Feb 19, 2023 07:55 UTC
  • Mafanikio ya kisayansi ya Iran baada ya mapinduzi ya Kiislamu (2)

Karibuni katika makala hii maalumu ya sayansi na teknolojia ambayo inaangazia mafanikio makubwa ya Iran katika uga wa sayansi na teknolojia tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu miaka 44 iliyopita.

Mfano mwingine wa maendeleo ya kisayansi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kukua kwa kasi katika uga wa anga ya juu au anga ya mbali. Iran inashikilia nafasi ya kwanza katika eneo la Asia Magharibi katika uzalishaji wa sayansi ya anga.

Sekta ya anga ya juu inachukuliwa kuwa moja ya vipengele vya nguvu ya nchi yoyote, na katika miaka ya hivi karibuni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepiga hatua za kimaendeleo katika uga wa kufikia teknolojia ya anga ya juu. Katika ramani ya kina ya kisayansi ya nchi, uwanja wa anga unazingatiwa kama moja ya nyanja muhimu za teknolojia kwa maendeleo ya nchi na ni moja ya teknolojia mpya na za kisasa.

Sekta ya anga ya Iran

Sekta ya anga ya juu ya Iran inaweza kutathminiwa kwa mitazamo miwili ya ndani na kimataifa. Kwa mtazamo wa ndani, Iran ilikuwa na idadi ndogo ya antena na vifaa vya kupokea mawimbi ya satelaiti kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, na taarifa za kiufundi za ndani kuhusu satelaiti zilikuwa sufuri.  Kwa hiyo, nchi ililazimika kupokea taarifa za satalaiti kutoka  nchi chache zilizokuwa na uwezo huo.  Lakini baada ya kuanza vita vya miaka minane vya kujihami kutakatifu wakati Iraq ilipoanzisha uchokozi dhidi ya Iran mwaka 1980, Iran iliamua kuendeleza teknolojia ya anga kwa ajili ya ulinzi wa nchi. Pia, kwa msaada wa wahitimu wa chuo kikuu, wataalamu wa ndani ya nchi walifanya kazi kwa bidii katika kadhia ya uundaji satelaiti.

Tofauti kuu kati ya mpango wa anga ya juu wa Iran na nchi nyingine za eneo la Magharibi mwa Asia ni kwamba Iran imeegemea kwenye uwezo wake wa ndani na imenufaika na teknolojia yake ya ndani. Kutokana na mipango na juhudi za wataalamu wa Iran, hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu imefikia kiwango cha uwezo mkubwa katika uga wa satelaiti za mawasiliano ya simu na picha ambazo hazihitaji tena msaada wa kigeni na ina uwezo wa kukidhi mahitaji ya nchi katika uwanja huo.

Hivi sasa Iran ni  miongoni mwa nchi 9 duniani ambazo zina teknolojia ya utengenezaji wa satelaiti. Si hayo tu bali Iran pia imefikia kiwango cha uwezo katika uga wa kujiundia kikamilifu roketi za kubeba satelaiti na hali kadhalika imeweza kujenga vituo vya kurusha satalaiti katika anga za juu. Kwa msingi huo Iran haihitajii msaada wowote wa kigeni katika kadhia ya kuunda na kurusha satalaiti katika anga za mbali.

Isa Zarepour, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Iran anasema hivi kuhusu maendeleo ya kuvutia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uga wa anga ya juu na kukuza nafasi ya Iran: Kwa juhudi za wanasayansi waaminifu na wenye kujitolea wa Iran ya Kiislamu, Iran imepanda kutoka nafasi ya 45 mwaka 1996 hadi ya 11 duniani mwaka 2017. Aidha amesema kuwepo mipango maalumu kati ya miaka ya themanini hadi mwanzoni mwa miaka ya tisini katika kutafuta vipaji na kuvutia vijana wasomi na waliobobea, kwa kutegemea maarifa na uvumbuzi, kulipelekea kuchukuliwa hatua imara kama vile kurushwa kwa satelaiti ya Omid, roketi ya kubeba satelaiti ya Safir Omid mnamo 2008, na baada ya hapo Iran ikajiunga na kundi la nchi chache  zenye uwezo wa kujiundia na kujirushia satalaiti katika anga za juu.

Mpango wa miaka 10 wa Shirika la Anga la Iran

Shirika la Anga za Juu la Iran hivi karibuni lilianza mchakato wa kutekeleza mpango wa kimkakati wa anga za juu wa miaka 10. Kwa mujibu wa mpango huo, katika kipindi cha miaka 10 ijayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itakuwa kitovu cha kieneo katika maendeleo ya teknolojia ya anga za juu na utoaji wa huduma za kurusha satelaiti katika anga za juu.

Roketi la kubeba satelaiti ya Safir Omid la Iran

Kwa msingi huo, maendeleo ya miundombinu ikiwa ni pamoja na uzinduzi wa vituo vya ardhini vya kupokea data za satelaiti, kuharakisha mchakato wa kubuni na kutengeneza satelaiti za mawasiliano ya simu, kuzindua satelaiti zenye uwezo wa kupiga picha za kiwango cha juu, kusonga kwa mwelekeo wa mwingiliano wa kimataifa na kutekeleza miradi ya pamoja, kutekeleza utafiti na miradi inayoangazia maendeleo ya miundombinu, kupanga na kuzindua satalaiti zenye uzito wa juu ni miongoni mwa nukta muhimu za mpango wa anga wa miaka 10 wa Iran.

Kutokana na mipango na juhudi za wataalamu wa Iran, hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu imefikia kiwango cha uwezo mkubwa katika uga wa satelaiti ambapo haihitaji tena msaada wa wageni katika uwanja huo. Hivi sasa wataalamu wa Iran katika uga wa satelaiti wana uwezo wa kukidhi mahitaji ya nchi na kuifanya kuwa miongoni mwa nchi 9 ambazo zina teknolojia ya utengenezaji wa satelaiti.

Mbali na kuunda satalaiti, Iran pia imeweza kupata mafanikio makubwa katika kujiundia roketi za kubeba satelaiti na hivyo hahitaji tena msaada wowote wa kigeni katika uga huu.

 Orodha ya baadhi ya mafanikio ya Iran katika anga za juu

Mwaka 2010, Iran ilizinduia kwa mafanikio roketi ya kubeba satalaiti ijulikanayo kama "Explorer Rocket 3". Aidha mwaka 2012 Iran ilirushwa kwa mafanikio satelaiti ya  "Navid" kwenye anga za mbali ambapo ilitekeleza majukumu yake kwa mafanikio.

Mnamo 2013, satelaiti za "Nahid" na "Zuhre" zilizinduliwa katika maonyesho ya kitekelnolojia. Baada ya muda usio mrefu  satelaiti mbili za  "Tadbir" na "Ghuba ya Uajemi" zilizinduliwa.

Mnamo mwaka wa 2015, satelaiti nyingine ya Iran iliyopewa jina la "Fajr" ilirushwa kwa mafanikio katika anga za mbali kwa kutumia roketi la kubebea sataliti la "Safir" na iliweza kutekeleza majukumu yake kwa mwafanikio

Mnamo 2015, satelaiti ya mawasiliano ya "Nahid 1" ilizinduliwa kwa mara ya kwanza. Hali kadhalika mwaka wa 2019, satelaiti ya "Payam" ilirushwa katika anga za juu kwa kutumia roketi la kubebea satalaiti la "Simorgh". Hata hivyo kulitokea hitilafu za kiufundi na Payam haikuweza kufika kwenye obiti kama ilivyotarajiwa.

Mnamo mwaka 2019, satelaiti ya "Noor-1" ikiwa ni satelaiti ya kwanza ya kijeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ilirushwa kwa mafanikio katika anga za mbali kwa kutumia roketi la kubebea satalaiti kutoka chombo cha satelaiti cha "Qased." Satalaiti hiyo ilirushwa katika anga za juu kupitia kituo kipya cha kurushia satalaiti cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika jangwa la kati mwa Iran na ikaweza kufika katika umbali wa kilomita 424 kutoka ardhi ya sayari ya dunia.

Mnamo Machi 2022, satelaiti ya pili ya kijeshi ya Iran inayoitwa Noor-2 ilirushwa katika anga za mbali kwa kutumia roketi ya kurusha satalaiti ya Qased ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na ikaweza kufika kwa mafanikio katika eneo la umbali wa kilomita 500 kutoka sayari ya dunia.

Mafanikio ya hivi karibuni hususan mfumu mzima wa kuunda na kurusha satalaiti ni nukta zinazoashiria kuimarika hadhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mbele ya waangalizi wa kimataifa.

Bila shaka katika miaka yote hii maadui hasa Marekani na utawala wa Kizayuni daima wamekuwa wakionyesha wasiwasi wao kuhusu maendeleo ya Iran katika uga wa anga za juu. Gazeti la Kizayuni la "Haaretz" limeandika kuhusiana na hilo: "Maafisa wa Israel wanasema kuwa Iran ina uwezo wa kutumia teknolojia ya anga za juu kuimarisha kwa kiasi kikubwa makombora yake ya kawaida”.

Wakuu wa utawala wa Kizayuni pia wamedai kuwa makombora mawili ya "Zol-Janah" na "Qaim -100" ambayo Iran iliyaunda kwa ajili ya kurusha satelaiti kwenye anga za mbali yana tekenolojia ambayo inaweza kutumiwa kwa madhumuni ya kijeshi."

Nukta ya mwisho ni kwamba sekta ya anga za juu ni muhimu sana kwa maendeleo ya uchumi wa nchi na inaweza kutumika katika nyanja za kilimo, mazingira, huduma na sekta zingine nyingi. Umuhimu maalumu wa teknolojia ya anga za juu na ulazima wa kutumia teknolojia hii ili kurahisisha maisha ya watu ni jambo lisilopingika. Katika miaka ya hivi karibuni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeonyesha mazingatio maalum kwa sekta hii na kuweza kuendeleza sekta hii kwa juhudi za vijana wasomi na wenye imani wa Iran kiasi kwamba sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kushika nafasi ya kwanza katika sekta hii ya teknolojia ya anga za juu katika eneo la  Asia Magharibi na miongoni mwa nchi za Kiislamu duniani.