Mar 22, 2020 02:32 UTC
  • Jumapili, Machi 22, 2020

Leo ni Jumapili tarehe 27 Rajab mwaka 1441 Hijria, sawa na tarehe 22 Machi 2020 Miladia

Siku kama ya leo miaka 1454 iliyopita, Mtume Mtukufu wa Uislamu Muhammad Mustafa (saw) alibaathiwa yaani kupewa Utume na Mwenyezi Mungu. Kipindi hicho Mtume Muhammad (s.a.w) alikuwa na umri wa miaka 40. Mtume Muhammad (saw) alianza kutafakari na kudurusu maumbile ya dunia akiwa bado mdogo na daima alikuwa akifirikia njia za kunyanyua utukufu wa mwanadamu. Alikuwa maarufu kwa ukweli, uaminifu na kutenda mema. Jumla ya sifa hizo njema zilimfanya Muhammad (s.a.w) kuwa shakhsia mwenye hadhi na heshima kubwa katika jamii. Alipitisha muda wake mwingi katika ibada na kutafakari katika Pango la Hiraa. Malaika Jibrail alimteremkia Muhammad akiwa katika pango hilo na kumpa bishara ya kwamba ameteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Mtume wake kwa walimwengu wote. Tangu siku hiyo Mtukufu huyo alipewa jukumu kubwa la kuongoza wanadamu na kupambana na ujahili, ukafiri, dhulma na uonevu. Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa siku hii adhimu.

Kubaathiwa Mtume Muhammad

Siku kama ya leo miaka 974 iliyopita alizaliwa faqihi, mfasiri wa Qur'ani na msomi wa Kiislamu na Kiirani, Jarullah Zamakhshari. Mwanazuoni huyo pia alikuwa gwiji katika elimu za hadithi na fasihi ya lugha ya Kiarabu. Msomi huyo wa Kiirani ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Muqaddimatul Adab na Asasul Balagha. Kitabu muhimu zaidi cha Jarullah Zamakhshari ni tafsiri ya Qur'ani ya al "Kash'shaf".

Eneo alikozikwa Jarullah Zamakhshari

Siku kama ya leo miaka 213 iliyopita, alifariki dunia Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa msomi na fakihi mtajika wa Kishia. Alizaliwa mjini Najaf huko Iraq na kuanza kujihusisha na masomo ya dini tokea kipindi cha utoto wake. Awali alisoma masomo ya msingi kwa baba yake na kisha baadaye akahudhuria masomo kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kama sayyid Mahdi Bahr al-Uluum. Baadaye Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa alianza kufundisha na kuandika vitabu na kufanikiwa kuwalea wanafunzi wengi na vile vile kuandika vitabu vingi katika nyanja mbalimbali.

Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa

Siku kama ya leo miaka 139 iliyopita ulianzishwa Muungano wa Soka wa Kimataifa kwa shabaha ya kusimamia mashindano ya mpira wa miguu kote duniani. Kabla ya kuundwa muungano huo, mashindano ya soka yalikuwa yakifanyika katika nchi mbalimbali kwa muundo usiokuwa rasmi. Muungano huo ulibadilisha muundo wake na kujulikana baadaye kwa jina la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na liliandaa pambano rasmi la kwanza la kimataifa mwaka 1901, kati ya Uingereza na Ujerumani.

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA)

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, yaani sawa na tarehe 22 Machi 1945, iliundwa Jumuiya ya Waarabu kutokana na mapendekezo ya Farouk,  aliyekuwa mfalme wa wakati huo wa Misri na kutiwa saini makubaliano ya kuundwa jumuiya hiyo na serikali za Syria, Iraq, Saudi Arabia, Misri na Yemen mjini Cairo. Lengo la kuanzishwa jumuiya hiyo lilikuwa ni kuhifadhiwa ardhi zote, kujitawala nchi wanachama na kuwepo ushirikiano wa karibu wa kisiasa kiuchumi na kiutamaduni kati ya wanachama.

Jumuiya ya Waarabu

Siku kama ya leo miaka 16 iliyopita aliuawa shahidi Sheikh Ahmad Yassin mwanachuoni na mwasisi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas pamoja na watu wengine 10. Sheikh Ahmad Yassin aliuawa shahidi baada ya kumaliza swala ya Alfajiri katika msikiti mmoja ulioko eneo la Ukanda wa Gaza, wakati aliposhambuliwa na helikopta za utawala wa Kizayuni wa Israel. Sheikh Ahmad Yasin aliasisi harakati ya Hamas mwaka 1987 akishirikiana na wanamapambano wengine kadhaa wa Kipalestina na miaka miwili baadaye alifungwa jela na utawala ghasibu wa Israel. Mauaji ya mpigania uhuru huyo ambaye alikuwa kiwete na kipofu wakati wa kuuawa kwake, yalidhihirisha tena ugaidi wa kiserikali wa utawala haramu wa Israel.

Sheikh Ahmad Yassin