May 27, 2023 04:46 UTC
  • Sura ya Muhammad, aya ya 25-28 (Darsa ya 933)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 933 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 47 ya Muhammad. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 25 ya sura hiyo ambayo inasema:

إِنَّ الَّذِينَ ارْتَدُّوا عَلَىٰ أَدْبَارِهِم مِّن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُمُ الْهُدَى ۙ الشَّيْطَانُ سَوَّلَ لَهُمْ وَأَمْلَىٰ لَهُمْ

Kwa hakika wanaoupa mgongo uongofu baada ya kwisha wabainikia, Shetani amewapambia mabaya yao na kuwaghuri kwa matarajio marefu.

Katika darsa iliyopita tulizungumzia watu wanafiki na wenye imani dhaifu walioacha kutafakari na kuzitaamali aya za Qur’ani, ambao kwa mujibu wa kitabu hicho cha mbinguni ni kama kwamba wana kufuli kwenye nyoyo zao. Aya hii tuliyosoma inasema, mtu mwenye kuupa mgongo uongofu wa Qur’ani na mwongozo wa Bwana Mtume SAW anaishia kumfuata shetani. Ni kawaida kwamba shetani huanza kwanza kumpambia mtu matendo maovu ili yaonekane mazuri mbele ya macho yake na kisha ndipo humchochea ili ayafanye. Na hiyo ndio sababu ya mtu kuona fakhari kwa maovu anayofanya. Mtu kama huyo, huwa anajipangia mustakabali wake kwa ndoto na matarajio ambayo siku baada ya siku humweka mbali zaidi na njia ya haki na kuufanya mgumu zaidi uwezekano wa yeye kurejea kwenye njia sahihi iliyonyooka. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kinyume na dhana waliyonayo wanafiki ya kujiona watu waliotaalamika na kuerevuka, kwa mtazamo wa Qur’ani, wao ni watu wenye fikra finyu na mawazo mgando, ambao wameiacha njia yenye nuru ya uongofu na kurejea kwenye giza la dhalala na upotofu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kufuata mtu wasiwasi anaotiwa na shetani ni miongoni mwa mambo yanayoidhuru na kuiharibu imani yake, na hatima ya hilo ni kuwa mbali na njia ya haki na kuishia kuwa na mwisho mbaya. Halikadhalika, aya hii inatutaka tujue kwamba, ujuzi na uelewa tu wa haki na ukweli hautoshi, bali inatakiwa mtu apambane pia kwa dhati na wasiwasi wa shetani. Wa aidha aya hii inatufunza kuwa, kuyapamba na kuyafanya mabaya yaonekane mazuri na kumjaza mtu ndoto na matarajio mengi na makubwa ni silaha na nyenzo zinazotumiwa na shetani.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 26 ya sura yetu ya Muhammad ambayo inasema:

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَالُوا لِلَّذِينَ كَرِهُوا مَا نَزَّلَ اللَّهُ سَنُطِيعُكُمْ فِي بَعْضِ الْأَمْرِ ۖ وَاللَّهُ يَعْلَمُ إِسْرَارَهُمْ

Hayo ni kwa sababu waliwaambia walio chukia aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu: Tutakut'iini katika baadhi ya mambo. Na Mwenyezi Mungu anajua siri zao.

Aya hii inazungumzia mawasiliano yaliyokuwepo baina ya wanafiki na makafiri na kueleza kwamba, wanafiki wa Madina walikuwa wakiwaendea Mayahudi wa mji huo na kuwekeana nao ahadi ya kushirikiana na kuchukua hatua dhidi ya Waislamu, kwa baadhi ya mambo yaliyokuwa na maslahi ya pamoja kwao. Tab’an walikuwa wakijaribu kufanya mawasiliano hayo kwa siri ili Bwana Mtume na Waislamu wasijue. Lakini Qur’ani inasema: Mwenyezi Mungu ataufichua usaliti wao huo ili njama yao hiyo idhihirike na watu waweze kuwatambua. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, Waislamu wanatakiwa wawe na hadhari na wajue kwamba baadhi ya watu katika jamii ya Waislamu wana uhusiano na maadui na makafiri; na wako kitu kimoja na wao. Kundi la watu hao huwa liko tayari kuyatoa mhanga maslahi ya jamii ya Waislamu kwa ajili ya manufaa yao na ya maadui wa dini. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, uhusiano wa wanafiki na maadui si wa dhahiri; ni wa kimyakimya na wa kificho. Kwa hivyo inatakiwa viongozi wa jamii wawe macho na kutumia mbinu na nyenzo mwafaka ili kuweza kuyagundua mahusiano hayo ya siri. Vilevile aya hii inatutaka tutambue kwamba, Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa mambo yote ayafanyayo mtu kwa siri na kwa kificho; na kama mtu atakuwa na imani ya kweli juu ya jambo hilo basi ataacha kula njama dhidi ya wanadamu wenzake.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 27 na 28 ambazo zinasema:

فَكَيْفَ إِذَا تَوَفَّتْهُمُ الْمَلَائِكَةُ يَضْرِبُونَ وُجُوهَهُمْ وَأَدْبَارَهُمْ

Basi itakuwaje Malaika watakapo wafisha wakawa wanawapiga nyuso zao na migongo yao! 

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمُ اتَّبَعُوا مَا أَسْخَطَ اللَّهَ وَكَرِهُوا رِضْوَانَهُ فَأَحْبَطَ أَعْمَالَهُمْ

Hayo ni kwa sababu wao waliyafuata yaliyo mchukiza Mwenyezi Mungu na wakachukia yanayo mridhisha, basi akaviporomosha vitendo vyao.

Aya hizi zinaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya zilizotangulia kwa kubainisha hatima ya wanafiki hapa duniani na kusema: watu hao wataadhibika wakati wa kutolewa roho. Kwa sababu malaika wenye jukumu la kutoa roho za watu, kwanza watawaadhibu wanafiki hao, kisha ndipo watakabidhi roho zao. Kutolewa roho namna hiyo ni matokeo ya matendo na amali zao. Na sababu ni kwamba, watu hao hawakuwa wakifanya yale yanayompendeza Mwenyezi Mungu, bali kinyume chake, walikuwa wakikazania kutenda yale yanayomchukiza Yeye Mola. Ni kawaida kwamba katika vipindi tofauti vya maisha yetu, sisi sote hutokezewa na hali ya kufika njiapanda na kulazimika kuchagua moja kati ya machaguo mawili. Lakini kawaida ya watu wengi huwa ni kuchagua lile linaloendana na matashi na kuwadhaminia zaidi maslahi yao. Hali ya kuwa kwa mtazamo wa mafunzo na mafundisho ya Qur'ani, kipimo cha kutumia mtu muumini anapolazimika kuchagua moja kati ya njia mbili za kufuata maishani, si kushika ile inayokidhi matakwa na maslahi yake, bali ni kuzingatia na kupima ni ipi itamwezesha kupata au kukosa radhi za Mola wake. Yaani kile kinachomridhisha Allah SWT ndicho atakachofanya, hata kama hakitaendana na matashi na matakwa yake; na chochote kile kinachomchukiza na kumghadhibisha Mola atakiacha, hata kama ndicho kipendwacho na moyo wake na chenye kuiridhisha nafsi yake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kifo sio mwisho wa mwanadamu, bali ni kumalizika kipindi cha maisha yake ya hapa duniani, ambapo malaika huichukua moja kwa moja roho ambayo mtu alipewa mwanzo wa kuumbwa kwake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mauti ya mtu mnafiki na mwenye nyuso mbili huwa mazito na yenye kuandamana na madhila na mateso. Aidha aya hizi zinatutaka tujue kwamba, japokuwa mwanadamu yuko huru kuchagua njia ya kufuata, lakini inapasa akubali pia athari na matokeo ya chaguo lolote lile atakalofanya. Hapana shaka kuchagua linalompendeza na kumridhisha Allah SWT kutakuwa na matokeo mema na ya kheri, na kujikosesha radhi zake Yeye Mola kwa kufanya linalomchukiza kutakuwa na matokeo mabaya ya kumpatisha mtu mateso na adhabu kali. Halikadhalika aya hizi zinatuelimisha kuwa, amali na matendo ya mtu, hata kama kidhahiri yataonekana mazuri na yenye kuwapendeza watu, lakini kama hayatakuwa yenye kumridhisha Allah yatayeyuka na kutoweka tu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 933 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuwezeshe kufanya yanayomridhisha Yeye, yatakayotupatia radhi na Pepo yake tukufu, na atuepushe kutenda yanayomghadhibisha, yatakayokuwa sababu ya kukhasirika na kuharibikiwa katika dunia na akhera yetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../