rajai alianza kazi ya ualimu sambamba na kushiriki kwake katika harakati za mapambano dhidi ya utawala dhalimu wa Shah na kuendelea katika njia hiyo hadi palipopatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, shahidi Rajai alihudumu nyadhifa za Mbunge, Waziri wa Elimu na Malezi, Waziri Mkuu na hatimaye Rais. Wakati wa kipindi cha Urais wake, Rajai alimteua Dakta Muhammad Javad Bahonar kushika wadhifa wa Waziri Mkuu. Kutokana na juhudi, bidii na ikhlasi waliyokuwa nayo katika kulihudumia taifa la Iran ili kupeleka mbele malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu, maadui wa mfumo wa Kiislamu hawakufurahishwa na utendaji wao huo na ndio maana katika tarehe kama ya leo, wakatega bomu katika ofisi ya Waziri Mkuu na kuwauwa shahidi. Imam Khomeini (MA) Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema baada ya kufa shahidi Rajai na Bahonar kuwa "thamani za mabwana hawa Rajai na Bahonar ni hizi kuwa, viongozi hao walikuwa bega kwa bega na wananchi."