Aug 31, 2021 02:22 UTC
  • Jumanne tarehe 31 Agosti 2021

Leo ni Jumanne tarehe 22 Muharram 1443 Hiijria sawa na Agosti 31 mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 983 iliyopita alifariki dunia msomi mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Muhammad bin Hassan Tusi, ambaye ni mashuhuri kwa jina la Sheikhul Twaaifa. Sheikh Tusi alizaliwa katika mji wa Tus kaskazini mwa Iran na akaelekea Iraq kwa ajili ya kutafuta elimu ya juu baada ya kukamilisha elimu ya msingi. Alipata elimu kwa wanazuoni mashuhuri wa Iraq na miaka kadhaa baadaye akaweka msingi wa chuo kikuu cha kidini cha Najaf. Kituo hicho cha kidini kina historia ya miaka elfu moja na ni moja ya vituo muhimu mno vya elimu ya Kiislamu. Sheikh Tusi ameandika vitabu vingi sana katika taaluma mbalimbali. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo wa Kiislamu ni tafsiri ya Qur'ani tukufu ya al Tibyan na vitabu vya hadithi na fiqhi vya al Istibsar na al Tahdhiib.

Katika siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, nchi ya Malaysia ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Wananchi wa Malaysia walianza kuingia taratibu katika dini ya Uislamu katika karne ya 13 Miladia. Ushawishi wa nchi za Ulaya ulianza kuenea nchini humo mwanzoni mwa karne ya 16 sambamba na kuwasili nchini humo baharia wa Kireno, Albuquerque. Uholanzi iliidhibiti nchi hiyo katika karne ya 17 na kuanza kuikoloni. Mwaka 1824 nchi za Uholanzi na Uingereza zilifikia makubaliano ambapo Waingereza waliichukua Malaysia na Waholanzi wakachukua Indonesia. Waingereza waliendelea kuikolonia Malaysia hadi nchi hiyo ilipopata uhuru katika siku kama ya leo.

Miaka 52 iliyopita katika siiku kama ya leo, alifariki dunia Ilya Ehrenburg mwandishi wa Umoja wa Kisovieti yaani Urusi ya zamani. Alizaliwa tarehe 17 Januari mwaka 1891 huko Kiev nchini Ukraine. Ilya ambaye anatambuliwa kuwa mkosoaji, mwandishi wa tamthilia, riwaya na hadithi alifanya kazi ya uandishi habari kwa miaka kadhaa huko Ulaya hususan Uhispania. Mwandishi huyo wa Kirusi aliandika vitabu visivyopungua 100 na miongoni mwa vitabu hivyo ni kile cha "tufani" na "kuanguka kwa Paris". 

Ilya Ehrenburg

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, Imamu Mussa Sadr, mwanazuoni na msomi mashuhuri wa Lebanon alitoweka katika mazingira ya kutatanisha akiwa safarini nchini Libya. Alizaliwa mnamo mwaka 1928 katika mji mtakatifu wa Qum nchini Iran na baada ya kuhitimu masomo yake alielekea Lebanon. Baada ya kuwasili nchini humo, Imamu Mussa Sadr alichukua hatua kubwa za kuboresha maisha ya Walebanoni waliokuwa katika hali mbaya ya kiuchumi, kijamii na kisiasa. Mwanazuoni huyo pia alikuwa muungaji mkono wa harakati za mapambano ya ukombozi wa Palestina na aliasisi Harakati ya Wanyonge kwa ajili ya kutetea haki za Waislamu wa Lebanon. Hadi sasa juhudi mbalimbali za kutaka kufahamu hatima ya Imamu Mussa Sadr bado hazijazaa matunda.

Imamu Mussa Sadr

Na siku kama ya leo miaka 16 iliyopita, karibu Waislamu 1000 wa Iraq waliaga dunia wakati walipokuwa katika hafla ya maombolezo katika mji wa Kadhemain jirani na Baghdad. Inaelezwa kuwa, zaidi ya Waislamu milioni moja wa Iraq walikuwa katika maombolezo ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Mussa al-Kadhim (as), ambapo kulishuhudiwa harakati za kutiliwa shaka sambamba na kusikika sauti za milipuko kadhaa. Watu wakiwa na lengo la kutoka katika eneo hilo walisongamana na kupelekea mamia ya wengine kukanyagwa huku wengine wakidondoka kutoka juu ya daraja.

Kadhemain

 

Tags