Jun 30, 2022 02:16 UTC
  • Alkhamisi, 30 Juni, mwaka 2022

Leo ni Alkhamisi tarehe 30 Dhulqaada 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 30 Juni mwaka 2022.

Katika siku ya mwisho ya mwezi Dhulqaada mwaka 220 Hijria Imam Muhammad Taqi AS mmoja kati ya wajukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi. Mtukufu huyo alipewa jina la 'Jawad' likiwa na maana ya mtu mkarimu sana kutokana na ukarimu wake mkubwa. Imam Jawad alizaliwa katika mwezi wa Ramadhani mwaka 195 Hijria na kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ridha (as). Kipindi cha maisha ya Imam Jawad kilikuwa kipindi cha kuchanua utamaduni wa Kiislamu na kuenea kwa fikra, itikadi na falsafa na kujitokeza mifumo ya fikra za Wagiriki na Warumi katika ulimwengu wa Kiislamu. Imam alifanya juhudi kubwa kulea kizazi chenye maarifa na kueneza elimu na mafundisho sahihi ya Uislamu kama njia ya kukabiliana na fikra za kigeni sambamba na kufichua siri na maovu ya watawala wa Bani Abbas. Suala hilo liliwakasirisha mno watawala hao ambao hatimaye waliamua kumuua shahidi mjukuu huyo wa Mtume (SAW) katika siku kama hii ya leo.

Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, yalianza mapambano ya raia wa Iraq chini ya uongozi wa Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Shirazi dhidi ya wavamizi wa Uingereza. Itakumbukwa kuwa baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia na kufuatia makubaliano ya waitifaki wa vita hivyo juu ya kugawana utawala wa Othmania, uongozi na usimamizi wa Iraq, Jordan na Palestina ulikabidhiwa mkoloni Mwingereza. Kuanzia wakati huo ukoloni wa London ukaanza rasmi kupora vyanzo na utajiri mkubwa wa nchi hizo. Baada ya kubainika makubaliano hayo ya kugawana mataifa ya Waislamu, kuliibuka mapinduzi makubwa katika maeneo yote ya Iraq. Aidha baada ya Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Shirazi kutoa fatwa ya jihadi, raia wa nchi hiyo walisimama kukabiliana na ukoloni huo wa Uingereza dhidi ya nchi yao, hata hivyo kutokana na uungaji mkono mkubwa wa madola ya kikoloni ya Magharibi kwa Uingereza na kadhalika njama mbalimbali za adui, mapinduzi hayo ya wananchi hayakuweza kufikia malengo yake makuu na badala yake Faisal Hussein akateuliwa kuwa mfalme wa Iraq.

Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Shirazi

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Zaire ya zamani) ilijitangazia uhuru na Joseph Kasavubu akawa rais wa nchi hiyo, huku Patrice Lumumba akiwa Waziri Mkuu. Kongo ilikoloniwa na Ubelgiji. Mapambano ya kudai uhuru yaliyoongozwa na Patrice Lumumba yalishika kasi katika miaka ya mwisho ya kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia na kupelekea nchi hiyo kujipatia uhuru wake. Hata hivyo baada ya Kongo kupata uhuru zilianza harakati nyingi za uasi zilizokuwa zikiungwa mkono na Ubelgiji. Katika upande mwingine kulishadidi mapigano kati ya Lumumba na Musa Chumbe kiongozi aliyekuwa akiungwa mkono na Ubelgiji. Hatimaye mnamo mwaka 1965 Jenerali Mobutu Sese Seko aliyeungwa mkono na Marekani alifanya mapinduzi ya kijeshi na kutwaa madaraka ya nchi hiyo ambapo badaye alianza kuwakandamiza wananchi masikini wa Kongo.

Katika siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, sawa na tarehe 9 Tir 1365 Hijria Shamsia, ilianza operesheni ya kijeshi ya Karbala -1 kwa ajili ya kukomboa mji wa Mehran huko magharibi mwa Iran uliokuwa umetwaliwa na jeshi vamizi la Saddam Hussein wa Iraq. Mji huo ulikaliwa kwa mabavu muda mfupi baada ya jeshi la Baath la Iraq kuvamia ardhi ya Iran Septemba 1981 na ulikombolewa na wapiganaji shupavu wa Iran katika operesheni makini ya Karbala-1.

Operesheni ya kijeshi ya Karbala -1

Miaka 33 iliyopita katika siku kama ya leo, Jenerali Omar Hassan Ahmad Al Bashir wa Sudan aliongoza mapinduzi ya kijeshi na kuuangusha utawala wa Swadiq Al Mahdi bila ya umwagaji damu. Utawala huo ulikuwa ukikabiliwa na matatizo mbalimbali ya ndani. Baada ya mapinduzi hayo Omar Hassan Al Bashir kwa kushirikiana na Hassan Al Turabi alianzisha chama cha Kongress ya Kitaifa huku yeye akiwa mwenyekiti wa chama hicho na rais wa nchi. Baada ya Al Bashir kutwaa urais alijitahidi kujitenga na siasa za Marekani, hatua ambayo iliipelekea serikali ya Washington kuichukia Khartoum na kuanzisha hatua za kiaduai dhidi ya serikali ya Al Bashir. Miongoni mwa hatua za kiadui zilizochukuliwa na Marekani dhidi ya Sudan ni kuwaunga mkono waasi wa Kusini mwa Sudan ambapo mwaka 2011 eneo hilo la kusini lilijitenga na Sudan na kujitangazia uhuru wake. Hata hivyo al Bashir alibadilisha mielekeo yake na kuwa tegemezi kwa utawala mwa kifalme wa Saudi Arabia. Utawala wa al Bashir ulitafunwa na ufisadi, utumiaji mbaya wa madaraka, hali mbaya ya uchuumi na kufuata kibubusa sera za Saudi Arabia katika vita vya Yemen. Mambo haya yaliwakasirisha Wasudani walioanzisha harakati ya upinzani dhidi ya al Bashir na hatimaye tarehe 11 Aprili mwaka 2019 kiongozi huyo alilazimika kung'atuka madarakani na kutiwa nguvuni kwa tuhuma za ufisadi na utakatishaji wa fedha chafu. Omar al Bashir anatumikia adhabu ya kifungo.

Omar al Bashir

Na katika siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, mfumo wa utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini ulihitimishwa. Kuanzia mwaka 1948, wazungu walio wachache nchini Afrika Kusini walianza kutekeleza siasa za kibaguzi dhidi ya wazalendo weusi. Kwa mujibu wa siasa hizo, wazungu waliokuwa wakiunda asilimia 20 tu ya wananchi wa Afrika Kusini walihesabiwa kuwa jamii bora zaidi na iliyokuwa na nafasi muhimu katika uendeshaji wa masuala ya nchi hiyo. Sheria kama vile za kupiga marufuku watu weusi kuoana na watu weupe na vilevile kushiriki katika harakati za kisiasa ni baadhi tu ya sheria za kibaguzi zilizotekelezwa na makaburu nchini Afrika Kusini. Siasa hizo ziliwakasirisha mno walimwengu na nchi nyingi duniani kukata uhusiano na utawala huo.

Nelson Mandela

 

Tags