Jumatano, Machi 24, 2021
Leo ni Jumatano tarehe 10 Shaaban 1442 Hijria, mwafaka na tarehe 24 Machi 2021 Miladia.
Miaka 1020 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 10 Shaaban mwaka 422 Hijria, aliaga dunia Abu Abdullah Abdulbaqi, mmoja wa malenga mashuhuri wa karne ya tano Hijria. Alikuwa akiishi katika mji wa Baghdad, ilipo Iraq ya sasa. Mbali na kupata elimu kwa malenga na wanafasihi wakubwa, Abdulbaqi alikuwa akihudhuria pia darsa za maulamaa watajika wa mji huo katika zama hizo na kufaidika kwa elimu mbalimbali hasa elimu ya Hadithi. Abu Abdullah Abdulbaqi alikuwa na kipaji cha maumbile cha kusanifu mashairi na ameacha athari nyingi katika uga huo.

Miaka 688 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 10 Shaaban mwaka 754 Hijria aliaga dunia Majdu-ddin Abul Fawaaris, mmoja wa maulamaa wakubwa wa Kiislamu. Alizaliwa nchini Iraq; na baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi alikamilisha masomo yake ya dini kwa maulamaa wakubwa, mpaka yeye mwenyewe akafikia daraja ya kuwa alimu mwenye wanafunzi walio chini yake. Alichota elimu nyingi katika fani za Fiqhi, Usul-Fiqhi, Hadithi, Ilmul-Kalam, Tafsiri ya Qur'ani na Fasihi ya Kiarabu. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ameacha athari nyingi, miongoni mwao ni kitabu kiitwacho Kanzul-Fawaaid.

Siku kama ya leo miaka 115 iliyopita, inayosadifiana na 24 Machi 1905 alifariki dunia mwandishi na mtunzi wa hadithi wa Kifaransa Jules Verne akiwa na umri wa miaka 77. Verne alizaliwa Februari mwaka 1828 Miladia na alifanikiwa kuandika vitabu vingi na vya kuvutia vya hadithi ambapo ndani yake alielezea utabiri wake kuhusu namna mwanadamu atakavyopiga hatua katika uga wa sayansi. Miongoni mwa athari hizo ni pamoja na vitabu alivyoviita Twenty Thousand Leagues Under the Sea, A Journey to the Center of the Earth na Around the World in Eighty Days. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, filamu mbalimbali zenye kutoa mafunzo kwa watoto na vijana zilitengenezwa kwa kutumia aghalabu ya hadithi hizo zilizotungwa na Jules Verne.

Miaka 32 iliyopita katika siku kama ya leo, tarehe 24 Machi 1989, na baada ya kupita miaka 70, Msikiti Mkuu wa mji wa Ganjeh katika Jamhuri ya Azerbaijan ulifunguliwa tena baada ya kukarabatiwa. Msikiti huo ambao ni miongoni mwa majengo ya kihistoria ya nchi hiyo, ulifungwa kuanzia mwaka 1920 lakini ukaja kufunguliwa katika miezi ya mwisho mwa muongo wa 80 katika hafla maalumu iliyoambatana na kusaliwa Sala ya jamaa katika msikiti huo. Inafaa kuashiria hapa kuwa, baada ya mabadiliko ya kisiasa yaliyojiri katika Urusi ya zamani na jamhuri zilizokuwa chini ya shirikisho hilo la Kisovieti; na kwa kutilia maanani ombi la wananchi Waislamu wa Jamhuri ya Azerbaijan, makumi ya misikiti ya nchi hiyo ilikarabatiwa na kuanza kutumika. Hata hivyo serikali ya Azerbaijan imekuwa ikitekeleza sera za Kisekulari na hivyo kuweka vizuizi mbali mbali dhidi ya shughuli za misikiti nchini humo.

Na tarehe 24 Machi ni Siku ya Kimataifa ya kupambana na Kifua Kikuu, TB.
Tarehe 24 Machi mwaka 1882, Dokta Dr. Robert Koch, tabibu wa Kijerumani alitangaza kwa mara ya kwanza katika mkutano uliofanyika Berlin Ujerumani, ugunduzi wake kuhusu ugonjwa wa Kifua Kikuu au TB. Kwa sababu hiyo tarehe 24 Machi kila mwaka inaadhimishwa kama Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Kifua Kikuu.
