Jumanne tarehe 22 Novemba 2022
Lei ni tarehe 27 Rabiulthani 1444 Hijria sawa na Novemba 22 mwaka 2022.
Siku kama ya leo miaka 203 iliyopita, alizaliwa Bi. Mary Ann Evans maarufu kwa jina la George Eliot, mwandishi wa riwaya na simulizi wa Uingereza. Akiwa mtoto mdogo, Evans alipendelea zaidi kusoma vitabu, na taratibu akaingia katika fani ya uandishi. Evans alikuwa na misimamo mikali ya dini ya Kikristo akiwa bado kijana. Hata hivyo misimamo hiyo ilipungua baadaye. Akiwa na umri wa miaka 30, Ann Evans alifasiri kitabu cha ‘Maisha ya Nabii Issa (as)’ (The Life of Jesus) kilichoandikwa na David Friedrich Strauss. Riwaya za Eliot zinahesabiwa kuwa miongoni wa vitabu maarufu zaidi vya karne ya 19 nchini Uingereza.
Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita, kufuatia kujiri kwa Vita vya Pili vya Dunia, nchi ya Lebanon ilijipatia uhuru wake. Lebanon ilitoka katika udhibiti wa utawala wa Othmania mnamo mwaka 1918 Miladia na kudhibitiwa baadaye na Ufaransa. Mwaka 1923 Miladia Ufaransa iliikalia nchi hiyo kwa idhini ya Umoja wa Mataifa. Tangu wakati huo Lebanon ikaanza kushuhudia siasa za ukoloni wa Mfaransa vikiwemo vitendo vya ubaguzi na machafuko. Nchi hiyo ilijipatia uhuru wake mwaka 1943.
Katika siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, John F. Kennedy, rais wa wakati huo wa Marekani aliuawa na raia mmoja wa nchi hiyo akiwa ziarani katika mji wa Dallas huko katika jimbo la Texas. Kennedy alizaliwa mwaka 1917 na alikuwa mwakilishi wa bunge la Marekani kwa duru tatu kuanzia mwaka 1946 na duru moja alikuwa mwakilishi wa seneti ya nchi hiyo. Siku kadhaa baadaye Lee Harvey Oswald ambaye alimuua Kennedy naye pia aliuawa na mtu aliyejulikana kwa jina la Jack Ruby na polisi ya Marekani ilidai kuwa mtu huyo vilevile aliaga dunia baadaye akiwa jela kutokana na maradhi ya saratani.
Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nambari 242 kuhusu Palestina. Miongoni mwa vipengee vya azimio hilo ni udharura wa kuondoka askari wa utawala ghasibu wa Israel katika ardhi zote za Palestina zilizokaliwa kwa mabavu Juni mwaka 1967 katika vita vya Waarabu na Israel, kusimamishwa operesheni za kijeshi na kutatuliwa kadhia ya wakimbizi wa Palestina kwa njia ya uadilifu. Hata hivyo kutokana na himaya ya pande zote ya Marekani na nchi za Magharibi kwa utawala ghasibu wa Israel, utawala huo haramu umekataa kutekeleza azimio hilo.
Katika siku kama hii ya leo miaka 51 iliyopita vikosi vya jeshi la Uingereza viliondoka Ghuba ya Uajemi baada ya kulikalia kwa mabavu eneo hilo kwa takriban karne mbili. Baada ya kudhoofika sana kwa Uingereza na kuanguka kwa ufalme wake kutokana na Vita vya Pili vya Dunia, pamoja na harakati nyingi za wananchi na kupata uhuru makoloni kadhaa ya Uingereza, mnamo 1968, serikali ya nchi hiyo ilitangaza sera ya kuondoka mashariki mwa Mfereji wa Suez. Kulingana na Waingereza, eneo hilo lilijumuisha Ghuba ya Uajemi, Bahari ya Oman, Singapore, Malaysia na maeneo mengine kadhaa. Hata hivyo, kabla ya kuondoka kwenye Ghuba ya Uajemi, London ilijaribu kuchukua hatua kutimiza malengo yake haramu na kuibua migawanyiko katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na kuimega na kujitenga Bahrain na Iran.
Katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari, faqihi na marjaa mkubwa wa Kishia. Akiwa na umri wa miaka 20, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Najaf, Iraq na kustafidi na elimu kutoka kwa wasomi wakubwa kama vile Muhaqqiq Khorasani, Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi, Shariat Isfahani na Muhaqqiq Naaini. Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari alielekea mjini Arak, Iran katika kipindi cha kuasisiwa chuo cha hauza cha mji huo na kujishughulisha na ukufunzi. Baadaye msomi huyo alishirikiana na Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Hairi katika shughuli za tablighi na baada ya kuasisiwa hauza ya Qum, chini ya usimamizi wa Ayatullah Hairi Yazdi, Ayatullah Ahmad Khansari alikuwa imamu wa Swala ya jamaa katika chuo cha Faiziya mjini humo. Alishirikiana bega kwa bega na wanazuoni wa Kiislamu wakiongozwa na hayati Imam Ruhullah Khomeini katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya utawala muovu wa Shah. Msomi huyo amelea ma lufunza wasomi wakubwa kama Ayatullah Murtadha Mutahhari, Imam Musa Sadr na Sayyid Ridha Sadr. Mwaka 1370 Hijiria, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Tehran na kuwa imamu wa swala ya jamaa katika msikiti maarufu wa ‘Sayyid Azizullah’. Ameandika vitabu vingi katika taaluma za sheria na teolojia ya Kiislamu.