Apr 04, 2021 02:31 UTC
  • Jumapili, Aprili 4, 2021

Leo ni Jumapili tarehe 4 Aprili mwaka 2021 Miladia, inayosadifiana na tarehe 21 Shaaban mwaka 1442 Hijria.

Katika siku kama ya leo miaka 936 iliyopita alizaliwa Abdulkarim bin Muhammad as-Sama'ani maarufu kwa lakabu ya Tajul Islam faqih, mpokeaji hadithi na mwanahistoria mtajika wa karne ya sita Hijria huko katika mji wa Marw kusini mashariki mwa Tukimanistan ya sasa na Khurasan kubwa ya zamani. As-Sama'ani alipitisha miaka mingi ya umri wake kwa kufanya safari katika nchi mbalimbali kama vile Iran, Sham, Hijaz na nyinginezo na kunufaika na bahari kubwa ya wasomi wa kila sehemu aliyokwenda. Kitabu maarufu cha msomi Sama'aani ni kile alichokita kwa jina la " al Ansaab."

##########

Katika siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, nchi ya Senegal inayopatikana magharibi mwa Afrika ilipata uhuru. Senegal ilikuwa chini ya ushawishi na ukoloni wa Wareno kuanzia karne ya 15 Miladia na kuanzia karne ya 17 pia Wafaransa nao walianza kuiba maliasili na utajiri wa nchi hiyo. Senegal iko katika pwani ya bahari ya Atlantic ikipakana na Mauritania, Mali na Guinea Bissau.

Bendera ya Senegal

##########

Miaka 53 iliyopita katika siku kama ya leo Martin Luther King kiongozi wa mapambano ya raia weusi wa Marekani aliuawa kwa kupigwa risasi na mtu mmoja au watu kadhaa wasiojulikana. Martin Luther alizaliwa mwaka 1929 katika mji wa Atlanta huko Marekani. Alipata mafunzo katika Chuo Kikuu cha Boston na baadae akaanza kuongoza harakati ya ukombozi ya Wamarekani weusi dhidi ya ubaguzi wa rangi waliokuwa wakifanyiwa raia weusi nchini Marekani. Katika kipindi hicho, raia weusi wa Marekani waliasisi harakati ya nchi nzima ya kupinga ubaguzi wa rangi na vilevile katika kulalamikia sheria iliyokuwa ikiitambua jamii ya wazungu kama watu wa daraja ya juu huko Marekani. Kwa mujibu wa baadhi ya ushahidi ni kuwa shirika la ujasusi la Marekani CIA lilihusika katika mauaji hayo.

Martin Luther King

##########

Na katika siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, Zulfiqar Ali Bhutto, Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan alinyongwa. Bhutto ambaye alikuwa mwasisi wa Chama cha Wananchi alikuwa Rais wa Pakistan mwaka 1971. Mwaka 1977 Jenerali Muhammad Dhiaul Haq alifanya mapinduzi na kumuondoa madarakani Bhutto akimtuhumu kwa kufanya mauaji na kuisaliti Pakistan. Hatimaye tarehe 4 Aprili mwaka 1979 Zulfiqar Ali Bhutto alinyongwa, licha ya viongozi wa baadhi ya nchi duniani kutaka asamehewe.

Zulfiqar Ali Bhutto