Oct 30, 2022 05:14 UTC
  • Hakika ya Uwahabi 1

Makhawariji walikuwa wakisoma sana Qur’ani Tukufu, lakini pamoja na hayo hawakuzingatia maana yake halisi, hivyo, kusoma kwao Qur’ani na kuswali hakukuwakinga na upotofu uliowakumba. Kiburi walichokuwanacho kiliwapelekea kuwatuhumu Waislamu wengine wote kuwa makafiri na kuwa ni wao tu ndio walikuwa Waislamu wa kweli.

Bismillahi Rahmanir Raheem.

Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane.

Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Salamu za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya Waisamu wote wa ulimwengu ambao wanatamka kalima ya La Ilaha Ila Allah na wala hawafikirii jambo jingine isipokuwa kuwatakia heri na salama Waislamu wenzao. Salamu za Mwenyezi ziwe juu ya wanadamu wote wanaompwekesha na kupigania heri na wema. Hiki ni kipindi kipya ambacho kitakuwa kikikujieni kila wiki chini ya anwani ya Uwahabi, Ukweli au Bid'a na ambacho tunatumai kwamba kitaelimisha na kutunufaisha sote kwa pamoja, karibuni.

***********

Baada ya kuaga dunia Mtume Mtukufu (saw), Umma wa Kiislamu ulianza kukabiliwa na changamoto nyingi. Kabla ya kuaga kwake kulikuwa na watu ambao walikubali na kuingia kwenye Uislamu kwa ajili tu ya kulinda maslahi yao ya kidunia na kimaada lakini pamoja na hayo Mtume Mtukufu (saw) hakuwafukuza kwenye dini akitumai kwamba siku moja wangetambua njia ya haki na kuifuata. Watu hao daima walikuwa wakitafuta fursa ya kutoa pigo dhidi ya Uislamu na kila mara maslahi yao ya kiuchumi yalipogongana na thamani za Uislamu, hawakusita kuusaliti Uislamu na kupanga njama za kuudhuru. Kundi jingine lilipuuzilia mbali ushauri na mapendekezo ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw) ya kutumia akili na badala yake likaamua kutumia ujahili na ujinga kwa kushikamana na mambo ya kidhahiri tu ya dini na kutozingatia undani wake. Hali iliendelea kuwa hivyo hadi taratibu kukajitokeza uadui, ujahili na ukaidi ambao ulipelekea kujitokeza kundi la kwanza ambalo lilipuuza Uislamu wa kweli na kueneza itikadi zisizo na msingi katika dini hii tukufu.

Historia chungu ya kudhihiri makundi kwenye Uislamu ilianza mnamo mwaka wa 37 Hijiria sawa na 657 Miladia ambapo Muawiyya bin Abu Sufyan, gavana wa wakati huo wa Sham alianzisha vita dhidi ya Imam wa Waislamu Ali bin Abi Talib (as) katika eneo la Swiffin. Jeshi la Imam Ali (as) lilikuwa limekaribia kupata ushindi wa mwisho katika vita hivyo lakini hila na usaliti wa Amru bin al-Aas ukapelekea baadhi ya makamanda wa jeshi hilo kuhadaika na hatimaye wakakataa kutii amri ya Imam wao ambapo badala ya kuendelea kupigana kwenye medani ya vita walimtaka Imam Ali (as) asimamishe vita na kufanya mazungumzo na Muawiyya. Baada ya kushinikizwa na makamanda hao wasaliti hatimaye Imam alilazimika kufanya mazungumzo hayo lakini la kusikitisha ni kuwa makamda hao hao ambao walimtaka Imam Ali afanye mazungumzo walimgeuka na kumtuhumu kuwa alikuwa amefanya dhambi kubwa ya kusimamisha vita na kukubali mazungumzo. Walidai kwamba kwa kuwa alikuwa amefanya dhambi hiyo kubwa hivyo alikuwa amekufuru na kutoka kwenye Uislamu. Kundi hilo lilijulikama kama Khawarij kutokana na upinzani wake dhidi ya Imamu wa Waislamu nalo likawa kundi la kwanza kujitenga na mafundisho ya Uislamu halisi.

 

Makhawariji walikuwa wakisoma sana Qur’ani Tukufu, lakini pamoja na hayo hawakuzingatia maana yake halisi, hivyo, kusoma kwao Qur’ani na kuswali hakukuwakinga na upotofu uliowakumba. Kiburi walichokuwanacho kiliwapelekea kuwatuhumu Waislamu wengine wote kuwa ni makafiri na kuwa ni wao tu ndio walikuwa Waislamu wa kweli. Licha ya kuwa katika kipindi cha miaka mingi, kundi la Khawarij taratibu limetokomea na kutoweka lakini bado mawazo na fikra zake za kijahili na ukatili zingali zinaonekana katika pembe tofauti za ulimwengu wa Kiislamu.

*********

Katikati ya karne ya saba Hijiria kulijitokeza mtu aliyekuwa na fikra kali za kijahili kwa jina la Ibn Taymiyya. Jina lake halisi lilikuwa Taaqi ad-Deen Ahmad bin Abdul Halim. Alizaliwa mwaka 661 Hijiria (1262 Milaadia) katika mji wa Harran kusini mwa Uturuki ya leo. Kwa zaidi ya karne moja familia yake ilikuwa mbeba bendera ya madhehebu ya Hambal na baba yake akijulikana sana kama mhubiri na mwalimu wa dini ya Kiislamu. Sawa na walivyokuwa makhawarij wengine, Ibn Taymiyya alipuuza kabisa misingi ya akili na mantiki katika kubainisha na kufafanua mafundisho ya Uislamu kwa kadiri kwamba alikuwa akifasiri sifa za Mwenyezi Mungu kidhahiri na kimaanda ambapo alidai kwamba Mungu ana mwili sawa na mwili wa binadamu. Ni mashuhuri kwamba siku moja alipanda kwenye mimbar na kusema: "Mwenyezi Mungu huteremka duniani kutoka mbinguni kama ninavyoteremka mimi hapa." Hapo akawa anawaonyesha watu alilokusudia kwa kuteremka ngazi moja kwenye mimbar hiyo. Wanazuoni waliokuwa hapo walikasirishwa sana na jambo hilo na wakawa wanamkosoa na kumkemea vikali.

Ibn Taymiyya alidai kwamba kuzuru makaburi matukufu ya Mtume (saw) na Maimamu watoharifu (as) ni bida' na hivyo akahalalisha kumwagwa damu ya watu wanaozuru makaburi hayo. Aliwakufurisha Waislamu wengi kuhusiana na suala hilo. Aliwashajiisha wafuasi wake wawakufurishe Waislamu waliokuwa wakizuru makaburi ya viongozi hao wema wa Uislamu na hasa Mashia kwa kadiri kwamba aliamua kushirikiana na jeshi la Mongolia katika kuwaua Mashia wa Kidruze katika eneo la Kasravan nchini Lebanon. Alikubali utawala wa Wamongolia katika hali ambayo Aya ya 141 ya Surat an-Nisaa inakemea na kukataza jambo hilo kwa kusema: ....wala Mwenyezi Mungu hatawapa makafiri njia ya kuwashinda Waumini.

Ibn Taymiyya na wafuasi wake walihalalisha umwagaji damu za Waislamu na uporaji wa mali zao katika hali ambayo Mtume Mtukufu (saw) alisisitiza mara nyingi kwamba kila mtu anayetamka kalima ya "La Ilah Ila Allah" huwa ni Mwislamu na kwa mujibu wa Qur'ani tukufu anapasa kunufaika na rehema, upendo na urafiki wa Waislamu wenzake na wala si kukabiliwa na uadui na chuki.

Kuenezwa kwa fikra potovu na hukumu zinazokwenda kinyume na mafundisho ya Uislamu halisi kulipelekea maulama na wanazuoni wa Kiislamu kutoa mara nyingi hukumu za kukamatwa na kuzuiliwa kwake gerezani. Mwishoni mwa umri wake alifungwa katika jela moja mjini Damascus na hatimaye akaaga dunia mwaka 728 Hijiria (1327 Hijiria) akiwa kwenye jela hiyo hiyo.

***********

Takriban, karne nne baada ya kuaga dunia Ibn Taymiyya huko Hijaz, mtoto alizaliwa katika moja ya koo za kabila la Tamim ambalo lilikuwa likifuata madhehebu ya Hambal naye akapewa jina la Muhammad. Baba yake alijulikana kwa jina la Abdul Wahhab, na alikuwa kadhi wa eneo la Uyaina huko Najd ambapo babu yake pia alikuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa mji huo. Baada ya kupata mafunzo ya msingi ya kidini katika miji ya Madina na Basra, Muhammad ibn Abd al-Wahhab taratibu alianza kujifunza fikra za Ibn Taymiyya na hapo akaanza kupinga itikadi za Waislamu.

Hutuba na matamshi yake ya kidini yaliwaudhi sana walimu, baba na ndugu yake ambao wote walikuwa wakiyakemea na kumtaka ajiepushe nayo. Pamoja na hayo lakini majivuno na kiburi alichokuwanacho vilimzuia kukubali ukweli na ushauri kutoka kwa mtu yeyote na hilo likawa linamfanya awe anawatwisha watu wengine fikra zake potovu. Ni kiburi hicho ndicho kilimfanya afumbie macho ukweli kutoka kwa wenzake na kukabiliana nao kwa msingi wa ukaidi na uadui. Walimu wake walikuwa wakimnasihi ajiepushe kutoa maoni na kuzungumzia mambo ambayo hakuwa na elimu wala ujuzi nayo na kukubali maoni ya wasomi lakini bado hakukubaliana na suala hilo.

*************

Maisha ya Muhammad ibn Abd al-Wahhab yalisadifiana na zama za kuenea nguvu na udhibiti wa madola makuu ya dunia na hasa Russia na Uingereza katika pembe tofauti za dunia ambapo madola hayo yaliuchukulia Uislamu na Waislamu kuwa kikwazo kikuu katika njia ya kufikia malengo yao haramu katika nchi zilizolengwa kukoloniwa. Hivyo utawala wa Uingereza uliazimia kutafuta njia za kukabiliana na adui wake huyo sugu kwa namba ambayo ingeliugharimu kiwango cha chini zaidi cha fedha, nguvukazi na wakati. Kwa msingi huo uliamua kuwalea watu ambao baada ya kuwafundisha lugha ya Kiarabu, sheria na hata desturi na mila za Waislamu uliwatuma katika nchi za Kiislamu kwa shabaha ya kubadilisha fikra na maisha ya Waislamu. Watu hao walikuwa na jukumu maalumu la kuvuruga uthabiti wa ufalme wa Uthmania na kusababisha mivutano na migawanyiko katika umma wa Kiislamu. Mmoja wa majasusi hao waliopewa mafundisho ya kuibua fitina na migawanyiko katika Umma wa Kiislamu ni mtu anayejulikana kwa jila na Hempher ambaye amechapisha kumbukumbu zake katika kitabu alichokipa jina la 'Memoirs of Mr. Hempher.' Humpher ambaye alipenya na kuishi miongoni kwa Waislamu kwa jina bandia la 'Muhammad' alijuana na kufahamiana na Muhammad ibn Abd al-Wahhab mjini Basra nchini Iraq. Baada ya kujuana kwa karibu na Muhammad ibn Abd al-Wahhab, fikra na nafasi ya familia yake akafikia yakini kwamba alikuwa amempata mtu aliyefaa ambaye angeweza kufanikisha malengo yake yenye sumu na maovu katika Umma wa Kiislamu.

Hempher, jasusi wa Uingereza katika nchi za Mashariki ya Kati

************

Hempher taratibu alianza kumshawishi Ibn Abd al-Wahhab aue idadi kubwa ya Waislamu kwa sababu kwa madai yake walikuwa wamekiuka 'misingi muhimu ya Uislamu' na hivyo kuwa mushrikina na murtadi waliotoka nje ya Uislamu. Ili kumfanya Muhammad ibn Abd al-Wahhab ajiamini na kuwa na ujasiri zaidi katika kubainisha misimamo na fikra zake, Hempher alimdanganya kwamba alikuwa amemwona Mtume ndotoni akimbusu machoni huku akimwambia: 'Wewe ni mkubwa zaidi.' Kisha alimtaka Muhammad ibn Abd al-Wahhab amrithi Mtume kwa ajili ya kuunusuru Uislamu kutokana na 'bida' na 'imani zisizo na msingi'. Hadaa na uongo huo mkubwa wa Hempher ulimtia kiburi na maringo zaidi Ibn Abd al-Wahhab kiasi cha kumfanya athubutu kuanzisha kundi jingine jipya katika Uislamu.

Katika kumbukumbu zake, Hempher anamtaja Ibn Abdul Wahhab kuwa mtu anayeyumbayumba kifikra, katili, mwenye hasira kali, mwenye kiburi, asiye na elimu na fasidi kimaadili. Alifanya utaratibu wa Ibn Abdul Wahhab kuwaoa kwa muda wanawake wawili majasusi wa Uingereza. Wa kwanza alikuwa Mkristo kwa jina bandia la Swafiyya ambaye aliishi naye katika miji ya Basra na kisha Isfahan nchini Iran. Wa pili alikuwa mwanamke wa Kiyahudi kwa jina la utani "Asia" ambaye alimuoa huko Shiraz.

*********

Ama kuhusu ni vipi kujuana Hempher na Muhammad ibn Abd al-Wahhab kulipelekea kuasisiwa kundi jipya la kuchochea fitina, migawanyiko na mauaji katika Uislamu kwa jina la Uwahabi na taathira za jambo hilo katika ulimwengu wa Kiislamu, ni suala ambalo tumepanga kulijadili katika vipindi vyetu vinavyokuja Inshallah.

Basi hadi wakati huo panapo majaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.