Apr 12, 2022 02:58 UTC
  • Jumanne tarehe 12 Aprili 2022

Leo ni Jumanne tarehe 10 Ramadhani 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 12 Aprili 2022.

Siku kama ya leo miaka 1446 iliyopita yaani tarehe 10 Ramadhani miaka mitatu kabla ya Hijra, alifariki dunia Bibi Khadija binti Khuwailid mke mwema na kipenzi wa Mtume Muhammad (saw) katika mji wa Makka. Bibi Khadija ambaye alikuwa mmoja wa wanawake mashuhuri na tajiri wa Makka, aliolewa na Mtume Muhammad (saw) miaka 15 kabla ya kubaathiwa mtukufu huyo. Bibi Khadija alikuwa mtu wa kwanza kuamini ujumbe wa Mtume Muhammad (saw) na alitumia uwezo na utajiri wake katika kuisaidia dini ya Uislamu. Kuweko Bibi Khadija (as) pamoja na Mtume wa Uislamu kulikuwa na umuhimu mkubwa kiasi kwamba Mtume (saw) alikitaja kifo cha mkewe huyo kipenzi kuwa ni msiba mkubwa. Mtume aliutaja mwaka aliofariki dunia Bibi Khadija na msaidizi wake mwingine mkubwa yaani Abu Talib, kuwa mwaka wa majonzi na huzuni. Hii ni kwa sababu Abu Talib, ami yake Mtume (saw), pia alifariki dunia mwaka huo huo.

Siku kama ya leo miaka 958 iliyopita waziri msomi na maarufu wa silsila ya utawala wa Seljuk, Khwaja (Khoja) Nizam al-Mulk, aliuawa na wapinzani wake. Alizaliwa mwaka 410 Hijiria katika mji wa Tous, kaskazini mwashariki mwa Iran ambapo alihudumu kwa kipindi cha miaka 40 katika utawala huo. Katika kipindi hicho Khwaja Nizam al-Mulk aliweza kuasisi shule kama vile Nidhamiyah ya mjini Baghdad na baada ya kuasisi shule hiyo alianza na kazi ya kuwafundisha elimu za fiqhi, tafiri ya Qur'ani na elimu nyingine karibu wanafunzi elfu sita. Athari maarufu ya Nizam al-Mulk ni kitabu cha 'Siyasat Nomeh' au 'Siyarul-Muluuk' chenye vipengee 50 kinachozungumzia mada tofauti zikiwemo za Qur'ani Tukufu, riwaya na sira ya Mtume Muhammad (saw), visa vya Mitume, hekaya na misingi ya uongozi wa nchi.

Siku kama ya leo miaka 202 iliyopita sawa na tarehe 12 Aprili 1820, dawa ya kutibu ugonjwa wa malaria iligundulika kutoka kwenye magamba ya mti wa Cinchona. Asili ya mti huu wenye majani ya kijani kibichi ni maeneo ya Amerika ya Kusini lakini hii leo unapandwa katika ameneo mengine ya dunia. Utomvu wa mti huu hutumika kutengeneza dawa chungu sana ya Quinine. Tarehe 12 Aprili mwaka 1820 kwa mara ya kwanza kabisa madaktari Pierre Joseph Pelletier na Joseph Bienaimé Caventou wa Ufaransa walifanyia majaribio dawa hiyo ya malaria katika Maabara ya Paris na kukaanza jitihada za kuzalisha dawa ya Quinine.

Siku kama ya leo miaka 199 iliyopita, sawa na tarehe 12 Aprili 1823, alizaliwa Alexandr Ostrovsky mwandishi wa tamthilia wa nchini Russia. Alihitimu masomo ya sheria katika chuo kikuu ingawa aliamua kujiunga na tasnia ya uandishi wa tamthilia na uigizaji. Karibu kila mwaka Alexandr Ostrovsky alikuwa akifanya uigizaji wa kihistoria au kuandika vichekesho ambapo alikuwa akiakisi hali halisi ya jamii. Alikuwa na taathira kubwa katika senema ya Russia. Miongoni mwa athari za mwanasanaa huyo ni pamoja na 'Binti wa Barafu', 'Msitu' 'Tufani' na 'Muhanga Mwingine.' Mwandishi huyo alifariki dunia mwaka 1886.

Alexandr Ostrovsky

Siku kama ya leo miaka 155 iliyopita, sawa na tarehe 12 Aprili 1867, Mutsuhito, mfalme maarufu na mwanamageuzi wa Japan aliingia madarakani nchini humo. Mfalme huyo aliingia madarakani wakati ambapo Japan ilikuwa inakabiliwa na changamoto nyingi za udhaifu katika nyuga tofauti. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Mutsuhito baada ya mwaka mmoja kuingia madarakani akabuni mapinduzi ya kijamii na kuanzisha mageuzi nchini Japan. Katika uwanja huo alihamisha mji mkuu kutoka Kyoto kwenya Tokyo sambamba na kubadili katiba ya nchi hiyo. Hata kama utawala wa Mutsuhito ulifikia tamati mwaka 1912, lakini Japan iliweza kupata maendeleo licha ya kuliibuka vita baina yake na China na Russia.

Mutsuhito

Katika siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, kwa mara ya kwanza mwanadamu alifika katika anga za mbali na kuizunguka dunia. Siku hiyo Yuri Gagarin mwanaanga wa Urusi ya zamani aliyekuwa na umri wa miaka 27 aliizunguka dunia kwa dakika 89 kwa kutumia chombo cha anga za mbali kwa jina la Vastok 1 na kwa msingi huo kukapatikana mafanikio makubwa katika sekta ya masuala ya anga. Gagarin alifariki dunia akiwa pamoja na mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa sekta ya masuala ya anga wa Urusi ya zamani katika ajali ya ndege hapo mwaka 1968.

Yuri Gagarin

Na siku kama hii ya leo miaka 30 iliyopita, Muhsin Saba mwalimu na mwandishi wa zama hizi wa Kiirani alifariki dunia. Baada ya kumaliza masomo yake ya msingi katika shule ya Darul Funun alielekea nchini Ufaransa. Alirejea nchini Iran baada ya kupata shahada ya uzamivu (PhD) na kuanza kufundisha. Dakta Muhsin Saba aliasisi Kundi la Taifa la Utambuzi wa Vitabu. Aidha hakuwa nyuma pia katika kutunga na kuandika vitabu.

Muhsin Saba

 

Tags