Hakika ya Uwahabi 15
Kama mngali mnakumbuka tulisema katika vipindi viwili vilivyopita kwamba watenda-jinai za kutisha huamua kusema na kukariri uongo mkubwa ili kukwepa kuangamia au kunaswa katika mtego wa sheria. Husema uongo mkubwa kadiri kwamba hata wao wenyewe hushawishika kuamini kuwa wanachokisema si uongo tena bali ni ukweli mtupu.
Bismillahir Rahmanir Raheem. Hamjambo wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.
Kama mngali mnakumbuka tulisema katika vipindi viwili vilivyopita kwamba watenda-jinai za kutisha huamua kusema na kukariri uongo mkubwa ili kukwepa kuangamia au kunaswa katika mtego wa sheria. Husema uongo mkubwa kadiri kwamba hata wao wenyewe hushawishika kuamini kuwa wanachokisema si uongo tena bali ni ukweli mtupu.
***************
Kabla ya kuanza Vita vya Pili vya Dunia, kulijiri mazungumzo kati ya Winston Churchill, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza na Theodore Roosevelt, rais wa wakati huo wa Marekani kuhusiana na jinsi ya kuunda umoja kati ya nchi hizo mbili kwa ajili ya kuuangamiza Uislamu na kuunga mkono Wazayuni. Waingereza walibuni ufalme wa Mawahabi huko Saudi Arabia na kuuarifisha kuwa sehemu ya ulimwengu wa Kiislamu na kisha Wamarekani wakabuni msururu wa uongo kwa ajili ya kufunika uongo huo mkuwa wa Waingereza.
Takriban tangu mwaka 1950 Miladia, na kwa msaada wa Marekani, Mawahabi walianzisha kampeni kubwa ya kujenga misikiti na shule za kidini pamoja na kutuma wahubiri wa itikadi zao katika pembe tofauti za dunia. Mawahabi walitekeleza siasa za makusudi za kuwaalika nchini Saudia walimu, waandishi wa magazeti na shakhsia wa kidini na kuwamiminia mapesa mengi kwa ajili ya kuwashawishi wakubali na kueneza fikra zao katika ulimwengu wa Kiislamu. Mbali na hayo walialika, kufadhili na kuwasajili wanachuo wengi katika vyuo vikuu vyao. Msimu wa Hija pia ulichukuliwa kuwa fursa nzuri ya kueneza propaganda na fikra za Mawahabi katika nchi na jamii za Waislamu.
Chombo kikuu cha kuenezwa propaganda na fikra za Mawahabi kinaitwa Rabitat al-Aalam al-Islami ambacho kiliasisiwa katika mji mkuu wa Saudia, Riyadh mnamo mwaka 1974. Taasisi hiyo ambayo ina matawi yake katika nchi karibu zote za Kiislamu, mbali na kujenga misikiti, shule za kidini na kutuma wahubiri wa Kiwahabi katika nchi tofauti za dunia, pia inajishughulisha na huduma za kijamii kama kujenga mahospitali, kuchapisha majarida, vitabu na magazeti pamoja na kuanzisha mashirika ya misaada ya kibinadamu ili kwa njia hiyo iweze kueneza fikra za uwahabi duniani. Kitengo muhimu zaidi cha taasisi hiyo ni kile kinachoitwa 'Kitengo cha Kupambana na Kuenea Ushia.' Lengo kuu la kitengo hicho ni kuibua mifarakano na migawanyiko kati ya Waislamu, mifarakano na hitilafu ambazo zimekuwa zikiibuliwa mara kwa mara kati ya Mashia na Masuni, suala ambalo kwa hakika limekuwa likitumiwa na Marekani na Uingereza kwa ajili ya kueneza uchokozi na uvamizi katika nchi za Kiislamu.
Hati ya muongozo ya Rabitat al-Aalam al-Islami inasema wazi kwamba: "Taasisi hii inafanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuwavutia watu wema watakaosaidia katika mapambano dhidi ya fikra za kigeni na watu wanaopinga Uislamu. Taasisi hii pia imejenga hatua na shughuli zake katika msingi wa kueneza ujumbe na misingi ya Uislamu ili kuweza kuvunja njama ambazo zinalenga kukandamiza itikadi za watu na kuibua mifarakano miongoni mwao."
Bila shaka maneno hayo yamepangwa kwa njia na lugha maalumu. Maneno yaliyotumika humo yamekusudiwa kufikia malengo ambayo si rahisi kwa mtu wa kawaida kuyajua. Ili kufahamu vyema makusudio ya maneno hayo, inatosha kupitia harakaharaka maneno yaliyotamkwa na Muhamman bin Abdul Wahhab, ambaye ni mwanzilishi wa fikra za Mawahabi. Anasema: " Sisi tunamchukulia kuwa kafiri, mtu yeyote ambaye wito wetu (Mawahabi) umemfikia na akabainikiwa wazi na dalili na hoja zetu lakini pamoja na hayo akawa anashikilia itikadi zake kutokana na kiburi na ukadi wake."
Sasa tunapoirejea hati ya Rabitat al-Aalam al-Islami, tunatambua kuwa kusudio la 'watu wema' katika hati hiyo ni wale waliokubali na kufuata fikra za Mawahabi, na wanaotajwa kuwa ni wageni wanaopinga fikra za Uislamu kwa hakika ni wale wanaopinga fikra za Kiwahabi, ibara ambayo kwa kweli inawajumuisha Mashia na Masuni. Ni wazi kuwa misingi ambayo inakusudiwa kuenezwa na taasisi hiyo ni misingi na fikra za Uwahabi na sio Uislamu. Ama kwa kweli ni muhimu kuzingatia zaidi hapa ibara iliyotumika katika sehemu ya mwisho ya hati hiyo inayosema kwamba Mawahabi wana jukumu la kuvunja njama zinazodaiwa kuibua mifarakano miongoni mwa Waislamu. Swali tunalopasa kujiuliza hapa ni kuwa je, ni vipi Mawahabi wakufurishaji ambao wanajiona kuwa ndio Waislamu pekee, wanataka kuzuia kuibuka mifarakano katika Umma wa Kiislamu? Huenda maana ya mifarakano hiyo inayodaiwa na Mawahabi matakfiri ikawa inatofautiana na ile inayofahamika na Waislamu.
**************
Essam al-Emmad, mmoja wa mamufti wa Kiwahabi ambaye karibuni amejitenga na fikra za Mawahabi na kujiunga na Mashia anasema: 'Mawahabi hawaamini hata kidogo suala la kukurubishwa pamoja madhehebu za Kiislamu.' Madai hayo yanathibitishwa na watu wengi akiwemo Muhammad Kubari mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa Saudi Arabia ambaye ameandika kitabu kizima kinachopinga fikra ya kukurubishwa pamoja madhehebu za Kiislamu. Vilevile Sheikh Abdul Aziz bin Baz, Mufti Mkuu wa Mawahabi wa Saudi anasema kuhusu suala hilo: "Hakuna uwezekano wowote wa kuwepo ukuruba baina ya Mashia na Ahlu Suna kwa sababu hakuna mfungamano wowote uliopo kati ya pande mbili hizo..... Kama ambavyo haiwezekani kuwakutanisha Ahlu Sunna na Mayahudi, Wakristo na waabudu masanamu....Kuwaunganisha Mashia na Ahlu Suna pia ni jambo lisilowezekana."
Laiti kungelikuwepo na mtu ambaye angemuuliza mufti huyu wa Kiwahabi swali lifuatalo: "Je, nyinyi ambao mnadai kuwa Mayahudi ni binamu zenu na daima mnafanya juhudi za mchana na usiku kwa ajili ya kuleta umoja na amani kati ya Waarabu na Israel na kutia saini mikataba mingi katika uwanja huo, ni vipi mtapinga kukurubiana Ahlu Suna na Mashia, katika hali ambayo pande mbili hizi zinakubaliana kuwa na Mwenyezi Mungu mmoja, Kibla kimoja na Mtume mmoja na mafungamano yao ya kidini ni mengi zaidi kuliko ukuruba wao na Mayahudi?
Tukiachilia mbali mitazamo, fatwa na vitabu ambavyo vimeandikwa na mamufti na wasomi wa Kiwahabi wa Saudi Arabia katika kupinga umoja na mshikamano wa Mashia na Masuni, ni wazi kuwa hatua na uchochezi wa vita ambao unaenezwa na makundi yanayofungamana na fikra za Mawahabi, unathibitisha wazi kuwa fikra hizo ndizo zinazoeneza mifarakano na migawanyiko katika Umma wa Kiislamu. Ukweli wa mambo ni kwamba fikra za makundi mengi ya kigaidi na kitakfiri yanayofungamana na Mawahabi kama vile Daesh na al-Qaida zinatokana na mitazamo na itikadi za pote hilo linalojifaharisha kuwa na uhusiano na Mayahudi.
***************
Ali bin Khudhair, mmoja wa wasomi wa kitakfiri na Kiwahabi anadai kuwa vitabu vya Muhammad bin Abdul Wahhab ni kati ya vitabu bora zaidi naye Abu Mus'ab Sury, mwanafikra mwingine wa kitakfiri na ambaye tayari amejiunga na kundi la kigaidi la al-Qaida anasema kuwa sera inayofuatwa na kundi hilo inatokana na fikra za Ibn Taymiyya na Uwahabi. Kwa mtazamo wake, makundi ya kigaidi na kitakfiri yanafuata sisa za kisheria kutoka kwa Ibn Taymiyya na fiqhi na itikadi kutoka kwa Uwahabi, yaani Muhammad bin Abdul Wahhab.
Abu Muhammad Maqdisi, mmoja wa viongozi wa kifikra wa al-Qaeda na Jabhat al-Nusra, anakiri katika kitabu chake alichokipa jina "Mazungumzo na Jarida la Al-Asr" kwamba yeye ni mmoja wa wanafunzi wa shule ya Mawahabi na kwamba alifunzwa na Abd al-Aziz bin Baz, Ibn Uthaymiyn na Sheikh Albani.
Abu Musab al-Zarqawi, ambaye anakiri kwamba alihusika na vitendo vya mabavu, madawa ya kulevya na pombe alipokuwa kijana, anaweza kuchukuliwa kuwa ndiye aliyehusika kimsingi katika kuibuka kundi la kigaidi la al-Qaeda nchini Iraq. Anamtetea Muhammad bin Abdul-Wahhab katika moja ya matamshi yake na hata kumtaja kuwa mfano wa mama aliye na huruma kubwa kwa mwanaye kuhusiana na masuala ya dini.
Osama bin Laden, kiongozi mashuhuri zaidi wa al-Qaeda, anahusisha fatwa zake na maneno ya Ibn Taymiyyah na Muhammad bin Abd al-Wahhab na kuwataja kuwa warekebishaji wakubwa wa dini na wafufuaji wa sharia.
**************
Wachambuzi wengi wa nchi za Kiarabu wanaamini kuwa chimbuko kuu la itikadi za kigaidi na kitakfiri linapatikana Saudi Arabia, hivyo jukumu la jinai yoyote inayofanywa na makundi hayo ya kigaidi linapaswa kubebwa na serikali ya Saudia ambayo si tu kwamba haijawahi kutangaza kujitenga na fikra hizo, bali siku zote hutumia utajiri wake kuzieneza.
Abdul Bari Atwan, mmoja wa wachambuzi mashuhuri wa ulimwengu wa Kiarabu, anaamini kwamba Daesh au kwa jina jingine ISIS inatekeleza kikamilifu fikra za Uwahabi.
Kwa maoni yake, ufundishaji wa vitabu vya Ibn Abd al-Wahhab katika shule za Saudia ndio msingi wa kukuzwa fikra na misimamo mikali ya Uwahabi na kujiunga vijana wa Saudia na makundi hayo ya kigaidi. Amethibitisha madai yake kwa kutegemea matokeo ya kura ya maoni iliyofanywa katika uwanja huo. Utafiti huo ambao ulifanywa nchini Saudi Arabia mwaka 2014, ulionyesha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya vijana wa nchi hiyo wanaamini kuwa tabia na mienendo ya Daesh inaendana na viwango na sheria za Uislamu.
Umuhimu wa suala hili unaongezeka pale tunapotambua kwamba Saudi Arabia inatekeleza mitaala ya masomo inayotumika katika shule na vyuo vyake vya ndani katika nchi nyingine nyingi za Kiislamu, jambo ambalo halijakuwa na matokeo mengine isipokuwa kuibuka magaidi wanaodai kuwa ni Mujahidina katika pembe tofauti za dunia. Magaidi ambao bila shaka tutawafahamu zaidi katika vipindi vyetu vinavyokuja.